07/01/2026
MGONGANO WA MASLAHI WATIKISA UCHAGUZI FRAT MKOA: WADAU WA SOKA WAPAZA SAUTI.
Kumekuwepo na sintofahamu kubwa ndani ya mchakato wa uchaguzi wa FRAT Mkoa, kufuatia uteuzi wa Wakili Musa Nyamwelo kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya FRAT Mkoa, hali inayodaiwa kukiuka misingi ya haki, uwazi na kuepuka mgongano wa maslahi.
Wadau wa soka wamehoji vikali uteuzi huo wakibainisha kuwa Wakili Nyamwelo kwa sasa ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya MZFA, jambo linalozua maswali mazito kuhusu uwezekano wa Conflict of Interest katika mchakato mzima wa uchaguzi.
Kwa mujibu wa wadau hao, haijawahi kutokea katika historia ya soka la Tanzania, mtu mmoja kushika nafasi za juu za Kamati za Uchaguzi katika ngazi mbili tofauti kwa wakati mmoja. Mfano umetolewa wa Wakili Kiomoni Kibamba, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi TFF na wakati huo huo hawezi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi MZFA.
MKANGANYIKO NDANI YA KAMATI TENDAJI FRAT
Taarifa zinaeleza kuwa ndani ya Kamati Tendaji ya FRAT Mkoa kulikuwapo na mjadala mpana, ambapo wajumbe wengi walikubaliana kuwa Wakili Madukwa aendelee kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, nafasi ambayo amekuwa akiishikilia hata katika uchaguzi uliopita uliofanyika Bwalo la Mgambo.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati Tendaji FRAT Mkoa, Emmanuel Mataba, anadaiwa kumteua Wakili Nyamwelo bila ridhaa ya wajumbe wa Kamati Tendaji, hatua iliyozua mpasuko na malalamiko makubwa miongoni mwa wajumbe.
TUHUMA ZA NJAMA NA MALALAMIKO YA NDANI
Taarifa zisizo rasmi (“za chini chini”) zinaeleza kuwa uteuzi wa Wakili Nyamwelo unadaiwa kuwa na lengo la kuwakata wagombea wengine ili kumwachia nafasi mgombea mmoja abakie peke yake, hali inayodaiwa kuhatarisha uhalali wa uchaguzi.
Aidha, baadhi ya wajumbe wa Kamati Tendaji ya FRAT Mkoa wanaomaliza muda wao wanadaiwa kupinga vikali uteuzi huo, wakieleza kuwa haukufuata taratibu za kikatiba na haukuhusisha jopo lote la Kamati Tendaji. Malalamiko hayo tayari yameripotiwa ngazi za juu kwa ajili ya uamuzi.