06/01/2026
Huzuni imetanda katika Kata ya Tumbi, Manispaa ya Tabora, baada ya mwili wa kijana mmoja dereva wa pikipiki kupatikana umefariki na kutupwa katika msitu wa Matitumbi.
Marehemu ametambulika kwa jina la Sigela Hamisi Maulidi (23), mkazi wa eneo hilo, ambaye aliripotiwa kupotea kwa siku tatu mfululizo.
Kwa mujibu wa viongozi wa eneo hilo, kijana huyo alionekana mara ya mwisho tarehe 4 ya mwezi huu majira ya saa moja usiku, baada ya kupokea simu kutoka kwa mtu aliyedhaniwa kuwa abiria. Tangu wakati huo hakurejea nyumbani wala kuwasiliana na ndugu zake.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Tumbi, Rajabu Hamsini, akizungumza pamoja na Mwenyekiti wa Kitongoji husika Mollo John, wamesema juhudi za kumtafuta zilianza mara moja kwa kushirikiana na familia ya marehemu pamoja na madereva wenzake wa bodaboda.
Hatimaye, leo mwili wake uligundulika msituni ukiwa umefungwa mikono kwa kamba na miguu ikiwa imefungwa kwa mipira, huku pikipiki yake ikiwa haijulikani ilipo.
Baba mzazi wa marehemu, Hamisi Maulidi, amesema mwanawe aliondoka nyumbani usiku huo bila kubeba abiria yoyote, hali iliyozua maswali zaidi juu ya mazingira ya tukio hilo la kikatili.
Akitoa tahadhari kufuatia tukio hilo, Mwenyekiti wa Maafisa Usafirishaji Mkoa wa Tabora, Mrisho Shime, amewataka madereva wa bodaboda kuwa waangalifu zaidi, hasa kuepuka kubeba abiria wasiowafahamu au zaidi ya mmoja, hasa nyakati za usiku na maeneo ya nje ya mji.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora limefika eneo la tukio na kuchukua mwili wa marehemu kwa ajili ya uchunguzi wa kina, huku uchunguzi wa kubaini waliohusika na tukio hilo ukiendelea.
✍️ Pascal Tuliano