27/04/2023
KIFO MIKONONI MWANGU – SEHEMU YA KWANZA
hadithi hii inaazia pale nilipokutana na MSICHANA ambaye nilikuwa simfahamu. Tulikutana tu kwenye harusi ya rafiki yangu, akaniambia ananifahamu. Msichana alikwenda mbali zaidi, akaniambia niliwahi kuwa mpenzi wake kisha nikamtoroka na siku ile ndiyo alikuwa ananiona. Kila nilivyomkatalia kwamba sikuwa nikimfahamu na kwamba mimi siye niliyekuwa mpenzi wake, msichana hakuniamini kabisa. Ilibidi baada ya tafrija kumalizika tuondoke pamoja. Alinipeleka nyumbani kwake na kunipa kinywaji. Sikufahamu kinywaji hicho alikitia nini na kwa madhumuni gani kwani baada ya kunywa tu kinywaji hicho, usingizi mzito ulinipitia.
Niliamka saa kumi na moja alfajiri na kumkuta mwenyeji wangu huyo ameuawa kando ya mlango kwa kupigwa na kitu kizito kichwani. Balaa likaniangukia mimi. Je, msichana huyo alikuwa nani, kwa nini alisema nilikuwa mpenzi wake na ni nani aliyemuua na kwa sababu gani?
SASA tuendelee
K**A wasemavyo wahenga maisha ni safari ndefu. Safari yenyewe si tambarare moja kwa moja. Ni safari yenye mabonde na milima. Naitwa Denis Wiliam Makita. Nilizaliwa miaka thelathini na nane iliyopita.
Kwa rehema ya Mungu nilizaliwa na mwenzangu wa kiume tukiwa pacha. Mwenzangu alikuwa akiitwa Charles Wiliam Makita.
Baada ya kumaliza masomo yetu ya kidato cha sita, mimi nilijiunga na Jeshi la Polisi. Niliomba kazi ya upolisi nikiwa Dar, lakini baada ya mafunzo ya upolisi nilikwenda kuanza kazi Wilaya ya Lushoto.
Mwenzangu hakutaka kufanya kazi ya kuajiriwa. Alijiingiza kwenye biashara na misukumo ya maisha ikatukutanisha tena huko Tanga. Wakati mimi nikiwa Lushoto, yeye alikuwa Tanga mjini.
Hapo Lushoto nilifanya kazi kwa mwaka mmoja, nikahamishiwa Tanga mjini. Baada ya kufanya kazi kwenye kituo cha Tanga kwa miaka saba ndipo nilipopendana na polisi mwenzangu aliyehamishwa kutoka Moshi na kuletwa Tanga. Alikuwa anaitwa Miriam.
Baada ya kuridhika na tabia zake na urembo wake, nilimchumbia Miriam na kuoana naye huko kwao Moshi.
Baada ya kuishi na Miriam kwa miaka miwili ndipo siku moja mke wangu huyo aliponipa habari nilizozifanyia kazi.
Aliniambia kwamba huko alikokwenda kusukwa alipata taarifa kwamba kulikuwa na watu ambao walikuwa wakifanya biashara ya meno ya tembo. Na walikuwa wakiyatoa meno hayo katika Msitu wa Handeni.
Akanieleza kwamba meno hayo husafirishwa hadi Kitongoji cha Mwambani kilichoko kilometa kadhaa nje ya Jiji la Tanga, pembezoni mwa Bahari ya Hindi.
Allinieleza kwamba meno hayo huhifadhiwa chini ya ardhi kwenye ufukwe wa bahari katika eneo hilo. Aliendelea kunieleza kwamba watu hao huchimba shimo usiku na kuyafukia meno hayo.
Baada ya hapo kuna usiku mwingine meno hayo hufukuliwa na kupakiwa kwenye majahazi kisha kusafirishwa kwenda kuuzwa nchi za nje.
