19/12/2021
MIAKA 700 YA WACHAGGA - 59
MAISHA YA KILIMANJARO BAADA YA UHURU WA TANGANYIKA 1961.
Tumeweza kuona kwamba baada ya uhuru wa Tanganyika taratibu maendeleo ya Kilimanjaro yalianza kufifia na kudumaa kwa sababu ya udumavu wa taasisi za kiuchumi na kisiasa zilizokuwa zimejengwa, kuimarishwa na kuboreshwa zaidi kwa ajili ya kusukuma maendeleo ya Kilimanjaro kwa makusudi karibu miaka 40 kabla ya uhuru wa Tanganyika.
Taasisi hizi zilianza kudumaa, kutelekekezwa na baadaye zote kufutwa kabisa moja baada ya nyingine na serikali mpya ya awamu ya kwanza ya Tanganyika/Tanzania chini ya Rais Nyerere. Japo hili lilikuwa ni pigo kubwa kwa Kilimanjaro lakini wachagga waliendelea kupambana katika hali hiyo hiyo ya udumavu huku taasisi muhimu za uongozi zikibadilika na mfumo uliokuja ni wa kuletewa viongozi kutoka kwenye serikali kuu tofauti na viongozi ambao wachagga waliwachagua wenyewe k**a ilivyokuwa inafanyika kabla ya uhuru wa Tanganyika.
Kwenye serikali ya awamu ya kwanza chini ya Rais Nyerere mambo yaliendelea hivyo lakini miaka michache baadaye sera ya serikali ilibadilika na kuzidi kujenga ukiritimba zaidi baada ya nchi ya Tanzania kuamua kufuata sera za kiuchumi na hata kisiasa za mrengo wa kushoto na mwaka 1967 likafanyika Azimio la Arusha ambalo lilikuwa azimio lililoweka sera kamili za kuiingiza nchi kwenye siasa na uchumi wa mrengo wa kushoto.
Sera za kiuchumi za mrengo wa kushoto ambazo msingi wake ni serikali kumiliki njia zote za kiuchumi zilikuja na mpango maalum wa kutaifisha biashara zote na mali zote zilizokuwa zinamilikiwa na taasisi binafsi pamoja na watu binafsi na kuzifanya ni mali ya serikali ambapo ilikuwa kila mtu anakabidhi biashara zake na kuiachia serikali kuziendesha.
Vitu k**a mashule yaliyokuwa yanamilikiwa na taasisi mbalimbali hasa taasisi za dini, vyuo vilivyokuwa vinamilikiwa na taasisi mbalimbali, mahospitali na vituo vya afya vilivyokuwa vinamilikiwa na taasisi binafsi, majengo makubwa, viwanda, maduka ya watu binafsi madogo kwa makubwa, mabenki na mashamba makubwa ya wafanyabiashara walioitwa “walowezi” na mashamba makubwa ya wachagga wenyewe ambapo tayari kuna ambao walikuwa wanamiliki mashamba makubwa na matrekta ya kisasa, vyote vilitaifishwa na serikali ya awamu ya kwanza chini ya Rais Nyerere.
Wakulima wakubwa wachagga na wageni huku wageni wengine wakiwa ni raia wa Tanzania waliondoka kwenye mashamba haya kupisha sera ya serikali ya utaifishaji wa mali zote ndani ya nchi baada ya Azimio la Arusha.
Mashamba haya yalikuwa yanafanya vizuri sana kabla ya huu utaifishaji lakini baada ya utaifishaji mashamba haya kwa sehemu kubwa yalitelekezwa na kudorora kabisa na serikali ilifanya haraka sana katika utaifishaji huu licha ya kwamba baada ya utaifishaji haikueleweka kwa nini serikali iliharakisha sana kuyataifisha huku ikiwa haina mpango wowote mkubwa wa maana wa kuyaendeleza, zaidi ilionekana ni k**a inataka tu kuhakikisha inakamilisha adhma ya kuifanya nchi kuwa ya kijamaa.
Serikali ya awamu ya kwanza iliyokuwa inaongozwa na Rais Nyerere iliamini kwamba inahitaji kumiliki njia zote za uchumi kwa kutaifisha biashara zote ndani ya nchi ili iweze kutoa huduma kwa usawa kwa watu wote. Hii ilikuwa ni sera ambayo ilichukuliwa kutoka kwenye nchi zilizokuwa na sera ya mrengo wa kushoto iliyopata umaarufu k**a siasa za kijamaa na kikomunisti.
