Peter Shayo, mzazi aliyepoteza watoto wawili katika ajali ya gari la Shule ya Msingi Ghati Memorial lililosombwa na maji jijini Arusha, amesimulia alivyosita kuwapeleka shule lakini baadaye akalazimika baada ya kupigiwa simu na dereva.
Akizungumza nyumbani kwake Mtaa wa Engosengiu Jumamosi Aprili 13, 2024, mzazi huyo wa marehemu Abigail Peter (11) na Abiabol Peter (5) amesema kabla ya janga hilo, alimtahadharisha dereva awe makini kutokana na mvua zilizonyesha.
Amesema hata baada ya kumweleza dereva huyo, hakumjibu kitu, ila alicheka kisha akaondoa gari kwa kasi.
(Video na Janeth Mushi)
#mwananchiupdates
#tunaliwezeshataifa
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amesema katika utaratibu wao wa kusikiliza kero za wananchi, hawatahusisha zilizopo mahakamani kwa sababu wana heshimu muhimili huo na utawala wa sheria.
Dk Nchimbi ameeleza hayo leo Jumamosi Aprili 13, 2024 wakati akizungumza na WanaCCM wa Mkoa wa Katavi katika ofisi za chama hicho zilizopo wilayani Mpanda mkoani hapa.
Dk Nchimbi alikuwa anatilia mkazo kauli ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Amos Makalla ambaye katika salamu zake za utangulizi amesema katika ziara zao wanawaalika watu wote kutoa kero isipokuwa zilizopo mahakamani.
Dk Nchimbi ambaye ni mwanadiplomasia na baadhi ya viongozi wenzake wanaounda sekretarieti ya CCM wameanza ziara ya mikoa sita ya kuimarisha, kukagua uhai wa chama hicho na kuangalia utekelezaji wa Ilani yake ya uchaguzi.
"Nitumie nafasi hii kumuunga mkono mwenezi wetu wa Taifa katika mambo tutakayoyashughulikia kama kero, hatutayagusa yaliko mahakamani, ndio utaratibu wa utawala bora. Moja ya sera ya CCM ni kusimamia utawala wa sheria,” amesema.
"Wakati wote wajibu wetu utakuwa kuzihamasisha mahakama zetu zitende haki bila kuziingilia katika uamuzi wake, nchi inayotaka kufanikiwa lazima isimamie utawala bora, ukijenga utaratibu wa kuingilia mahakamani siku moja, itawaumiza ... au wakija wengine watasema huyu mwenyekiti wa chama mkoa si alipenda kuagiza mahakama, acha tuagize akae mahabusu siku 90 kwanza kabla ya kuongea naye," amesema Dk Nchimbi.
Awali, akijenga hoja yake, Makalla amewataka wananchi kutambua kuwa mambo yaliyopo katika mhimili wa mahakama yanamalizwa hukohuko na hivyo wao hawatayasikiliza.
Katibu wa Idara ya Oganaizesheni ya chama hicho, Issa Ussi Gavu amewataka WanaCCM kuhakikisha wanawapata wagombea wenye sifa na malengo ya kutatua changamoto za wananchi na kuwa wale wenye makandokando hawatakuwa na nafasi.
#mwananchiupdates
#tunaliwezeshataifa
Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi na ujumbe wake wamewasili asubuhi hii mkoani Katavi kuanza ziara ya mikoa sita nchini. Katika ziara hiyo anaongozana na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makala na Katibu wa Idara ya Organaizesheni, Issa Ussi Gavu
#mwananchiupdates
#tunaliwezeshataifa
Rais wa Tanzania, Samia Suhulu Hassan ametaja mambo matatu ambayo aliyekuwa Waziri Mkuu, hayati Edward Sokoine alipambana nayo enzi za uhai wake, ikiwa ni pamoja na kusimamia ukombizi Kusini mwa Afrika, vita ya Nduli Iddi Amini na operation ya hujumu uchumi.
Rais Samia amesema hayo leo Aprili 12,2024 baada ya kushiriki ibada ya kumbukizi ya miaka 40 ya kifo cha Sokoine.
(Imeandikwa na Elizabeth Joachim)
#mwananchiupdates
#tunaliwezeshataifa
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM, Amos Makalla, amesema yupo tayari kushiriki mdahalo katika kukilinda na kukitetea chama chake dhidi ya vyama vingine.
Makala amesema hayo leo Aprili 12, 2024 jijini Dodoma wakati wa mapokezi ya viongozi wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu-Bara, John Mongella.
