
06/09/2025
JESHI LA POLISI WAANZA UCHUNGUZI VIDEO YA MTOTO KUPEWA POMBE
Jeshi la Polisi Tanzania limeeleza kusikitishwa na video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii, inayoonesha mwanamke mmoja akimnywesha pombe mtoto mdogo.
Kitendo hicho kinatajwa kuwa ni ukatili wa hali ya juu dhidi ya mtoto, na ni kosa la jinai linalokiuka sheria za nchi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi hilo iliyotolea leo September 6,2025, tukio hilo linakiuka Sheria ya Mtoto, Sura ya 13 pamoja na marekebisho ya mwaka 2023 kifungu cha 9(3) na 13, na pia Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 kifungu cha 169A, k**a ilivyorekebishwa mwaka 2023.
Jeshi la Polisi limesema uchunguzi wa kina umeanza mara moja, ili kubaini iwapo tukio hilo limetokea ndani ya mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kuhakikisha mhusika anapatikana na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Jeshi hilo pia linatoa wito kwa yeyote anayemfahamu mwanamke huyo kutoa taarifa kwa njia yoyote ile iliyo rahisi kwake, au kupitia namba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi, 0699 998899.
Aidha, mwanamke huyo ametakiwa kujisalimisha mwenyewe katika kituo chochote cha Polisi mara tu atakapoona taarifa hii.
Jeshi la Polisi linakemea vikali vitendo vya ukatili dhidi ya watoto, na linaendelea kusisitiza kuwa litaendelea kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria ili kulinda haki na ustawi wa watoto wote nchini.