Hata hivyo kwa upande wa mashamba makubwa hata baada ya serikali ya awamu ya kwanza kuyataifisha kwa sehemu kubwa haikufanya chochote zaidi ya kuyatelekeza kwa miaka mingi kukiwa hakuna chochote kinachofanyika. Baadaye baada ya mashamba haya kueguka kuwa mapori bila kuwa na uzalishaji wowote wa maana yalikuja kugawanywa kwa vyama vya msingi vya ushirika vilivyoaminiwa kwamba viko kijamaa na vitafufua kilimo katika mashamba haya. Lakini hata hivyo kwa sababu ya changamoto mbalimbali vikiwemo kukosekana kwa mitaji, maarifa na uzoefu, vyama hivi navyo vilishindwa kufufua mashamba haya pia.
Baada ya utaifishaji wa mali zilizokuwa zinamilikiwa na sekta binafsi kupitia taasisi binafsi na watu binafsi serikali ya awamu ya kwanza iliongeza wigo wa kutoa huduma za elimu na afya bila malipo kwa wananchi walio wengi. Hata hivyo kutokana na serikali kukosa uzoefu wa uendeleshaji wa biashara ambazo ilizichukua kwa watu na taasisi binafsi na kutokana na mambo kuendeshwa kisiasa na kiserikali kwa namna ya kutafuta umaarufu wa kisiasa mambo yalianza kwenda kombo huku wakurugenzi na maafisa wa serikali wakitumbukia kwenye vitendo vya rushwa iliyokithiri.
Watu wengi hasa wa vijijini walianza kupata changamoto kupata huduma hizi zilizoanza kutolewa na serikali k**a ununuzi wa vitu kwenye maduka na huduma nyingine kwenye taasisi nyingine k**a kwenye mashule na mahospitali kwani ilihitaji kujuana au kutoa rushwa kwa maafisa hawa ili kuweza kupewa kipaumbele kutokana na uhaba ulioanza kujitokeza uliotokana na ukiritimba wa serikali yenyewe.
Uhaba huu uliotokana na ukiritimba ulioambatana na rushwa iliyokithiri ilipelekea kukosekana kwa pembejeo muhimu na huduma nyingine kwa wakulima wa kahawa Kilimanjaro na kuzidi kudidimiza na kudumaza ustawi wa Kilimanjaro ambao bado ulikuwa unategemea sana zao la kahawa.
Rushwa iliendelea kutawala kwa kiasi kikubwa na kudhoofisha mambo mengi sana Kilimanjaro kuanzia elimu, afya, kilimo, uchumi na mambo mengine yaliyokuwa yamepiga hatua kubwa kabla ya uhuru wa Tanganyika ambapo rushwa ilitawala kwenye kila taasisi ya serikali ambayo ndio ilikuwa inatawala Kilimanjaro baada ya mifumo ya utawala iliyokuwepo kabla ya uhuru wa Tanganyika kufutwa.
Kipindi hiki ndio kipindi ambacho vigogo wa serikali walianza kuonekana ni watu muhimu na wa hadhi ya juu, kuogopwa na kuwa na sauti kubwa dhidi ya watu wengine ambao hawakuwa serikalini hasa katika nafasi za juu na haikuwa rahisi kushindana naye bila kujikuta kwenye matatizo.
Rushwa na ufisadi vilikithiri lakini kutokana na kwamba serikali haikuwa tayari kukiri kwamba kuna rushwa na badala yake kutumia propaganda kutangaza kwamba hakuna rushwa na serikali ya awamu ile ni safi na hakuna mtu aliyeruhusiwa kuongea kitu chochote kinyume na vile inavyotaka serikali huku vyombo vya vyote vya habari vikimilikiwa na serikali pekee, rushwa iliongezeka sana na kudumaza kabisa shughuli za kiuchumi na huduma za kiserikali pia.
Baada ya sera ya utaifishaji wa mali za taasisi binafsi sambamba na zile za watu binafsi kushindwa vibaya na kupelekea uchumi wa nchi kudorora sana, baadaye mwishoni mwa utawala wa awamu ya kwanza serikali ilirudisha baadhi ya biashara kwa watu binafsi zikiwa zimeporomoka kabisa na nyingi zikiwa hazina mitaji k**a zilivyokuwa nao wakati zinataifishwa na serikali ambapo nyingi zilikufa kabisa kwa kukosa mitaji.
