26/10/2023
Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) limegundua eneo jipya lenye kivutio cha kipekee cha Utalii ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ambalo limepambwa na nguvu za asilia (Natural Pillars).
Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Ruaha, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Godwell Meing’ataki amesema jitihada za kulitangaza eneo hilo zimeanza ndani na nje ya mipaka ya Tanzania ili kuvutia watalii wengi zaidi na wawekezaji kutembelea na kuwekeza katika aina hiyo mpya ya Utalii.
Kamishna Meing'ataki amesema TANAPA inafanya taratibu za kuwaalika watafiti mbalimbali wa miamba, udongo na Malikale (Archiolojia) wa ndani na nje ya nchi ili kubaini na kupata taarifa sahihi za malikale zilizopo, taarifa ambazo zitalitambulisha eneo hilo kimataifa.
Eneo hilo ambalo limepewa jina la "Ruaha Magic Site", mandhari yake inafanana na masalia ya zana za Mawe mithili ya zile zilizotumika Zama za Mawe za Mwanzo.