SASA NI RASMI DOGO RAMA MALI YA TWANGA PEPETA
Rais wa Twanga Pepeta, Chaz Baba amethibitisha kuwa mwimbaji Dogo Rama TBS amerejea nyumbani.
Akizungumza na Saluti5, Chaz Baba amesema wanatarajia kumtambulisha rasmi Dogo Rama ndani ya Twanga Pepeta Septemba 4.
"Tunafanya mazungumzo na ukumbi wa Kisuma 5G Temeke, ili tuandae tukio la kumkaribisha Dogo Rama ukumbini hapo Jumatano ya tarehe 4 mwezi ujao," ameleeza Chaz Baba.
Naye Dogo Rama alipoulizwa na Saluti5 juu ya habari za kurejea rasmi Twanga, alikiri kuwa jambo hilo limeisha na kilichobakia ni siku ya kuanza kazi.
Dogo Rama anarejea Twanga Pepeta baada ya miaka tisa tangu alipoihama mwaka 2015.
Alipitia bendi kadhaa ikiwemo Double M Plus, Ivory Band, Smart Band, Paris Band pamoja na Town Classic aliyoachana nayo wiki iliyopita.
Said Mdoe
23/8/2024
MAKAMUZI YA JIMMY MANZAKA JUKWAANI
Mfalme wa Rhumba, Jimmy Manzaka akifanya makamuzi ndani ya Town Classic.
Sio kuimba tu bali hata linapokuja suala la kushambulia jukwaa, Jimmy Manzaka yumo.
Hii ni jana usiku katika onyesho lake la pili tangu ajiunge na Town Classic.
Show ilifanyika maeneo ya Boko Magereza jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa GW Garden Park.
Said Mdoe
17/8/2024
DOGO RAMA AKACHA SHOW YA TOWN CLASSIC NA KUIBUKIA TWANGA PEPETA
Ratiba ya show ya Town Classic kwa siku ya jana ilionyesha wangekuwa Juliana Pub, Mbezi Beach, lakini mwimbaji wake tegemeo Dogo Rama akaibukia Twanga Pepeta.
Dogo Rama TBS akakwea jukwaa la Twanga Pepeta ndanii ya Small Planet, Tabata na kusalimia kisanii.
Mwimbaji huyo akaiambia Saluti5 kuwa bado kabisa hajaongea ila sasa ndio anakuja kunena, watu watege sikio.
Said Mdoe
16/8/2024
AYA 15 ZA SAID MDOE: TWANGA PEPETA HII SIO SAWA SAWA
Pengine hili nitakuwa nalirudia kwa mara ya tatu au zaidi, ni kuhusu nyimbo nyingi za dansi zinazoozea studio na mazoezini.
Dansi kwenye suala la kutoa ngoma mpya kwa wakati bado kuna kazi kubwa sana. Mimi siku hizi hata nikiona wasanii wa dansi wako mazoezini au studio wakipika kazi mpya wala sish*tuki.
Kati ya bendi ambazo sisiti kuzishutumu kwenye hili, ni Twanga Pepeta yenye zaidi ya robo karne kwenye gemu na inayomiliki robo na ushee ya mashabiki wa dansi hapa Tanzania.
Oktoba 15, 2023, Twanga Pepeta ilifanya onyesho maalum ndani ya ukumbi wa kisasa wa Warehouse, Masaki jijini Dar es Salaam.
Onyesho lilikuwa la kusikilizisha (Listening Party) mashabiki nyimbo mpya: "Kosa Langu" utunzi wake Saleh Kupaza, "Sawasawa" wa Msafiri Diouf na "Pisi Yangu" ambao umetungwa na Chaz Baba.
Hadi leo ni zaidi ya nusu mwaka, licha ya tungo hizo kupigwa sana jukwaani, hakuna wimbo wowote ulioachiwa hewani, matokeo yake Diouf kaamua kuhama na kibao chake cha "Sawasawa" na kwenda kukirekodi VDS Chama la Wana.
Twanga imezifanyia mazoezi ya muda mrefu hizi nyimbo, wasanii wamelipwa posho za mazoezi, pia kuna gharama za uchakavu wa vyombo, lakini mwisho wa siku kazi hazionekani au zinakwenda kutumika sehemu nyingine.
Najiuliza, menejimenti ya Twanga haijihurumii kwa hizo gharama za mazoezi zinazopotea bure? Vipi kuhusu wasanii ambao wameumiza vichwa kuweka michango yao kwenye nyimbo?