Hata hivyo urudishwaji wa biashara hizi haukuzingatia zilipochukuliwa, zipo biashara nyingi ambazo zilipewa watu wengine kwa namna ya upendeleo na kujuana ili mradi kurudishwa kwa watu binafsi na zile zilizobahatika kurudishwa kwa wahusika zilirudi zikiwa zimefilisika kabisa na bila kuwa na mtaji wowote, na kwa sababu wakati zinachukuliwa wahusika hawakulipwa pesa yoyote ya fidia walirudishiwa hizi biashara wakiwa hawana mtaji na hivyo nyingi ziliishia kufa kwani hata biashara ya kahawa ambayo ndipo wachagga wengi walipatia huko mitaji ya kuanzisha biashara hizi ilikuwa imedorora sana na hivyo kukosa msingi wa mtaji wa kufufua tena biashara hizo. Kwa upande wa taasisi binafsi hasa taasisi za kidini nyingi zikiwa zimetaifishiwa mashule na mahospitali hazikurudishiwa mali zao isipokuwa shule chache sana.
Taasisi nyingi zinazotoa huduma za elimu na afya zilibaki kuwa ni za serikali mpaka leo kwa mfano chuo cha ualimu Marangu na vinginevyo. Mabadiliko pekee yaliyokuja kufanyika baadaye ni kutungwa kwa sheria ya kulinda mali za taasisi hizi ambapo taasisi za kidini na nyingine za binafsi ziliruhusiwa kujenga shule nyingine kwa mkataba kwamba serikali haitakuja kuzitaifisha tena k**a jinsi ilivyofanya mwanzo na kuziingiza taasisi hizi kwenye matatizo makubwa, uliopata umaarufu k**a Memorandum of Understanding(MoU).
Wachagga hawakuendana nayo wala kuipenda sera ya ujamaa kwa sababu kwanza kuanzishwa kwake kulidhoofisha zaidi vyama vya ushirika ambavyo vilikuwa na manufaa makubwa Kilimanjaro na baada ya muda vikafutwa kabisa. Pili sera hii ya ujamaa ilipelekea mali nyingi za wachagga kutaifishwa na serikali kwa namna ya k**a kunyang’anywa ambazo zilikuwa zimetafutwa kwa muda mrefu na kwa hali na mali na hivyo hata nje ya uchumi wa kahawa wachagga waliathirika zaidi kwenye biashara nyingine hivyo kupelekea uchumi wa Kilimanjaro kuanguka kabisa.
Hakuna mtu aliyejali mfumo uliokuwepo ulikuwa na faida kiasi gani wala ulikuwa na umuhimu kiasi gani, badala yake ilikuwa ni amri tu kwamba mali zote zitataifishwa na kufanywa za umma na kuendeshwa na serikali. Taasisi mbalimbali Kilimanjaro pamoja na wachagga wenyewe waliona wazi kwamba nchi inaenda kuangukia kwenye mfumo wa kikomunisti na kuona wazi kwamba Kilimanjaro inaenda kudhoofika sana.
Namna sera hizi za kijamaa zilivyokuwa zinatekelezwa wachagga walishindwa kuzielewa kabisa na kupata mtazamo hasi sana juu yake na kufikiri kwamba zimetengenezwa makusudi kuwaumiza na kuwasababishia msongo mkubwa wa mawazo.
Hata hivyo serikali ya awamu ya kwanza ilijaribu kutumia makanisa kujenga ushawishi kwa watu kuukubali ujamaa. Rais Nyerere mwenyewe alitumia kanisa na viongozi wa dini kueneza propaganda za sera za ujamaa kujaribu kupunguza mtazamo hasi juu ya ujamaa ili kuwaondoa watu wasiwasi kwamba hakukuwa na agenda za siri zilizojificha katika kuibadilisha nchi kuwa ya kikomunisti.
Hata hivyo bado hiyo haikutosha kuwashawishi wachagga kuukubali ujamaa baada ya kuwa biashara zao zote mpaka biashara ndogo ndogo kabisa mitaani na vijijini zikiwa zimetaifishwa na serikali huku wao hawajalipwa hata fidia na badala yake zimechukuliwa na maafisa wa serikali na badala yake sasa wanapata huduma kwa shida sana na hata wakati mwingine kulazimika kutoa rushwa kwa biashara ambazo zilikuwa ni za kwao wenyewe.
