11/04/2023
KESHA LA ASUBUHI LA WATOTO NA VIJANA.
SIKU YA 101
(Aprili 11)
*Daudi Awahesabu Israeli - 2 Samweli 24 na 1 Mambo ya Nyakati 21*
🌻Daudi alimkasirisha Bwana kwa kuhesabu watu. Shetani alimwingia na akamwita Yoabu na kumwambia aende akahesabu Israeli na Yuda. Hata naye Yoabu aliyekuwa na shida za kiroho nyingi, na ukatili pia, aliona hili ni makosa. Akamwambia azunguke katika makabila yote “apate kujua jumla ya watu hao.” Hii haikuwa sensa ya kawaida, maana tunaona watu wamehesabiwa kuanzia watoke Misri, na hata kuna kitabu cha Hesabu cha kuhesabu watu. Yoabu kwa hekima akasema, “BWANA, Mungu wako na awaongeze watu hesabu yao ikiwa yoyote mara mia, tena macho ya bwana wangu mfalme na yawaone; ila kwa nini neno hili limempendeza bwana wangu mfalme?” Yoabu akaongeza “kwa nini awe na sababu ya hatia katika Israeli?” Lakini neno la mfalme likawa na nguvu juu ya Yoabu na juu ya majemedari wa jeshi, naye akatoka na majemedari wa jeshi machoni pa mfalme na kwenda kuwahesabu watu wa Israeli. Wakavuka Yordani wakafanya sensa wakienda makabila yote hata mipakani, ikawachukua miezi tisa na siku ishirini. Siku zile ambazo teknolojia ilikuwa ndogo, ilichukua muda kuhesabu watu, kwa mwendo wa mguu na nyumba kwa nyumba. Mfalme alitaka watu wahesabiwe wa umri wa kuwa jeshini, ili ajivunie kwamba jeshi lake ndilo kubwa na pengine anashinda kwa sababu ya maarifa, teknolojia au jeshi lake kubwa. Yoabu akamwambia watu ambao ni zaidi ya miaka 20 ambao wanaweza kusajili jeshi ni 800,000 katika Israeli na 500,000 katika Yuda. Ila hawakuhesabu Walawi na Benjamini kwani hakuafikiana na wazo la mfalme. Hapa Yoabu alikuwa sawa. Je ni mara ngapi nasi tungependa watu wa kanisa letu au kikundi chetu wawe namba kubwa ili tujigambe kwa namna fulani baada ya kuijua hiyo namba?
🌻Basi moyo wake Daudi ukamchoma baada ya kuwahesabu Israeli, naye Daudi akaungama kwa BWANA kwamba amekosa sana kwa aliyofanya. Akasema, “nakusihi uuondolee mbali uovu wa mtumishi wako; kwani nimefanya upumbavu kabisa.” Inaonekana alikiuka masharti yaliyo wazi kabisa kutoka kwa Mungu. Daudi alipoamka asubuhi, Gadi, nabii, alimjia akiwa ametumwa na Mungu kwamba achague adhabu moja kati ya tatu. Ya kwanza, miaka saba ya njaa ije nchini, ya pili, miezi mitatu akimbie mbele ya adui zake huku wakimfuatia, au achague siku tatu iwe tauni katika nchi. Akamwambia mfalme afanye shauri, afikiri papo hapo, ili amrudishie jibu “Yeye aliyemtuma.” Daudi akaingia mashaka sana, na kusema “sasa na tuanguke katika mkono wa BWANA kwa kuwa rehema Zake ni nyingi; wala nisianguke katika mkono wa wanadamu.” Basi BWANA alileta tauni toka asubuhi mpaka jioni, na wakafa watu 70,000, ila malaika aliponyosha mkono Wake kuelekea Yerusalemu ili auharibu, BWANA akaghairi katika mabaya, na kumwambia yule Malaika “yatosha sasa ulegeze mkono Wako.” Naye Yule malaika wa BWANA Alikuwako karibu na kiwanja cha kupuria cha Arauna Myebusi. Daudi alipomwona malaika aliyepiga watu, akaanguka kifudifudi na kusema, kwamba ni yeye mfalme aliyekosa na kupotoka, “Lakini kondoo hawa, wamefanya nini? Mkono wako na uwe juu yangu, na juu ya nyumba ya baba yangu.” Basi Gadi nabii akaenda kwa Daudi akamwambia akwee na kumwinulia BWANA madhabahu penye kiwanja cha Arauna, Myebusi. Daudi akakwea huko k**a BWANA alivyoamuru, na Arauna alipomwona mfalme, alitoka na kusujudu kwa mfalme kifudifudi hata nchi na kusema, “bwana wangu mfalme amenijia mtumwa wake kwa kusudi gani.” Naye Daudi akasema makusudi yake, ni kununua kiwanja chake ili amjengee BWANA madhabahu, ili kwamba adhabu ya tauni pate kuzuiliwa katika watu.