Wakati huo mke wangu alikuwa na cheo cha ukoplo, mimi nilikuwa na cheo cha Sajin Meja. Kicheo mimi nilikuwa nimemzidi na tulikuwa tunafanya kazi katika kituo kimoja.
Mke wangu aliniambia habari ile badala ya kuiripoti kituo cha polisi kwa sababu nilikuwa mkuu wake. Aliona akinipa mimi taarifa hiyo ndiyo itakuwa imefika kituo cha polisi. Inawezekana pia aliniambia mimi ili tufanye uchunguzi kabla ya kuiripoti kituoni.
Na mimi nikafanya uchunguzi wangu. Baada ya uchunguzi wa siku tatu, nikagundua kuwa habari ile ilikuwa ni ya kweli na nilimgundua aliyekuwa akihusika na meno hayo.
Alikuwa ni mtu mmoja mwenye asili ya Mombasa nchini Kenya, lakini raia wa Tanzania aliyekuwa akiitwa Azzal Mubarak.
Baada ya kupata data zote nikaripoti kwa wakuu wangu. Siku hiyo tuliondoka usiku polisi kumi tukaenda katika eneo hilo kwa kutumia boti tatu za polisi.
Tulipofika mahali hapo tulikuta watu wakichimba. Walipotuona walitupa machepe na kukimbia. Baada ya kufukuzana nao tulik**ata mtu mmoja.
Baada ya kumk**ata mtu huyo tukaendelea kupafukua pale mahali. Tulikuta karibu vipande themanini vya meno ya tembo.
Vipande hivyo vilipakiwa kwenye boti zote tatu na kusafirishwa hadi jijini.
Baada ya kumhoji yule mtu tuliyemk**ata alituambia yeye alikuwa anachukuliwa k**a kibarua tu wa kufukua yale mashimo na kutoa meno yaliyozikwa ili jahazi likija yapakiwe.
Alipotakiwa kuwataja wahusika wenyewe alisema alikuwa hawafahamu ila anawafahamu watu watatu wa kati waliokuwa wakiishi Mwambani.
Alipotajiwa jina la Azzal Mubarak, mtu aliyekuwa akishukiwa kumiliki meno hayo alituambia alikuwa akimfahamu Azzal kwa jina tu, lakini hakuwahi kukutana naye.
Msako ukaanza usiku uleule. Baadhi ya polisi walikwenda Mwambani kwa gari wakiwa na yule mtu ambaye aliwapeleka polisi hao katika nyumba walizokuwa wakiishi watu hao aliowataja, lakini hakukuwa na mtu yeyote miongoni mwao aliyepatikana. Wote walishakimbia.
Polisi wengine nikiwemo mimi tulikwenda kumk**ata Azzal Mubarak aliyekuwa akiishi katika eneo la Raskazoni.
Yeye na yule mtu aliyek**atwa kwanza walifunguliwa mash*taka. Polisi tulifuatilia kesi ile kwa miezi nane. Azzal Mubarak alikuwa ameweka wakili wa kumtetea.
Wakati kesi yake ikiendelea nilipata pigo. Ndugu yangu, Charles alifariki dunia. Alifariki dunia kwenye ajali ya basi. Basi alilokuwa akisafiria kutoka Dar kuja Tanga liligongana uso kwa uso na basi lingine lililokuwa likitoka Tanga kwenda Dar. Abiria watatu akiwemo ndugu yangu walifariki dunia hapohapo.
Kifo cha Charles kilinifanya nigundue kuwa ndugu yangu huyo pamoja na kujiingiza katika biashara zisizoeleweka alikuwa jambazi. Chumbani kwake nilikuta bastola na risasi kumi. Pia nilikuta vielelezo vilivyobainishia kuwa kazi yake halisi ilikuwa ujambazi na alihusika katika matukio mengi ya ujambazi na mauaji.
Nilishukuru kwamba sikumgundua mapema kwani angeniharibia kazi.