Vyama vya ushirika vikiwa vimefutwa na kuletwa taasisi nyingine kutoka serikali kuu ambao hawakuwa wana uelewa wowote mpana juu ya vyama hivyo na uzoefu wa kilimo hususan cha kahawa. Hiyo ilipelekea wakulima walipohitaji ushauri wa kitaalamu walijikuta wakulima wenyewe wana uwezo mkubwa na uelewa mpana wa kitaalamu kuliko hata wale walioletwa na serikali kuu kwa jukumu hilo, badala yake maofisa wengi wa serikali walijikuta wanageuka kuwa wabadhirifu na wala rushwa.
Tabia ya uvivu na kutojali ilishika kasi sana na wasimamizi waliokuwa wameletwa na serikali kuu ya Tanzania hawakuwa wanajali sana kazi hizo wala kuwa na shauku yoyote nazo na badala yake walijikuta wanashinda maofisini wakipiga hadithi na wengine kuamua kwenda kujishughulisha na biashara zao mbalimbali ili kuweza kupambana na hali ya maisha wakati huo mishahara yao ikiwa ni duni sana.
Hali hii ya uzembe na uvivu wa watumishi wa serikali ndio ilikuwepo miaka ya baada ya uhuru wa Tanganyika tofauti na kipindi cha Mangi Mkuu ambapo watu walikuwa wanajua lengo lao kiuchumi na wengi wakiwa sehemu ya kunufaika na kilimo biashara cha mazao hususan zao la kahawa basi walikuwa wakihamasika sana kuweka bidii kubwa na hivyo hakukuwa na uzembe wala uvivu wa kiasi hiki.
Wakati wa kipindi cha utawala wa Mangi Mkuu kazi zilifanyika kwa kujituma sana bila kisingizio wala kujali ugumu wa mazingira ya kazi lakini baada ya uhuru wa Tanganyika maofisa wapya walioletwa na serikali kuu walikuwa hawaishi visingizio hasa kusingizia kwamba hawana vifaa k**a vile usafiri au vitu vingine muhimu na hivyo maofisi yakageuka zaidi kuwa maeneo ya kwenda kupumzika badala ya kufanya kazi.
Ofisi hizi ambazo wakati wa utawala wa Mangi Mkuu zilijikita zaidi kwenye kufanya kazi zikiongozwa na kauli mbiu mbalimbali za kazi, lakini baada ya uhuru wa Tanganyika na viongozi kuletwa kutokea maeneo mengine siasa za itikadi zilianza kushika kasi na watu kuongea na kusambaza propaganda za chama na serikali ya awamu ya kwanza ikawa ndio tabia mpya inayojijenga na inayowapa watu kujulikana na kupandishwa vyeo au kupelekwa kwenye fursa kubwa zaidi hasa baada ya Azimio la Arusha.
Azimio la Arusha ndio lilikuja na ari kubwa zaidi katika kufanya propaganda na kutukuza itikadi ya chama na kutukuza viongozi na fikra za viongozi hasa Mwenyekiti wa chama Rais Nyerere ambapo kulikuwa na kauli mbiu kabisa ya kwamba "zidumu fikra za Mwenyekiti" badala ya kuweka “fokasi” kwenye kazi na kufuata ushauri wa wataalamu na sio maneno ya siasa.
Taasisi zote ambazo zilijengwa na wachagga kwa hali na mali kwa zaidi ya miaka 40 kabla ya uhuru wa Tanganyika na kuleta mabadiliko na maendeleo makubwa Kilimanjaro na ambazo ndizo zilizokuwa msingi wa maendeleo makubwa Kilimanjaro hazikuwahi kuonekana k**a zina maana yoyote wala kukubalika, zaidi ya kuishia kudhoofika na baadaye kufutwa kabisa. Sera zilizotekelezwa ni zile ambazo zililetwa na serikali kuu ya Tanzania.
Watu walioletwa Kilimanjaro kwa ajili ya utekelezaji wa sera hizo hawakuwa na uwezo wala uzoefu wa namna mambo yalikuwa yakifanyika Kilimanjaro na hivyo zile huduma mbalimbali kwa wakulima(extended services) zilizokuwa zinatolewa kipindi cha Mangi Mkuu vijijini ni k**a zilipotea kabisa na wakulima Kilimanjaro walipohoji au kuhitaji huduma hizo kwa ajili ya kuhakikisha mavuno yanakuwa yenye ubora wa viwango sahihi waliitwa wavivu, wazembe, wasio na uzalendo na wenye mitazamo ya kikoloni.
