.
#AzamTVXpose Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipopita kwenye banda la UFM wakati wa utambulisho na uzinduzi wa vifaa vipya vya kurushia matangazo vya Azam TV.
Waziri Mkuu alipokelewa na kutambulishwa shughuli mbalimbali za UFM na Mkuu wa Radio, Baruan Muhuza.
#UFMRadio
Aliyekuwa Mgombea wa Uenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, Peter Msigwa amekata rufaa kwa Kamati Kuu ya chama hicho kupinga uchaguzi uliofanyika.
Amedai kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa utaratibu wa uchaguzi lakini pia baadhi ya wapiga kura walizuiwa kushiriki bila sababu yoyote.
#UFMUpdadtes
13 WASHIKILIWA KWA KUJIHUSISHA NA RAMLI CHONGANISHI KATAVI
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Kaster Ngonyani amesema wanawashikilia watuhumiwa 13 wanaojihusisha na upigaji wa ramli chonganishi.
Amesema vijana wengi wameonekana wakijihusisha na waganga wa jadi ili kujipatia kipato kwa uraisi na kujiingiza kwenye uhalifu.
#UFMUpdates
Mtoto mwenye ualbino, Kazungu Julius (9) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Katoro wilayani Geita amenusurika kifo baada ya kujeruhiwa sehemu za kichwani, mkononi na kidole cha mkono aliposhambuliwa na mtu asiyejulikana kwa kutumia kitu chenye ncha kali.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita, SACP Safia Jongo amesema tukio hilo lilitokea Mei 4 mwaka huu saa mbili usiku katika Mtaa wa Mtakuja Mamlaka ya Mji mdogo Katoro.
Amesema mtu mmoja ambaye hajajulikana alimvizia mtoto huyo akitoka chooni na kuanza kumshambulia na kitu chenye ncha kali, hali iliyosababisha majeraha makubwa mwilini.
#UFMUpdates
Jeshi la polisi mkoani Mbeya linamshikilia dereva wa lori, Said Rajab (35) mkazi wa Dar es salaam kwa kusababisha ajali ya barabarani baada ya gari alilokuwa akiendesha likiwa limebeba shehena ya mchele kupinduka katika eneo la mbembela jijini Mbeya.
Waliojeruhiwa kwenye ajali hiyo ni dereva mwenyewe, dereva wa pikipiki aliyefahamika kwa jina la Ambakisye Kyejo na utingo wa lori hilo, Kassim Husein.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP Abdi Isango amesema majeruhi hao wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya MZRH.
#UFMUpdates
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema anafanyia kazi mpango wa Bima ya Afya ya NHIF iweze kutumika kuwaona madaktari bingwa ili kuwarahisishia wananchi kupata huduma kwa gharama nafuu.
Waziri Ummy ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa kambi ya madaktari bingwa 25 watakao hudumu katika Mkoa wa Iringa kwa siku tano.
#UFMUpdates
MAKONDA ATANGAZA WIKI YA UTOAJI HAKI ARUSHA
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda ametangaza siku tatu za kusikiliza kero za wananchi wa kada zote ndani ya mkoa huo ikiwa ni pamoja na malalamiko ya migogoro ya ardhi, mirathi, biashara, ukatili wa kijinsia na madhila mbalimbali.
Makonda amesema kuwa katika siku wanasheria na wataalamu mbalimbali watakutana na wananchi wenye changamoto na kuwasaidia kupata utatuzi.
#UFMUpdates
Watu wanne wamejumuishwa kwenye kesi ya uharibifu wa bomba la mafuta la TAZAMA na kufanya idadi yao kufikia 24 ambapo inadaiwa walitoboa na kufanya uharibifu wa bomba hilo kisha kuchota zaidi ya lita laki saba za mafuta aina ya dizeli yenye thamani ya shilingi bilioni 2.2 katika eneo la Ruaha Mbuyuni Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa.
Kesi hiyo imekuja kwa mara ya tatu mahakamani hapo ambapo bado mtuhumiwa mmoja na muhimu hajapatikana ili kesi hiyo iweze kuanza kusikikilizwa.
#UFMUpdates
Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi imeanza kutenga maeneo ya viwanja kwa waathiriwa wa mafuriko katika Vijiji vya Karema, Mchangani, Ikola na Isengule ambavyo vinatajwa viko kwenye hatari kubwa ya kukumbwa tena na mafuriko kutokana na makazi ya wanavijiji hao kuwa karibu na Ziwa Tanganyika.
Akikabidhi misaada iliyotolewa na Serikali, Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko ameziagiza kamati za usalama za wilaya na mkoa kuchunguza endapo kutakuwa na ubadhirifu kwenye ugawaji wa misaada hiyo hatua kali za kisheria zichukuliwe.
Aidha, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Halima Kitumba amebainisha idadi ya kaya zilizoathiriwa na mafuriko hayo.
#UFMUpdates
Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupamabana na Rushwa mkoani humo kuchunguza matumizi ya fedha za ujenzi wa mradi wa bweni la wanafunzi wenye mahitaji maalum katika Shule ya Msingi Ipapa iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Ileje.
Agizo hilo limekuja baada ya Chongolo kukagua ujenzi wa mradi huo na kutia shaka baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa ujenzi wa mradi huo ambao unadaiwa kuanza mwaka 2022.
Mradi huo unajengwa kwa gharama ya zaidi ya shiling milioni 100 zinazotoka Serikali kuu ambapo ukikamilika utawanufaisha wanafunzi wenye mahitaji maalum zaidi ya 300.
#UFMUpdates
Jeshi la polisi Mkoa wa Pwani linamtaka aliesambaza video na maneno ya kumkashifu aliyekuwa Waziri na Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo wa zamani, Shukuru Kawambwa ajisalimishe kituo cha polisi Bagamoyo.
Aidha, Kamanda wa polisi mkoani humo, SACP Pius Lutumo amewataka wananchi wa Mkoa wa Pwani kuacha kijichukulia Sheria mkononi na badala yake wafuate utaratibu na kanuni za sheria za nchi kwenye kumaliza changamoto zozote.
Hii inakuja baada ya video iliyosambaa mtandaoni Aprili 24 mwaka huu ikimuonyesha Kawambwa akishambuliwa na kudhalilishwa kwa kutishiwa kufungwa pingu na mgambo wilayani Bagamoyo.
#UFMUpdates
WANAFUNZI WATOZWA SHILINGI LAKI MBILI KWA KUKUTWA NA SIMU
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoani Mara imebaini kuwepo kwa adhabu kandamizi katika kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nyamunga iliyopo Wilaya ya Rorya na kusema hatua hiyo si rafiki katika mifumo ya adhabu shuleni.
Mkuu wa Takukuru mkoani humo, Mohamed Shariff amebainisha hayo wakati akitoa taarifa ya miezi mitatu kwa waandishi wa habari mkoani humo kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu.
#UFMUpdates