Kule kugundua kwangu kwamba Charles hakuwa mtu muaminifu, nilimsahau mara moja. Mtu wa namna ile akifa unashukuru Mungu hata k**a ni ndugu yako.
Kwenye ile kesi ya Azzal Mubarak, mwisho wa siku mahak**a ilimuachia huru kwa kukosekana ushahidi thabiti wa kumtia hatiani. Yule msh*takiwa wa pili alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela.
Akiwa nje ya mahak**a, Azzal aliniambia;
“Ulinik**ata kwa kunionea tu.”
Aliniambia mimi hivyo kwa sababu nilikuwa mpelelezi wa kesi yake. Pia katika wale polisi waliokwenda kumk**ata siku ile, mimi ndiye niliyekuwa mkubwa niliyetoa amri ak**atwe.
“Unasemaje?” Nikamuuliza nikiwa nimemkunjia uso.
“Nimekwambia ulinik**ata kwa kunionea tu.”
“Kumbe ulitaka tukuachie hata k**a unashukiwa?”
“Kuwa na roho mbaya haitakusaidia.”
“Kama mahak**a imekuachia, shukuru Mungu. Usinilaumu mimi. Mimi niko kazini.”
“Sawa. Tutaonana.”
Nikashtuka. “Tutaonana kwa heri au kwa shari?” Nikamuuliza.
Azzal hakujibu, akaelekea kwenye gari lake la kifahari lililokuwa likimsubiri hapo mahak**ani. Akajipakia na kuondoka. Wakati gari linaondoka alinipungia mkono wa kuniaga. Nikampuuza.
Hata hivyo, kwa vile alikuwa mtu tajiri na katili kwa mujibu wa sifa zake tulizozisikia, maneno yake yalinitia wasiwasi sana.
Polisi wengi hatukuwa tumeridhika na ile hukumu kwa sababu tulikuwa na uhakika kwamba Azzal ndiye aliyehusika na yale meno ya tembo. Lakini tulitambua tatizo letu ni kukosekana kwa ushahidi wa kutosha wa kumuhusisha na meno hayo ambayo aliyakana.
Mimi na mke wangu siku nyingine tulikuwa tunatofautiana kuingia kazini. Mimi nikiingia mchana, yeye anaweza kuingia usiku. Au mimi nikiingia usiku, yeye anaweza kuingia mchana.
Baada ya wiki moja hivi tangu kumalizika kwa kesi ya Azzal, nilialikwa kwenye harusi ya rafiki yangu mmoja ambaye zamani alikuwa polisi na nilikuwa naye Lushoto, lakini baadaye alifukuzwa kazi kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Mtu huyo baada ya kufukuzwa kazi alikuja Tanga na kujiingiza kwenye biashara ziliompa mafanikio.
Katika kadi yake ya mwaliko aliyonipa ilionesha kuwa tafrija ilikuwa ikifanyika katika Hoteli ya Mkonge usiku. Hoteli ya Mkonge ilikuwa katika eneo la Raskazoni, pembezoni mwa Bahari ya Hindi.
Mwaliko ulikuwa ni wa mimi na mke wangu, lakini siku ile mke wangu alikuwa na zamu ya kuingia kazini usiku. Kabla ya kwenda kazini aliniambia kwa vile yeye alikuwa anakwenda kazini, nisiende huko kwenye tafrija.
“Kama unaenda kazini si ninaweza kwenda peke yangu?” Nikamwambia.
“Kwa nini uende peke yako wakati kadi yako imeandikwa bwana na bibi? Nakushauri ulale.”
“Si vizuri. Huyu mtu ni rafiki yangu na nimemthibitishia kuwa nitahudhuria.”
“Sawa. Tutaonana hapo asubuhi nikitoka kazini.”
Mke wangu alipotoka kwenda kazini kwake, nikaanza kujiandaa. Nilivaa ile suti yangu niliyokwenda
Je, nini kiliendelea? Usikose KUfuatilia sehemu inayofuta utaipata hapa hapa