Hii iliwakatisha sana tamaa wachagga na hawakuwahi kuiamini serikali ya Tanganyika/Tanzania ambayo iliwakuta kwenye mafanikio makubwa na kasi kubwa ya kimaendeleo kuelekea kwenye utajiri na kudororesha uchumi na kuwarudisha nyuma kwenye hali ngumu ya maisha na hivyo kupelekea wachagga kujenga mtazamo kwamba sera yoyote ya serikali inayokuja Kilimanjaro ina lengo baya la kuwaumiza na kuwadhoofisha. Katika nyakati hizi hizi ilianzishwa sera ya serikali ambayo huwa ni maarufu k**a “quota” juu ya ufaulu wa wanafunzi wanaojiunga na elimu ya sekondari.
Sera hii ilikuja na hoja kwamba Kilimanjaro watu wameshasoma na hivyo hawapaswi kupewa kipaumbele na badala yake wanatakiwa wasubiri watu wa maeneo mengine ya Tanzania wasome kwanza. Hivyo alama za ufaulu kwa watu wa Kilimanjaro zilipandishwa kufikia angalau 85% ili kuweza kuchaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari wakati huo mikoa mingine watu walihitajika kupata angalau 55% kuweza kuchaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari.
Sera hii ilijumuisha shule za sekondari zilizokuwepo Kilimanjaro ambazo ndio zilikuwa nyingi zaidi kuanzia zile zilizojengwa na wachagga wenyewe kupitia KNCU mpaka zile ambazo zilikuwa zinamilikiwa na taasisi za kidini Kilimanjaro ambazo pia zilijengwa na wachagga kwa kushirikiana na viongozi wa dini lakini zikataifishwa na serikali ya awamu ya kwanza na serikali kugoma kabisa kuzirudisha kwenye taasisi binafsi zilikotaifishwa.
Serikali ya awamu ya kwanza iliyoongozwa na Rais Nyerere ilikuja na hoja hii kwamba mikoa mingine inatakiwa iendelee kwanza kuifikia Kilimanjaro tuwe sawa ndio fursa zirudi kawaida kwa hivyo Kilimanjaro italazimika kupunguza kasi ya maendeleo mpaka hayo maeneo mengine ya nchi yaendelee kwanza na watu wa huko wasome kwanza kufikia kiwango cha Kilimanjaro, japo hata hivyo haikujulikana ni lini muda huo utafika kwani hakuna tarehe kamili iliyopangwa kwamba mpaka mwaka fulani.
Kwa bahati mbaya zaidi hakukuwepo hata na mbadala wala shule binafsi ambazo watu wangeweza kusoma baada ya kukosa fursa kwenye sekondari za serikali kwani serikali ilikuwa imetaifisha shule zote ikiwa ni pamoja na zile za dini zilizokuwepo Kilimanjaro pamoja na zile zilizojengwa na wachagga wenyewe kupitia KNCU na hivyo wachagga walilazimika kufuata maamuzi ya serikali juu ya sera hii ambayo wenyewe waliiona k**a sera iliyotungwa ili kuwabagua na kuwarudisha nyuma kimaendeleo kwa makusudi. Wachagga walijiona kwamba ni k**a wanapewa adhabu kwa kosa ambalo hawajafanya wao, kwa sababu wao hawahusiki chochote kwa maeneo mengine ya nchi kuwa nyuma kimaendeleo.
Wachagga waliona kwamba huu ni k**a mpango ovu uliopangwa dhidi ya wachagga na Kilimanjaro na sera hii ya serikali ya awamu ya kwanza waliiona kuwa imejaa ubaguzi ndani yake na lengo lake lilikuwa ni kuwakomoa wachagga na kuwanyima elimu kwa kipindi kirefu kisichojulikana. Wakati wachagga wanaiona sera hii k**a sera ya kibaguzi na inayowaumiza, maeneo mengine ya nchi waliifurahia na kuiona iko sahihi kwa sababu haikuwa inawaumiza lakini kwa kuwa ndio wengi na wanaoipa nguvu serikali na zaidi kupitia propaganda za serikali ya awamu ya kwanza, sera hii ilipata uhalali wa kupitishwa na kuingizwa kwenye utekelezaji.
Wachagga walitegemea fursa ziwe sawa kwa kila mtu na sio kupitisha sheria zinazoleta ubaguzi na kuwanyima fursa watu wenye uwezo mkubwa wanaotokea Kilimanjaro huku watu wenye uwezo wa kawaida kutoka maeneo mengine ya nchi wakipewa nafasi.
