07/10/2024
WHAT I'M AFRAID OF BEFORE I DIE ( Kinachoniogofya kabla ya kifo changu)
Ninapofikiri kuhusu maisha yangu na safari iliyo mbele yangu, mara nyingi kuna hofu hunijia, hofu ya kupoteza maono ya lengo kuu la maisha na zawadi hii ya uhai na uzima. Katika zama hizi tulizonazo ni rahisi kuingia kwenye kinyang'anyiro cha kutafuta mali, mafanikio, na uthibitisho (sifa na vyeo vitokanavyo na hayo). Kila siku, tunakimbilia katika kujikusanyia vitu,tukipima thamani yetu kwa kujifananisha na wengine na kujitahidi kupanda ngazi isiyo na mwisho ya mafanikio. Hata hivyo, katika mbio hizi, nina wasi wasi kuhusu jambo moja..
Si jengine ila lile linalo nipa hofu kubwa kila wakati nalo ni kufika mwisho wa uhai wangu nikiwa na majuto na huzuni.Nadhani mara nyingi, tunatumia muda wa kutosha kwa mambo yetu binafsi ikiwemo ukuaji wa kibinafsi, na kutafuta maarifa. Lakini je ni kwa kiasi gani haya mambo yetu binafsi hutueka mbali na wengine ? familia na marafiki?
Je, tumetoa muda wa kutosha kweli kutambua uzuri wa ulimwengu na mazingira yanayonizunguka?
Zaidi ya hayo, ninahisi hofu wakati ninapowaza kuhusu ukomo wa uhai wangu . Wazo (idea) la kusimama mbele ya ukweli wa mwisho wa maisha yangu , nikitafakari jinsi nilivyotumia siku zangu.Je, niliishi kwa upendo? Je, nini kiliku kipaombele changu?
Kadri ninavyotafakari kuhusu umauti, nazidi kubaini ya kwamba kila sekunde hapa ulimwenguni ni zawadi. Masaa yanakatika, na kila kila kipimo cha muda ni muhimu.
Ila nimebaini hofu yangu si kifo chenyewe, bali wazo la kufa bila kuishi na kufikia lengo la kua ulimwenguni .Ewe nafsi yangu na ya mwenzangu kumbuka lengo kuu la Uhai wako hapa duniani, acha kupumbazika kwingi kwa kisingizio cha kutafuta mali na kukimbizana na kivuli cha mafanikio ya kidunia (yenye udanganyifu).