Fanani na Hadhira

Fanani na Hadhira Fanani atasimulia, na hadhira itasikiliza. Simulizi | Makala | Chambuzi | Vitabu
(23)

DIDDY; FROM MANSION TO CUBBYHOLEKUANZIA muvi ya “Straight Outta Compton” hadi andiko la kitaaluma (dissertation) la Kris...
04/10/2024

DIDDY; FROM MANSION TO CUBBYHOLE

KUANZIA muvi ya “Straight Outta Compton” hadi andiko la kitaaluma (dissertation) la Kristen Bowen, Chuo Kikuu cha North Carolina. Documentaries za “In The Dark”, “Surviving Diddy” kisha “Freak Off Parties”. Halafu kitabu “Mercedes Ladies” cha Sherri Sher.

Kila moja inatosha kujenga picha ya mwanzo wa mwisho wa binadamu ambaye alipata kuwa kila kitu katika ulimwengu wa burudani. Sean Combs “Diddy”, zamani “P Diddy”. Miaka ya 1990, aliitwa “Puff Daddy” au simply “Puffy”.

Muvi ya Straight Outta Compton, inasimulia maisha halisi ya vijana watatu wenye vipaji na fedha kutoka Compton, California; Eazy E, Ice Cube na Dr Dre. Walikuwa memba wa Hip Hop crew ya N.W.A (Ni**az Wit Attitudes). “Straight Outta Compton” ni albamu yao ya kwanza na iligonga platinum mwaka 1988.

Ndani ya movie ya Straight Outta Compton, kilichowasilishwa k**a uhusika wa Eazy, Cube na Dre, ndicho kimeandikwa na Kristen katika dissertation (tasnifu) yake yenye jina “Sexual Violence, Black Survivors, and Moving Beyond Resilience.”

N.W.A, baada ya kufanya vizuri sokoni, utawaona wakiangusha house parties za nguvu. Humo ni pombe, wanawake na bangi. Mapenzi kwa makundi. Mastaa watatu katikati ya msitu wa wanawake. Uchafu wa kila aina unafanyika. Huoni thamani ya mwanamke zaidi ya kuwa chombo cha starehe.

Wanawake wote ni Weusi. Hili linafafanuliwa na Kristen katika tasnifu yake chuoni North Carolina, kwamba wanawake weusi kutumikishwa kingono ni mnyororo wa kihistoria tangu zama za utumwa. Kisha, utamaduni maarufu (popular culture), mwanzoni ulitawaliwa na Wazungu kibiashara.

Kutokana na hali hiyo, Wazungu waliwazubaisha mastaa Weusi kwa kuwaandalia parties zenye pombe na wanawake. Fedha zao nyingi zilipotea humo. Ndicho kinachoonekana kwenye muvi “Straight Outta Compton”, na ni moja ya sababu za kusambaratika kwa N.W.A mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Parties hizo za pombe na wanawake Weusi, zinashabihiana na Freak Off Parties za Diddy, vilevile mnyororo wa mastaa Weusi, kukumbwa na kashfa nyingi za kuwanyanyasa kingono wanawake Weusi, hadi ubakaji. Diddy akaunga orodha. Hatimaye yupo nyuma ya nondo.

Mwaka 1993, Rapa Tupac Shakur, alitoa ngoma “Keep Ya Head Up”, ambayo iligeuka wimbo pendwa kwa kila mwanamke Mweusi. Katika single hiyo, Tupac anawashukia vikali wanaume Weusi, tabia yao ya kubaka wanawake. Alipokuwa hai, Tupac alisema, aliandika wimbo kwa sababu vitendo vya ubakaji kwa wanawake Weusi vilikuwa vingi na wabakaji ni wanaume Weusi.

Oktoba 1999, ikiwa ni miaka mitatu tangu kifo cha Tupac, ulitolewa wimbo mwingine wa rapa huyo, unaoitwa “Baby Don’t Cry”, ambao ni sehemu ya pili ya “Keep Ya Head”, akifikisha ujumbe jinsi wanawake Weusi wanavyonyanyaswa kingono kwa kubakwa hovyo na wanaume Weusi.

