05/09/2022
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Innocent Bashungwa amesema hataki kuona mawasiliano na mahusiano hafifu kati ya waganga wakuu wa mikoa,wakurugenzi wa halmashauri na taasisi za Dini ambazo zinatoa huduma za afya kwa wananchi.
Akizungumza leo Jumatatu Septemba 5 ,2022 jijini Dodoma wakati akifungua mkutano wa 85 wa Chama cha Madaktari wa Hospitali za Mashirika ya Dini(TCMA),Waziri Bashungwa amesema suala la mahusiano kati ya serikali na taasisi za dini ambazo utoa huduma za afya kwa wananchi ni muhimu.
Kauli hiyo imekuja kufuatia rais wa Chama cha Madaktari wa Kikristo nchini, Dk Paul Kisanga kueleza katika risala kuwa kuna baadhi ya halmashauri zimekuwa zikishindwa kuhuisha mikataba ya vituo vya afya vya kanisa hata pale ambapo bado kituo cha serikali hakijafikia kutoa huduma stahiki kwa wagonjwa.
Waziri Bashungwa amemwagiza Katibu Mkuu wa Tamisemi,Profesa Riziki Shemdoe hataki kuendelea kusikia mawasiliano hafifu kati ya waganga Wakuu wa Mikoa,Wakurugenzi na taasisi za dini ambazo zinatoa huduma kwa wananchi.