Amesema kuwa mapokezi haya ni kutesti mitambo kuelekea kwenye ziara ya mikoa sita ambayo itakuwa na mambo manne, ikiwemo kwenda kutatua kero za wananchi jambo ambalo alilifanya kwa nguvu kubwa mtangulizi wake kwenye nafasi hiyo, Paul Makonda.
#mwananchiupdates
#tunaliwezeshataifa
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amewataka watu wanaotumia fedha kuwatuma watu kumtukana Rais Samia Suluhu Hassan mtandaoni kuacha mara moja na endapo wataendelea, Jumatatu ya Aprili 15,2024 atawajata.
Makonda amesema, "Wapo watu wanaotumia fedha kuwaagiza watu kumtukana Rais Samia, naomba waache mara moja, ninawafahamu kwa majina, msipoacha Jumatatu nitawataja, wapo hadi mawaziri."
Makonda amesema hayo leo Aprili 12, 2024 kwenye maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 40 ya kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Sokoine yaliyofanyika Monduli mkoani Arusha.
(Imeandikwa na Elizabeth Joachim)
#mwananchiupdates
#tunaliwezeshataifa
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi CCM, Ally Hapi amesema kila chama kina uhuru wa kufanya siasa zake, hivyo kufanya uwanja wa siasa kuwa sawa kwa kila chama, huku akisema hakutakuwa na kuachiana nafasi kwenye chaguzi za mwaka 2024 na mwaka 2025.
Hapi amesema hayo leo Ijumaa Aprili 12, 2024 jijini Dodoma wakati wa mapokezi ya viongozi wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu -Bara, John Mongella.
#mwananchiupdates
#tunaliwezeshataifa
Wakati Pamba Jiji ikitarajiwa kushuka uwanjani kesho kucheza mechi ya mwisho ya Championship ikiwa nyumbani dhidi ya FGA Talents, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amewaongezea mzuka mastaa wa timu hiyo kwa kuwaibukia na kufanya nao mazoezi kisha kuwapa ahadi tamu kama itashinda.
Mtanda aliyekabidhiwa ofisi na aliyekuwa Mkuu wa mkoa huo, Amosi Makalla Aprili 6 katika kikao chake cha kwanza na timu hiyo leo kwenye Uwanja wa Nyamagana amefanya mazoezi na timu hiyo kuanzia saa 3:00-4:00 asubuhi kisha akazungumza na benchi la ufundi na menejimenti ya timu hiyo.
Akizungumza na wachezaji baada ya mazoezi, Mtanda aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara na mlezi wa Biashara United, amewatoa wasiwasi wachezaji akiahidi kuendelea kutoa motisha, kuendeleza mipango iliyoachwa na Makalla huku akiahidi kuanza mikakati mapema ya mechi mbili za mwisho ugenini.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Trivonia Kisiga amewataka wachezaji kuyafanyia kazi maelekezo yote ambayo yametolewa na Mtanda huku akisisitiza yote yaliyoahidiwa yatatekelezwa, huku mchezaji wa zamani wa Pamba, Fumo Felician alikazia kwa kusema;"Hii ni neema ambayo tumepata msimu huu kuwa na Amos Makalla na Said Mtanda wote ni wanamichezo, naamini mwaka huu mvua inyeshe jua liwake tutakwenda Ligi Kuu."
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji, Haruna Chanongo amesema; "Kipindi kama hicho tunaangalia mikakati ya kumaliza ligi, kitu kikubwa tunachozungumza kama wachezaji ni kutobweteka kwa sababu safari bado haijaisha mpaka tufanikishe mipango yetu ya kuipandisha timu."
#mwananchiupdates
#tunaliwezeshataifa
Katibu Mkuu wa Umoja wa vijana CCM (UVCCM), Jokate Mwegelo amesemakuwa vijana wa CCM watajibu hoja za wapinzani wao kwa hoja, watatafuta na kulinda kura za wateule wote watakaoteuliwa na CCM kugombea nafasi mbalimbali kwa namnna yoyote, ikiwemo kwa kutumia teknolojia mbalimbali.
Jokate amesema hayo leo Ijumaa Aprili 12,2024 jijini Dodom kwenye mapokezi ya viongozi wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM wakiongozwa na Naibu katibu Mkuu wa CCM, John Mongella.
#mwananchiupdates
#tunaliwezeshataifa
Askofu wa Jimbo la Arusha, Isack Amani amesema Edward Sokoine angekuwa hai angehakikisha wakazi wa Arusha wanajihadhari na matumizi ya 'cha Arusha'.
Pia amesema hayati Sokoine alikuwa mkereketwa wa uhujumu uchumi pamoja na chachu ya kuwasaidia wamasai kupeleka watoto shule.
