13/12/2024
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili na Mshauri wa Rais masuala ya Afya na Tiba, Prof. Mohamed Janabi, ametoa wito kwa Wananchi kuzingatia njia za kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza, akisisitiza magonjwa hayo kwa sasa ni changamoto kubwa kutokana na gharama na usumbufu wa kuyatibu.
Akizungumza na waandishi wa habari Desemba 12, 2024 alipokuwa akitoa salamu za Krismasi, Prof. Janabi ameeleza kuwa, amekuwa mstari wa mbele kutoa elimu kuhusu madhara ya magonjwa yasiyoambukiza kwa lengo la kuimarisha afya ya jamii.
Katika mazungumzo hayo, Prof. Janabi ameeleza mtazamo wake kuhusu ulazima wa kunywa chai asubuhi.
"Kunywa chai asubuhi sio lazima, Najua mtasema Profesa Janabi amekataza watu kunywa chai, lakini naomba niweke wazi: neno breakfast maana yake ni kuvunja funga. Mimi binafsi huanza kula saa sita mchana na kisha nakula tena saa mbili usiku."
Ameendelea kufafanua kuwa hospitalini hawajawahi kukutana na mgonjwa aliyelazwa kwa sababu ya kutokunywa chai:
"Hatujawahi kumlaza mtu hapa Muhimbili kwa sababu tu hajanywa chai, wala mtu hajawahi kufariki kwa sababu hiyo."
pia ameeleza jinsi anavyopangilia ratiba yake ya chakula akisema:
"Kuna siku nakula matunda saa sita mchana kisha nakuja kula tena saa kumi na mbili jioni. Siku nyingine, chakula cha kwanza ninaingiza mdomoni saa nane mchana na baadaye kula tena saa kumi na mbili jioni. Halafu mara moja kwa mwezi huwa nakula mara moja tu kwa siku."
Hata hivyo Prof. Janabi amesisitiza kuwa ratiba ya kula inapaswa kuzingatia mahitaji ya mwili, badala ya kufuata mazoea yasiyo ya lazima huku akihimiza jamii kufikiria afya zao kwa kuzingatia lishe bora, mazoezi, na mbinu za kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.