Katika bendi zetu za dansi, wimbo unapotengenezwa kwenye uwanja wa mazoezi, kuna mchango mkubwa kutoka kwa wasanii wengine unaokwenda kuboresha wazo la mtunzi.
Hivyo basi wimbo unapokaa muda mrefu bila kurekodiwa hadi ikafikia hatua ya mtunzi kuhama na tungo yake, maana yake ni kwamba wote waliochangia mawazo kwenye bendi ya awali wanakuwa wametwanga maji kwenye kinu.
Nimeona baadhi ya mashabiki wa Twanga Pepeta wameponda kitendo cha Diouf kuhama na "SawaSawa", lakini nani wa kulaumiwa? Aliyechelewa kurekodi kwa zaidi ya nusu mwak au aliye
Hiyo ni sauti ya Rama Igwe kupitia wimbo wake mtamu "Waka Waka"
Kwa kweli Saleh Kupaza anajua sana kuimba
KINDE MAKENGELE KUTAMBULISHWA BOGOSS LEO USIKU
Staa wa gitaa la solo, Kinde Makengele aliyetangaza kuachana na Waluguru Original ya Morogoro, ametua mkononi mwa rais wa vijana, Nyoshi el Saadat.
Naaam, Kinde Makengele atatambulishwa kama msanii mpya wa Bogoss Musica leo usiku ndani ya ukumbi wa TTG Lounge, Kimara Korogwe.
Kinde ameithibitishia Saluti5 kuwa ni kweli amejiunga na Bogoss na ataanza kazi rasmi leo usiku.
Msanii huyo mwenye mbwembwe nyingi jukwaani, ameiambia Saluti5 kuwa kule Waluguru Original amewaachia zawadi ya wimbo mpya "Plan B" ambao umesharekodiwa
"Nimetunga nyimbo mpya nyingi Waluguru ukiwemo "Plan B" ambao ni zawadi yangu kwao, lakini zingine ambazo hazijarekodiwa kama "Njaa" na "Sangoma" nitahama nazo," alifafanua Kinde ambaye mbali ya kutunga na kupiga solo, lakini pia ana uwezo kucharaza rhythm, bass, drums pamoja na kuimba.
Said Mdoe
4/5/2024
DOGO RAMA NI KAMA ALIZALIWA KWA AJILI YA TWANGA PEPETA ...angalia alivyoukandamizia Penzi Sigara Kali
Aliitumikia Twanga Pepeta kwa kiasi cha kama miaka sita tu, lakini akafanikiwa kuuaminisha umma wa wapenzi wa muziki kuwa yeye ndiye kiraka anayeweza kuimba sauti ya mwimbaji yeyote aliyeihama bendi hiyo.
Na ndivyo ilivyokuwa, anapokuwepo kwenye jukwaa la Twanga Pepeta, basi hakuna pengo la sauti ya mwimbaji wa kiume litakaloonekana, atafukia mashimo yote kuanzia uimbaji hadi rap.
Huyo ni Dogo Rama mwimbaji aliyetua Twanga Pepeta mwaka 2009 akitokea Mwanza na kudumu hadi mwaka 2015 alipojiunga na Double M Plus ya Mwinjuma Muumini.
Mwaka 2022, Dogo Rama aliendelea kuonyesha ubabe wake kwa nyimbo za Twanga Pepeta alipokuwa mjini Lindi akiitumikia Paris Band.
Kupitia kipande hiki cha video ya mwaka 2022, angalia namna Dogo Rama alivyounyanyasa wimbo wa Twanga Pepeta "Penzi Sigara Kali" utunzi wake Chaz Baba.
Said Mdoe
1/5/2024
PAPII KOCHA: NABAKIJE MWENYEWE!
Sikiliza kionjo hiki kutoka kwa Papii Kocha "Mtoto wa Mfalme" rais wa Town Classic.
Papii Kocha ni kiumbe aliyejaaliwa uwezo mkubwa wa kucheza na sauti halafu wala hatumii nguvu.
Papii Kocha anakufanya uone kuwa kuimba ni kazi rahisi kwa namna anavyoimba kwa kurelax.