Amesema hayo leo Aprili 12, 2024 katika misa maalumu ya kumbukizi ya miaka 40 ya kifo cha Sokoine iliyofanyika nyumbani kwake Monduli mkoani Arusha.
(Imeandikwa na Elizabeth Joachim)
#mwananchiupdates
#tunaliwezeshataifa
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba amesema miongoni mwa nyakati ambazo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kunashamiri fitina ni pale uchaguzi mkuu unapokaribia, huku Rais aliyepo madarakani akipaswa kuendelea na muhula wa pili.
Makamba alitoa kauli hiyo jana Alhamis Aprili 11, 2024 katika moja ya hotuba zake mbele ya wananchi wa Kijiji cha Mahezangulu mkoani Tanga, wakati wa Idd pili aliyosherehekea na wananchi wa eneo hilo.
#mwananchiupdates
#tunaliwezeshataifa
Viongozi wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM wakiongozwa na Naibu katibu Mkuu wa CCM, John Mongella, Katibu wa itikadi na uenezi CCM, Amos Makalla, Katibu Mkuu wa Umoja wa vijana CCM (UVCCM), Jokate Mwegelo na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi CCM, Ally Hapi wakipokelewa kwenye ofisi za Makao Makuu ya chama hicho Dodoma leo Ijumaa Aprili 12, 2024.
#mwananchiupdates
#tunaliwezeshataifa
Mkurugenzi wa Huduma za Afya Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais –Tamisemi, Dk Rashid Mfaume amebaini ukiukwaji wa mununuzi ya vifaa ikiwemo majokofu ya kuhifadia damu katika kituo cha afya Mwalugulu katika Halmashauri ya Msalala Mkoa Shinyanga.
Dk Rashid Mfaume amebaini changamoto hizo akiwa katika ukaguzi na ziara ya usimamizi shirikishi wa shughuli za huduma za afya ndani ya kituo cha afya Mwalugulu.
Amebaini majokofu mawili yaliyonunuliwa katika kituo hicho kwa ajili ya kuhifadhi damu ni majokofu kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.
Pia amebaini baadhi ya vifaa tiba, ikiwemo mashine ya dawa za usingizi vimepokelewa bila kukaguliwa wakati malipo yalishafanyika bila viambatanisho vya taarifa ya ukaguzi na mapokezi.
(Video kwa hisani ya Ofisi-Tamisemi)
#mwananchiupdates
#tunaliwezeshataifa
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewasili katika Kijiji cha Enguiki, wilayani Monduli, nyumbani kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, hayati Edward Sokoine na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda ili kushiriki misa maalumu ya kumbukumbu ya miaka 40 ya kifo cha Sokoine kilichosababishwa kwa ajali ya gari tarehe kama ya leo miaka 40 iliyopita.
(Imeandikwa na Elizabeth Joachim)
#mwananchiupdates
#tunaliwezeshataifa
Katika kumbukizi ya miaka 40 ya kifo aliyekuwa Waziri wa Tanzania, Edward Sokoine ngo'mbe 100 wamechinjwa kuadhimisha kumbukizi hiyo inayofanyika leo Aprili 12, 2024 Monduli mkoani Arusha.
Katika kumbukizi hiyo, viongozi mbalimbali wameshiriki ikiwa ni pamoja na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango pamoja na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
(Imeandikwa na Elizabeth Joachim)
#mwananchiupdates
#tunaliwezeshataifa
Wanafunzi saba wa Shule ya Msingi Ghati Memorial wahofiwa kufariki dunia baada ya gari la shule waliokuwemo kuangukia kwenye korongo lililojaa maji eneo la Dampo, Kata ya Muriet mkoani Arusha.
Korongo hilo lililojaa maji yaliyotokana na mvua kubwa iliyonyesha usiku usiku wa kuamkia leo April 12, 2024, ilisababisha maji kujaa hadi barabarani.
Wakizungumza katika eneo la tukio, mashuhuda wamesema kuwa saa 12 asubuhi, gari lenye namba za usajili T 496 EFK lilikatiza juu ya barabara hiyo, dereva alishindwa kulidhibiti, hivyo liliyumba kabla ya kuangukia katika korongo hilo linalomwaga maji yake katika mto mkubwa wa Themi.
Lilian Mussa, amesema baada ya watu kuona hali hiyo walisogea eneo la tukio na kufanikiwa kuokoa watoto wanne kabla ya gari kuendelea kusogea tena na watoto wengine walionekana kusombwa na maji.