Hata hivyo baada ya sera hii kuingizwa kwenye utekelezaji wachagga wengine waliamua kubuni mbinu mbadala kukabiliana na sera hii ya serikali ya awamu ya kwanza iliyokuwa inabagua wachagga kwenye eneo la elimu ambayo waliifanya kimya kimya. Mikoa mingine ilikuwa na utoro mkubwa wa wanafunzi na hivyo kwa kujua kwamba kupata alama za ufaulu ukitokea mkoa wa Kilimanjaro imekuwa ni changamoto, kwa siri wachagga walianza kualikwa kwenda kununua nafasi hizi zilizokuwa zinaachwa wazi kwenye mikoa mingine kwa sababu ya utoro wa wanafunzi.
Hivyo mikoa hii ambayo ilikuwa na utoro mkubwa kwa sababu mbalimbali k**a vile binti kuolewa akiwa bado yuko shuleni, vijana kutakiwa kwenda machungani na sababu nyinginezo zilizopelekea nafasi nyingine kupatikana wachagga wengi walizinunua na kuzitumia. Kwa sababu ufaulu kutoka mikoa hii kwenda sekondari ulikuwa rahisi wachagga wengi waliochukua hatua kununua nafasi hizi kwa kuingia maelewano na wakuu wa shule hizo na kusoma kwenye mikoa mingine wengi waliweka bidii kubwa sana kwenye masomo na walifaulu na kuendelea na masomo ya sekondari, tofauti na Kilimanjaro ambako ni wanafunzi wachache sana walikuwa wanafaulu na mara nyingi shule nyingi zilikuwa zinatoa kapa bila kufaulisha hata mwanafunzi mmoja kutokana na alama za ufaulu kuwekwa juu sana kwa wanafunzi wanaotokea Kilimanjaro.
Hata hivyo haikuchukua muda mrefu wachagga waliokuwa wananunua nafasi hizi ili kusoma kwenye mikoa mingine walianza kugundulika kwamba kuna ujanja wanatumia. Kwa sababu taarifa zilipelekwa kwenye uongozi wa juu kwamba wanashangaa kuona kwamba majina ya ukoo wa kichagga k**a Lyimo, Shayo, Mrema, Kileo, Massawe n.k. wanatokea mikoa mingine kwa wingi isivyo kawaida katika kuchaguliwa kwenda Sekondari. Ilikuwa inawashangaza kuona watu wa ukoo wa Shirima kutokea mkoa wa Mtwara au Lindi au mtu wa ukoo wa Mushi anatokea mkoa wa Tabora, ndipo walipoanza sasa kufuatilia watu kwa majina yao ya ukoo kuhakikisha kwamba wachagga hawapigi chenga na kupita njia mbadala ili kusoma sekondari k**a walivyokuwa wanafanya.
Baada ya mbinu hii ya wachagga kununua nafasi kwenye mikoa mingine ili kurahisisha kupata fursa ya kujiunga na elimu ya sekondari kujulikana, wachagga walikuja na mbinu nyingine mpya ya kununua jina la mtu wa mkoa husika na kulitumia k**a lilivyo ambapo hapa wachagga walilazimika kujitahidi sana kuficha utambulisho wao halisi kwa hali na mali ili wasijulikane kwamba wametokea mkoa wa Kilimanjaro na walihakikisha majina bandia waliyokuwa wananunua ndio majina pekee yanayojulikana.
Mbinu hii ya kutumia majina bandia ya watu wa mikoa mingine iliwasaidia sana wachagga kuendelea kielimu katika mazingira ambayo yaliwabana sana kwenye fursa za elimu. Lakini hata hivyo bado sio wote wamefanikiwa kupona moja kwa moja kwenye mbinu hii ya kutumia majina ya wengine kwani wengi ndio hao waliokuja kushutumiwa kuwa na vyeti feki na serikali ya Magufuli ya awamu ya tano na kufukuzwa kazi bila kulipwa mafao yao. Wengi zaidi walioumia katika sakata hilo la vyeti feki walikuwa ni wachagga na wengi walinunua majina hayo kipindi hicho cha awamu ya kwanza chini ya Rais Nyerere kutokana na sera ya elimu iliyowagua na kuwabana.
Hata hivyo baada ya sera za ujamaa zilizoletwa Tanzania na serikali ya awamu ya kwanza kufeli vibaya sana hasa kuanzia miaka ya 1970’s na 1980’s na kusababisha anguko kubwa sana la uchumi Tanzania na mambo mengi kudorora sana Rais Nyerere alikubali kuachia madaraka baada ya kukaa madarakani kwa karibu miaka 25 na kumpisha madarakani Rais Ali Hassan Mwinyi.
