21/08/2024
WAANDISHI wa habari nchini, wametakiwa kuielimisha jamii juu ya ugonjwa wa homa ya nyani ‘Mpox’ hasa katika makundi yanayoonekana kuwa hatarini zaidi kupata ugonjwa huo endapo utaingia nchini.
Akitoa elimu ya ya ugonjwa huo kwa waandishi hao katika Ofisi za Kitengo cha Elimu ya Afya Meya Zanzibar, Meneja wa kitengo hicho, Bakar Hamad Magarawa, aliwataka wandishi kuielezea jamii juu dalili za ugonjwa huo na njia za kujikinga nao.
Alisema ugonjwa huo unaosababishwa na kirusi cha ‘Monkeypox’ uligundulika kwa
mara ya kwanza mwaka 1958 nchini Denmark na kuenea katika nchi nyengine ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa upande wa nchi za Afrika.
Magarawa alieleza kuwa maambukizi ya ugonjwa huo yalianza kutoka kwa mnyama kwenda kwa binaadamu katika nchi zilizo karibu na misitu ya Kitropiki na kwamba uzoefu unaonesha kuwa Zanzibar ni nchi yenye muingiliano wa wageni kutoka nchi tofauti hivyo inakuwa ni miongoni mwa nchi zilizo katika hatari ya kupata ugonjwa huo.
Aidha Magarawa alisema ugonjwa unapatikana kwa njia ya kujamiiana na mwenye maambukizi hasa mapenzi ya jinsia moja, kula au kugusa mizoga ya wanyama, kugusana na mtu mwenye dalili za ugonjwa huo kwa kusalimiana kwa kukumbatiana au kushikana mikono pamoja na kugusa maji maji ya mwili wa mtu mwenye maambukizi.
Alisema dalili za ugonjwa huo zinafanana na maradhi mengine, jambo ambalo ni gumu mtu kujitambua, hivyo aliishauri jamii kuwahi kituo cha afya mara tu anapopata homa, vidonda vya koo, maumivu ya kichwa, maumivu ya mgongo, misuli, uchovu wa mwili, kuvimba kwa mitoki na kuwashwa kwa muendelezo.
Aliongeza kuwa ugonjwa huo hauna matibabu maalum ila jamii inashauriwa kuwahi kituo cha afya kupata matibabu ya dalili za ugonjwa huo ambazo hujitokeza ndani ya wiki mbili baada ya kupata maambukizi.