🌻Arauna akamwambia akichukue tu, “akatolee yaliyo mema machoni pake”. Kisha akampa mfalme ng’ombe wa sadaka ya kuteketezwa, vyombo vya kupuria, kuni, na vitu vyote akisema, “Ee mfalme, mimi Arauna nakupa wewe mfalme, … Bwana Mungu wako na akukubali. Lakini mfalme akamwambia Arauna, la sivyo, sitachukua kwako bure bali nitavinunua vitu hivi kwako kwa thamani yake; sitamtoelea BWANA, Mungu wangu, sadaka za kuteketezwa
zisizonigharimu.” Daudi akakinunua kiwanja cha kupuria na wale ng’ombe kwa shekeli hamsini za fedha na shekeli 600 za dhahabu kwa uzani; naye akamjengea BWANA madhabahu huko, akatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani, na BWANA akaikubali sadaka yake, akaibariki nchi na tauni ikazuiliwa katika Israeli.
Daudi alikubali dhana ya kidunia ya mafanikio; ufanisi ulipimwa kwa ukubwa wa jeshi. Kiburi na tamaa mbaya ndiyo iliyomchochea mfalme kuchukua hatua hiyo. Ukuu wa Israeli k**a watu wa Mungu haukuja kutokana na ukubwa wa jeshi Lake, au utisho Wake kwa mataifa. Ukuu wao ulipatikana katika utii wao kwa Mungu wao, na Mungu aliwafanya kuwa kichwa na si mkia, kwani Mungu alikuwa ameahidi, akisema: Itakuwa utakaposikia sauti ya Bwana, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya Maagizo Yake yote nikuagizayo leo, ndipo Bwana, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani; na baraka hizi zote zitakujilia na kukupata usikiapo sauti ya Bwana, Mungu wako. Utabarikiwa mjini, utabarikiwa na mashambani. Utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, na uzao wa wanyama wako wa mifugo, maongeo ya ng'ombe wako, na wadogo wa kondoo zako. Litabarikiwa kapu lako, na chombo chako cha kukandia unga (Kumb 28).Ilikuwa ni katika kutimiza ahadi hii kwamba Mungu alikuwa amepigana na kushinda kwa niaba ya Israeli katika vita vyote walivyopigana. Sio ukubwa wa jeshi lao ndiyo ulishinda vita. Kupima mafanikio kwa njia ya ulimwengu kulimfanya Daudi atende dhambi nzito.
🌻Ikiwa maombi zaidi yangetolewa katika vyumba vyetu vya Sanitarium vya wagonjwa wa muda mrefu kwa ajili ya uponyaji wa wagonjwa, nguvu kuu ya Mponyaji ingeonekana. Wengine wengi wangeimarishwa na kubarikiwa, na magonjwa mengi ya dharura (papo hapo) yangeponywa.
*🌻Nabii Gadi alimwambiaje Daudi? Kwanini si vizuri kujigamba kamba mna washiriki wengi? Mungu anapenda hesabu hata ana kitabu cha Hesabu, kwanini alichukizwa na wazo la Daudi? Daudi alichagua adhabu gani? Daudi alimwambia nini Arauna? Kwa nini sadaka wanazotupatia watu kutoa tukiwa na zetu, ni wao wametoa na wala si sisi?*
MUNGU AKUBARIKI SANA MTOTO NA KIJANA WA YESU