01/10/2022
Bismillaahi rahmaani Rahiim
Kwa hakika tumepambaukiwa na kukabiliwa na mwezi mtukufu wa RABI'UL AWAL (Mfungo sita). Mwezi ambao amezaliwa ndani yake Mtukufu wa daraja na kipenzi chake Allah Subhaanahu wataala nae si mwengine ni Mtume Muhammad Swalla Allahu Alayhi Wasallam.
Kuzaliwa kwa Mtume huyu kulileta Nuru katika dunia baada ya kipindi kirefu dunia kuzama katika Ushirikina, Dhulma, Maasi, Uhaasid, unafiki, choyo, Kutumia nguvu, Unyanyasaji wa wanawake, kutezwa nguvu, ukosefu wa haki, kujifadhilisha na kuwa bora kwa Kabila, Mali, Cheo nk.
Allah akamleta mbora wa viumbe kutoka katika pande za majabali ya bara arabu ili awe Mtume na mjumbe wake.
Aje kuiokoa na kuielekeza na kuifundisha jamii kumuabudu Mungu mmoja ambae ni Allah Subhaanahu wataala na kutomshirikisha kwa chochote katika Ufalme wake uliotukuka.
Amekuja kutuonya na kutupa bishara njema (Bashiir na Nadhiir).
Na amekuja kuilingania dini ya Allah kwa idhini yake Subhaanahu wataala.
Sharafu na utukufu wa Mtume huyu ilionekana tokea siku ulipoumbwa Ulimwengu na nuru ya Mtume Muhammad Swallahu Alayhi wasallam iliumbwa.
Hivyo Risalaah na Utukufu wake Mtume Swalla Allahu Alayhi wasallam ndio dira na muongozo wa maisha na kufaulu kwa kila binadamu na Uislam kwa ujumla.
Allah Aziidi kummiminia ziada za Rehma kila wakati na Iwe ni sababu ya kuondokewa na mashaka na matatzo yetu na maradhi na hasad kwa BarKa zake Nabia.
Waislamu tunatakiwa tuzidi na kukithirisha kumswalia Mtume Muhammad Swalla Allahu alayhi wasalam kwani tutapata thawabu, tutasamehewa dhambi zetu, tutaondokewa na mashaka yetu na shida zetu zitatatulika na kupata faraja na amani.
Waffakanallahu fiymaa yuhibbuhu Wayardhwa.