30/05/2024
Wahitimu 188,787 kati ya 197,426 waliofaulu mitihani ya kidato cha nne, wamechaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha tano na sita pamoja na vyuo mbalimbali kwa mwaka 2024.
“Wanafunzi waliochaguliwa baada ya kukidhi vigezo wapo wenye mahitaji maalumu 812 na kupangiwa kujiunga na kidato cha tano katika shule mbalimbali nchini pamoja na vyuo vya kati katika fani mbalimbali,”amesema Mchengerwa.
Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa amesema hayo leo Alhamisi Mei 30, 2024 wakati akitangaza uchaguzi wa wanafunzi.
Mchengerwa amesema wanafunzi 131,986 wakiwamo wasichana 66,432 na wavulana 65,554 wenye sifa, wamechaguliwa kujiunga na shule za sekondari za kidato cha tano 622 zikiwamo shule mpya 82 zinazoanza mwaka huu wa 2024.
“Wanafunzi 1,462 wakiwamo wasichana 669 na wavulana 793 walipangwa katika shule za sekondari nane zinazopokea wanafunzi wenye ufaulu wa juu zaidi ambazo ni Kilakala, Mzumbe, Ilboru, Kisimiri, Msalato, Kibaha, Tabora Boys na Tabora Girls,”amesema Mchengerwa.
Pia, amesema wanafunzi 6,576 wakiwamo wasichana 3,449 na wavulana 3,127 wamepangwa katika shule za sekondari za kutwa za kidato cha tano huku wanafunzi 123,948 wakiwamo wasichana 62,636 na wavulana 61,312 wamepangiwa katika shule za sekondari za bweni za kitaifa za kidato cha tano.