“Dereva alipoona gari linamshinda aliruka ndio watu wakaona wakaanza kusaidia hao watoto, lakini gari lilizidi kusogea kwenye kina tukaamua kuita Jeshi la Zimamoto na Polisi,” amesema Lilian.
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto Mkoa wa Arusha, Osward Mawanjejele amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kwa taarifa za awali ni kwamba gari hilo lilikuwa na watoto 11 na walimu wawili.
“Niko kwenye msafara wa Rais kwa ajili ya tukio la maadhimisho ya miaka 40 ya kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Sokoine, lakini kikosi hadi sasa wananiambia wameokoa watoto wanne na walimu wawili… bado wanaendelea kufuatilia wengine wanaosemekana walikuwepo kwenye hilo gari,” amesema.
Amesema kikosi chake kimeelekeza nguvu katika mto Themi ambapo korongo hilo linamwaga maji yake, ili kuona namna ya kuwaokoa watoto wengine wanaodaiwa walikuwepo ndani ya gari hilo.
Endelea kufuatilia mitandao ya Mwananchi kwa taarifa zaidi
(Imeandikwa na Bertha Ismail)
#mwananchiupdates
#tunaliwezeshataifa
Watu tisa wamefariki dunia na wengine 19 kujeruhiwa katika ajali ya basi la Lujiga Express lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Mwanza kupata ajali eneo la Malendi wilayani Iramba Mkoa wa Singida.
Ajali hiyo imetokea leo Aprili 10, 2024 majira ya saa 11 alfajiri na majeruhi kupelekwa katika hospitali ya wilaya ya Iramba.
Mkuu wa Wilaya ya Singida Godwin Gondwe amesema baadhi ya majeruhi wamepewa ruhusa na kuendelea na safari.
Chanzo cha ajali hiyo kinadaiwa ni uzembe wa dereva wa basi.
(Imeandaliwa na Jamaldini Abuu)
#mwananchiupdates
#tunaliwezeshataifa
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka Watanzania kuendelea kutenda mambo mema waliyokuwa wakiyafanya mwezi mtukufu wa Ramadhani pamoja na mfungo wa Kwaresma kwa kuachana mambo maovu yatakayowaingiaza matatani.
Majaliwa ametoa wito huo leo Jumatano, Aprili 10, 2024 aliposhiriki swala ya Idd el-Fitri kwenye Msikiti wa Gadafi, jijini Dodoma na kusema viongozi wa dini wamekuwa wakifanya kazi kubwa ya kuwaasa waumini kutenda mema katika kipindi hicho na kuacha maovu.
#mwananchiupdates
#tunaliwezeshataifa
Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wafanyabiashara kuacha tabia za kukwepa kodi huku akitaja kitendo hiko kuwa ni dhuluma.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Jumatano Aprili 10, 2024 wakati akitoa salamu za Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) katika Baraza la Idd El Fitri lililofanyika kitaifa mkoani Dar es Salaam na kuhudhuriwa pia na Rais mstaafu Jakaya Kikwete.
"Ulipaji wa kodi ni halali ni jukumu la mmoja wetu kulipa kodi kwa haki kulingana sheria za nchi, inasikitisha wafanyabiashara wanafanya dhuluma ya kodi nawasihi kuacha kwa sababu inachelewesha maendeleo yetu.
“Nimeamua kutumia jukwaa hili(Baraza la Idd) kwa sababu hapa kuna wafanyabiashara wakubwa lakini baadhi yao wana vipenyo vya kukwepa kodi, imani yangu tutaelewana na watalipa," amesema Rais Samia.
(Imeandikwa na Bakari Kiango)
#mwananchiupdates
#tunaliwezeshataifa
Wananchi wa Jiji la Arusha wakiwemo wafanyabiashara na wadau wa utalii wamemtaka Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda kuzibana halmashauri kuacha kutoza utitiri wa tozo.
Wamesema licha ya halmashauri za mkoa huo kama zilivyo zingine hupata ruzuku kutoka Tamisemi, lakini bado zimekuwa zikiwasumbua wananchi pamoja na watalii barabarani kudai tozo.
Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne, Aprili 9, 2024 wananchi hao wamemwomba aingilie kati kudhibiti tozo hizo kwa kushirikiana na mamlaka husika ili ustawi wa maisha na biashara za Arusha uweze kukua kwa kasi.
Pia, wamemwomba ahakikishe soko la madini ya Tanzanite ambalo liliing'arisha Arusha, linarejea tena baada ya kusitishwa kwa miaka kadhaa sasa.
(Imeandikwa na Elizabeth Joachim)
#mwananchiupdates
#tunaliwezeshataifa