Rais Ali Hassan Mwinyi japo alirithi mifumo iliyojaa ukiritimba wa serikali ambayo haikuwa mizuri kwa ukuaji wa uchumi kutoka kwa Nyerere lakini Mwinyi yeye alikuja na sera nzuri za kuchochea ukuaji wa kiuchumi kwa kupunguza sana ukiritimba wa serikali katika kuhodhi njia za uchumi na kuruhusu sekta binafsi kuanza kukua tena kupitia taasisi binafsi kuanza kujijenga katika kumiliki njia za kiuchumi.
Sera nyingi zilizokuwa zinakwamisha maendeleo ya kiuchumi kwa mfumo wa uchumi kumilikiwa na serikali na kusababisha mdororo mkubwa wa kiuchumi wakati wa awamu ya kwanza ya Rais Nyerere ziliondolewa kwa kiasi kikubwa na hivyo taratibu uchumi wa nchi ulianza kukua tena na biashara Kilimanjaro zilizokuwa zimepoteza kabisa mwelekeo zilianza kupata matumaini japo wachagga wengi walikuwa wamepoteza ile ari ya maisha, matumaini makubwa ya kimaendeleo na mapambano makubwa waliyokuwa nayo kabla ya uhuru na miaka michache ya mwanzoni baada ya uhuru wa Tanganyika.
Taasisi za kidini zilianza kujenga tena taasisi binafsi za elimu, vituo vya afya na huduma nyingine za kijamii kwa kasi Kilimanjaro. Baada ya kuruhusiwa kujenga tena taasisi hizi wachagga walianza tena uhamasishaji wa kujenga mashule ya sekondari hasa kupitia taasisi binafsi kwa kasi ili kukabiliana na changamoto ya ukosekanaji wa shule mbadala za sekondari.
Mwaka 1992 ilipitishwa sera ya demokrasia ya vyama vingi ambayo ilizidi kujenga matumaini zaidi ya kisiasa na kiuchumi kwa Kilimanjaro na hivyo watu walizidi kuwekeza katika kuhakikisha zilipatikana shule nyingi za kutosha uhitaji kadiri ya watu watakavyoweza kumudu gharama. Wachagga pia walikuwa mstari wa mbele sana katika kuanzisha vyama mbalimbali vya kisiasa Tanzania baada ya fursa hiyo kujitokeza tena mwaka 1992 baada ya zaidi ya miaka 30 ya utawala wa kiimla wa chama kimoja.
Licha ya serikali kugoma kabisa kurudisha shule na taasisi nyingine ilizotaifisha kutoka kwa taasisi za kidini pamoja na kwamba taasisi hizi ziliiomba na kuisihi sana serikali kurudishiwa taasisi zao ilizozitaifisha na kugomewa, lakini hata hivyo haikuchukua muda mrefu Kilimanjaro ilianza tena kupata umaarufu wa kuwa na shule nyingi zinazofanya vizuri sana na wazazi wengi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi ya Tanzania walijenga mtazamo kwamba Kilimanjaro kuna elimu nzuri na wale wenye uwezo wengi walipeleka watoto wao kwenda kusoma Moshi.
Baada ya sera za serikali ya awamu ya pili Tanzania chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi kuanza kuruhusu taasisi binafsi kuanza kutoa huduma mbalimbali k**a elimu, afya n.k.,. na taasisi hizi kuanza kujengwa tena kwa kasi Kilimanjaro wachagga walipata matumaini mapya ya kusonga mbele kupitia elimu ambayo ilikuwa imekuwa changamoto sana kwao kwenye serikali ya awamu ya kwanza Tanzania chini ya Rais Nyerere iliyokaa madarakani karibu miaka 25.
Hata hivyo kwa mujibu wa Dr. Reginald Mengi kwenye kitabu chake cha “I can, I must and I will” anasema kwamba mwaka 1989 baada ya yeye na wawekezaji wengine ndani ya nchi kuwa wameanza kupata mafanikio makubwa Nyerere alijaribu kumshawishi Rais Mwinyi arudishe tena sera za Ujamaa k**a yeye alivyofanya akiwa madarakani na hivyo watu walioanza kutajirika mali zao zitaifishwe tena na kufilisiwa.