Said Mdoe
21/4/2024
SELE MUHUMBA SASA NI RASMI MALI YA TWANGA ...MISHAHARA YAMKIMBIZA TOWN CLASSIC
Mkali wa kucharaza nyuzi za gitaa la solo na gitaa la kati, Sele Muhumba, amerejea bendi yake ya zamani Twanga Pepeta.
Sele Muhumba anaongeza idadi ya wasanii kadhaa walioondoka Town Classic Band ndani ya kipindi kifupi.
Nyota huyo ametambulishwa rasmi kama msanii wa Twanga leo usiku ndani ukumbi wa Andrew's Lounge, Sinza jijiini Dar es Salaam.
Siku moja iliyopita, meneja wa Twanga Pepeta, Martin Sospeter aliiambia Saluti5 kuwa Sele ametimiza wiki tangu aliporejea kundini.
Sele ni mmoja kati ya wasanii walioasisi Town Classic mwaka 2022.
Saluti5 ilipowasiliana na Sele Muhumba siku ya Alhamisi, akasema bado hajaondoka rasmi Town Classic ingawa yuko mbioni kufanya hivyo na aliulalamikia mfumo wa kulipana mshahara ndani ya bendi hiyo.
"Wakati wa utawala wa marehemu Patrick Kessy mishahara ilikuwa inatoka kwa wakati, lakini sasa hivi tarehe zinapitiliza, kwa mfano mpaka jana tarehe 17 mshahara wa mwezi uliopita haujatoka," alisema Sele Muhumba.
Afisa Habari wa Town Classic, Anania Junior alipoongea na Saluti5 Alhamisi mchana, akasema anachojua ni kwamba Sele ni msanii wao na mkataba wake bado haujaisha.
Anania pia alikanusha suala la uchelewaji wa mishahara na kusema hiyo imetokea mwezi Machi tu na ni kwa vile uliandamana na mfungo wa mwezi wa Ramadhan ambao ulifanya bendi ibakiwe na show moja tu kwa wiki.
Yote kwa yote, usiku huu CEO wa Twanga Pepeta, Luizer Mbutu, ametangaza rasmi kurejea kundini.
Said Mdoe
20/4/2024
HATIMAYE MSONDO NGOMA WAINGIA STUDIO KUSHUSHA VYUMA VIPYA
Msondo Ngoma "Baba ya Muziki" wameingia studio kupakua nyimbo mbili mpya.
Unaambiwa sasa ni wasaa wa kupata sauti ya mamlaka kwenye muziki wa dansi.
Nyimbo hizo ambazo zote zimetungwa na waimbaji ni "Last Chance" wa Juma Katundu na "Pangu Pakavu" kutoka kwa Athumani Kambi.
Studio inayotumika ni Sound Crafters chini ya producer Enrico.
Mmoja kati ya watu watakaokufurahisha sana kwenye kazi hizi ni Hassan Moshi "TX Junior" ambaye katika "Last Chance" ameimba pamoja na kusherehesha vizuri sana kwenye sebene.
Kwenye video hii, ilikuwa ni mazoezi ya mwisho kabisa jana kabla ya kuingia studio leo.
Said Mdoe
26/3/2024
MWIMBAJI MPYA WA JODE MUSICA KUTOKA TOWN CLASSIC HUYU HAPA
Mwimbaji chipukizi Said Shaaban Salum maarufu kama Tweeter Melody, ndiye msanii mpya wa Jode Musica aliyetambulishwa jana usiku.
Tweeter Melody amejiunga na Jode Musica akitokea Town Classic aliyoitumikia tangu Februari 2023 hadi mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mwimbaji huyo ameiambia Saluti5 kuwa ameondoka Town Classic kiroho safi na ataendelea kuiheshimu kwa kumlea na kumkuza.
"Sina ugomvi na Town Classic, imenilea vizuri sana ila nimeona sasa ni muda sahihi wa kwenda kutafuta changamoto mpya," ameeleza Tweeter na kuongeza kuwa jana aliiaga rasmi bendi yake ya zamani kupitia group la WhatsApp.
Tweeter ni zao llililoimarishwa zaidi na Mwinjuma Muumini baada ya kupita bendi kadhaa ikiwemo Wisdom Musica ya Arusha.
Kwa Muumini alishirikishwa kwenye wimbo "Mtumbue" na baadae Muumini huyo huyo akampeleka Tweeter Town Classic kupitia kwa mmiliki marehemu Patrick Kessy.
Licha ya kutumika sana jukwaani kwenye show za Town Classic, lakini Tweeter Melody hakufanikiwa kupata kipande chochote cha kuimba kwenye nyimbo za bendi hiyo zilIzoachiwa hewani.
Hata hivyo mwimbaji huyo ameiambia Saluti5 kuwa ameingia studio na kurekodi nyimbo mbili za Town Classic ambazo bado hazijatoka.
Said Mdoe
17/3/2024
PAPII KOCHA ATUPA JIWE GIZANI NA DUNIA MSONGAMANO
Mwanzoni mwa miaka ya 80, Ndala Kasheba akiwa Orchestra Safari Sound (OSS) alisukuma hewani wimbo "Dunia Msongamano" ambao umekuwa moja ya nyimbo bora za miaka yote.
Wakati huo OSS chini ya Kasheba ilikuwa na upinzani mkubwa sana na Maquis Original chini ya Nguza Vicking baba mzazi wa Papii Kocha.
Jana usiku usiku katika ukumbi wa TTG Lounge, Kimara Korogwe, Papii Kocha akiwa na Town Classic Band, akakumbushia enzi za ufalme wa Kasheba kwa kuimba sehemu ya wimbo huo Dunia Msongamano.
Kama kawaida ya Papii ya kunogesha nyimbo za zamani kwa kuchanganya na matukio mapya ya karibuni, ndivyo alivyofanya kwenye wimbo huo wa Kasheba aliyefariki mwaka 2004 akiwa na umri wa miaka 58.
Papii akatupa jiwe gizani kwa kuchomekea namna baadhi ya watu walivyofurahia kusikia mmiliki wa bendi yao ya Town Classic, Patrick Kessy amefariki dunia.
Said Mdoe
16/3/2024
ANAITWA KILIMANJARO
Huyu ni dansa mpya wa Bogoss Musica ambaye amebatizwa jina la Kilimanjaro.
NESA NESA YA BOGOSS MUSICA USIPIME
Wakati Bogoss Musica ikiendelea kutamba na mitindo mingi ya uchezaji ikiwemo Teke la Ng'ombe na Vimba, sasa inakuja na kitu kingine kipya.
Sasa hivi ukienda kwenye show za Bogoss chini yake Nyoshi el Saadat, utakutana na staili ya Nesa Nesa.
Hii ni silaha nyingine ya Bogoss ambayo itazidi kuwaweka kileleni kwenye idara ya ubunifu wa show.
Nyuma ya staili hii, utasindikiza na rao tamu kutoka kwa rapa Kimbunga ambaye ndiye kama kiranja anayehakikisha Nesa Nesa inabamba vizuri.
Jana usiku kwenye show ya Vunja Jungu ndani ya Blue Park Lounge, Kinyerezi Mwembeni mashabiki waliipata live Nesa Nesa ya Bogoss Musica.
Said Mdoe
11/3/2024
SIKINDE OG YAITEKA MAGOMENI, NYIMBO MPYA ZAONDOKA NA KIJIJI
Onyesho la Sikinde OG lillofanyika jana usiku Magomeni jijini Dar es Salaam, lilitia fora.
Ilikuwa ndani ya Mbizo Garden ambapo ilionekana kama vile Sikinde OG imeiteka Magomeni kwa namna ukumbi huo ulivyofurika mashabiki.
Onyesho hilo lililopewa jina la Usiku wa Ushauri wa Bure, lilipambwa na nyimbo mbili mpya zilizoachiwa hewani wiki chache zilizopita.
Nyimbo hizo "Pua ya Nguruwe" na "Ushauri wa Bure" zilitia fora sana licha ya kwamba jana ndiyo zilikuwa zinapigwa kwa mara ya kwanza jukwaani.
Ngoma hizo mpya ndizo zilizonyanyua mashabiki wengi kutoka kwenye viti vyao na kwenda kusakata goma la OG.
Waimbaji Fresh Jumbe na Skassy Kasambula walijipambanua wazi kuwa bado wako kwenye kiwango bora sana.
Katika nyimbo mbili tatu za mwanzo 'sound' haikuwa kwenye ubora na ilionekana kama vile kitumbua kinatiwa mchanga, lakini baadae ikatii amri na mambo yakawa bam bam.
Katibu wa Chama cha Muziki wa Dansi (CHAMUDATA) Said Kibiriti alipokaribishwa jukaaani na MC wa onyesho hilo Rajab Zomboko, kiongozi huyo akasema amevutiwa sana na muziki wa OG.