Dr. Reginald Mengi anasema kwamba Nyerere alidai kwamba ubepari na unyonyaji unarudi tena na kutolea mfano kiwanda chake cha vinywaji baridi cha Bonite Bottlers Co. Ltd kilichopo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro k**a mfano wa ubepari wa kimarekani ambao yeye binafsi anaamini ni mbaya na wa kinyonyaji. Mfanyabiashara Reginald Mengi anasema kwamba yeye pamoja na wawekezaji wenzake waliogopa sana.
Hata hivyo Nyerere alipendekeza haya bila kujali kwamba sera zake za ujamaa wa serikali kutaifaisha mali za taasisi binafsi na watu binafsi na kuhodhi njia zote za kiuchumi zilisababisha kutokea kwa njaa, umaskini mkubwa na uhaba mkubwa wa bidhaa uliopelekea watu kukosa hata mahitaji ya kawaida ya kila siku na uchumi wa nchi kuanguka vibaya sambamba na nchi kukumbwa na madeni makubwa ambayo yamekuwa mzigo kwa nchi mpaka leo.
Hata hivyo kwa mujibu wa Reginald Mengi Rais Mwinyi alikataa kabisa pendekezo hilo la Nyerere jambo lililopelekea kutokea kwa mvutano mkali na kurushiana na maneno makali kati ya Mwinyi na Nyerere kwenye mkutano wa chama na hiyo ikawa moja kati ya sababu ya Nyerere kuamua kujiuzulu uenyekiti wa chama. Endapo Rais Mwinyi angekubaliana na pendekezo hili la Nyerere ni wazi kwamba mambo yangekuwa magumu tena na hatua ambayo Kilimanjaro ilikuwa imeanza kupiga kwenye kujenga tena upya taasisi zinazotoa huduma muhimu za kijamii lisingekuwa limefanyika au kufanyika kwa kiwango kidogo k**a wangekuja kuruhusu tena baadaye.
Japo wachagga mpaka leo bado hawajaweza kupata uongozi wa wazawa uliokuwa na mafanikio makubwa lakini ukafutwa baada ya uhuru wa Tanganyika na serikali ya awamu ya kwanza lakini wameendelea kupitia taasisi binafsi na taasisi za kidini kujenga taasisi zaidi za kutoa huduma mbalimbali za kijamii mpaka sasa na vyuo vikuu mbalimbali vimeendelea na vinaendela kufungua matawi zaidi Kilimanjaro katika kutanua zaidi wigo wa elimu ya juu.
Kupitia taasisi binafsi wachagga wamejaribu na wanaendelea kupambana kuwekeza kwenye teknolojia ya habari na mawasiliano na hata ujasiriamali na hizi zimesaidia sio wachagga peke yake bali hata watanzania kwa ujumla wameendelea kunufaika na taasisi hizi.
Licha ya taasisi mbalimbali za kitaaluma kuendelea kuongezeka Kilimanjaro na wachagga mbalimbali kutoka Kilimanjaro kuendelea kubobea katika fani mbalimbali na kuendeleza uwezo mkubwa unaonufaisha taasisi mbalimbali maeneo mbalimbali duniani bado Kilimanjaro haijaweza kuja na mpango sahihi wa kuinua uchumi wa Kilimanjaro kwa viwango vya juu k**a ilivyotokea kipindi cha Mangi Mkuu.
Ukweli ni kwamba hili sio jambo linaloweza kutokea kiurahisi k**a jinsi lilivyotokea wakati wa serikali ya Mangi Mkuu kwa sababu za kimifumo pengine pamoja na za kisiasa lakini bado kuna namna nyingine nyingi za kusaidia kurudisha maendeleo na utukufu wa Kilimanjaro uliopotea bila kutegemea kupitia mifumo ya kiserikali moja kwa moja ambayo hata ukisema uitegemee itaishia kukuangusha na kujikuta mnaishia kwenye mitego ya kisiasa na kukwama.
Chama cha ushirika cha KNCU ambacho kilifanya makubwa sana zamani hasa miaka ya kabla ya uhuru wa Tanganyika kilikuja kufufuliwa na kiko hai hata sasa lakini hakiwezi kufanya tena makubwa k**a kiliyofanya zamani kwa sababu mbalimbali zikiwezo za kisiasa na kiutendaji lakini kubwa zaidi ni kukosa nia na maono na kushindwa kujenga imani na matumaini kwa wanachama ambayo yanahitaji kuongezewa nguvu na mipango na mikakati sahihi inayoongozwa na nia njema.
Ahsanteni.
CREDIT@ URITHI WETU WACHAGGA FACEBOOK PAGE. 👏👏👏🔥🔥