Said Mdoe
9/3/2024
SIKINDE OG KUIRUDISHA JIKONI "USHAURI WA BURE" IJUMAA HII
Ijumaa hii ndani ya ukumbi wa Mbizo Garden, Magomeni jijini Dar es Salaam, kutakuwa na onyesho maalum la Sikinde OG ambalo limebeba historia nzuri nyuma ya pazia.
Onyesho limepewa jina la Usiku wa Ushauri wa Bure ambalo pamoja na mambo mengine mengi, litashuhuhudia nyimbo mpya za bendi hiyo zikitambulishwa live jukwaani.
Nyimbo hizo ambazo tayari zinafanya vizuri kwenye vituo vya radio tangu ziachiwe hewani siku chache zilizopita, ni "Ushauri wa Bure" na "Pua ya Nguruwe".
"Ushauri wa Bure" umepewa heshima ya kubeba jina la onyesho hilo la kesho Machi 8.
Historia ya wimbo "Ushauri wa Bure" inaonyesha kwamba ulifanyiwa mazoezi Mbizo Garden hadi unakamilika na kwenda kurekodiwa kwenye studio za Sound Crafters chini ya producer Enrico.
Kwa maana nyingine ni kwamba wimbo Ushauri wa Bure ulipikwa Mbizo Garden na sasa unakwenda kutambulishwa rasmi jukwaani hapo hapo Mbizo Garden.
Hili ni moja ya maonyesho makubwa ya dansi kabla ya kuingia kwenye mapumziko ya mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Said Mdoe
7/3/2024
AYA 15 ZA SAID MDOE: TUKUYU SOUND KUNA SEHEMU SIJAWAELEWA
Tukuyu Sound ni kama vile imefanikiwa kujitengenezea dhehebu lake lenye waumini watiifu. Katika umri wake wa miaka mitatu tu, tayari bendi hii imekuwa na wafuasi wengi sana jijini Dar es Salaam.
Kalala Junior boss wa Tukuyu Sound anaonyesha kwa vitendo kwamba yeye ni bidhaa inayouzika vizuri sokoni. Kilichobakia kwake ni kuhakikisha bendi yake inatengeneza wafuasi mikoani na nje ya mipaka ya Tanzania.
Nilikuwa mmoja wa mashuhuda kwenye onyesho la Tukuyu Sound la kutimiza miaka mitatu Jumamosi iliyopita ndani ya ukumbi wa Brake Point Makumbusho.
Tukuyu walifaulu upande wa 'sound' eneo ambalo huwa korofi kwenye matukio mengi makubwa ya dansi. Maskio yetu yalipokea muziki safi usio na chembe ya uchafu.
Uzinduzi wa video mpya ya wimbo "Fumbo" ni eneo lingine ambalo Tukuyu Sound walifaulu. Utambulisho wa wasanii wapya Jackson Soloo, Victor Kalume, Muu Bella na Totoo Kalala ulivutia na kuongeza thamani ya onyesho.
Kama nilivyosema siku moja baada ya onyesho hilo, kwa umati ule, huku kiingilio cha chini kabisa kikiwa shilingi 10,000 na kwa muziki ulionyukwa jukwaani, ni lazima tukiri kuwa Tukuyu Sound wameuheshimisha muziki wa dansi.
Onyesho lilirushwa live na Channel Ten Plus kwa ubora wa hali juu. Naamini kupitia production ile, basi Tukuyu Sound wamejiongezea namba ya mashabiki kutoka kwa watu waliokuwa wakilifuatilia onyesho lile kutokea majumbani mwao.
Mshereheshaji wa onyesho hilo, MC Mtama alilitendea haki, hakuwa na mambo mengi yaliyotafuna muda. Show ya utangulizi kutoka kwa Seif Kisauji na bendi yake ya Babloom, ilikuwa poa.
Tukuyu Sound imeenea vizuri katika kila idara, muziki wao hauboi na kwasasa sioni kama bendi inahitaji kuingia sokoni kufanya usajili, itakuwa ni fujo tu.
Ipo sehemu ndogo sana ninayo wadai Tukuyu Sound, ni Ile tabia ya kurefusha mno nyimbo zao jukwaani. Bendi ilianza kutumbuiza saa 5:35 usiku hadi saa 10 kasorobo alfajiri lakini nyimbo zilizosikika hazikuzidi tano.
Ku