Sherri, mwasisi wa kundi la Mercedes Ladies, ambalo ni Hip Hop squad ya kwanza ya wanawake Marekani na duniani, kupitia kitabu chake “Mercedes Ladies”, amesimulia k**a hadithi ugumu wa wanawake kwenye tasnia ya burudani.

Kuanzia alivyobakwa na guardian wa Hip Hop, Russell Simmons, hadi vikwazo ambayo yeye na wenzake walipitia kila hatua, wakishurutishwa watoe rushwa za ngono. Mstari wa Solo Thang, “binti kulala kwa prodyuza” au line ya Dataz “binti kupromotiwa kimuziki na kimwili.” Ndiyo hali Mercedes Ladies waliipitia. Sherri amesimulia.

HATIMA YA DIDDY

Diddy, mwana-Hip Hop tajiri ambaye mwishoni mwa miaka ya 1990 hadi katikati ya muongo wa pili wa miaka ya 2000, alitambulika k**a mwanamuziki mwenye fedha nyingi zaidi duniani, kabla ya kupitwa na Jay Z, kisha Kanye West na Rihanna.

New York finest, Diddy, ni mtetezi hasa wa jumuiya ya watu Weusi. Alianzisha slogan ya kukweza mafanikio ya watu Weusi, aliyoiita “Black Excellence”. Zaidi, Diddy, alikuwa kiunganishi cha watu Weusi maarufu na mpatanishi palipo na migogoro. Hata hivyo, hivi sasa ni k**a anaielekea omega!

Diddy, yupo mahabusu kwenye magereza ya MDC (Metropolitan Detention Centre), Brooklyn, New York. Anash*takiwa kwa makosa mengi ya ukatili wa kingono kwa wanawake. Alik**atwa Septemba 16, 2024, Manhattan, New York.

Kabla ya kuk**atwa, Machi 25, 2024, polisi walivamia nyumba za P Diddy zilizopo Los Angeles, California na Miami, Florida. Katika uvamizi huo wa kiupelelezi, polisi walinasa makopo 1,000 ya mafuta ya watoto, vilainishi na dawa za kulevya. Vyote hivyo vinatajwa kuwa vitendea kazi vyake vya ukatili wa kingono.

Diddy, binadamu mwenye ufahari mkubwa wa kimaisha, hivi sasa analala kwenye kichumba kidogo k**a cubbyhole. Kina ukubwa wa futi nane kwa 10. Kitanda ni chuma chenye upana wa meta moja na nusu, halafu godoro halina mto. Akitaka kunyoosha miguu chumbani, atatembea kwa hatua tano tu. Hakuna hata kitabu cha kusoma.

Maisha ya mansions za baharini (waterfront), mahekalu makubwa yenye kila starehe. Massage za kila siku kwenye vyumba maalum, picnics baharini kwa kutumia yachts zake za kifahari, misele kwa ndege zake binafsi, matembezi kwa magari ghali duniani na mavazi ya kikwasi. Vyote hivyo hana uhuru navyo. Kwa sasa, analazimika kupaita MDC nyumbani, akisubiri hatima yake.

Akiwa MDC, Diddy analazimika kuchangia mahabusu na haramia hatari wa dawa za kulevya kutoka Mexico, Ismael Zambada Garcia “El Mayo” na tapeli wa fedha za kidigitali (cryptocurrency), Bankman Fried. MDC pia walishakaa, Rapa Fetty Wap na mfalme wa R&B, R Kelly, ambaye anatumikia kifungo cha miaka 20, baada ya kukutwa na hatia ya kuwatumikisha watoto kingono.

Gereza la MDC, linatajwa kuwa hatari kwa wafungwa na mahabusu. Vurugu za kupigana pamoja vifo hutokea. Juni 2024, msh*takiwa wa kesi ya bunduki, Uriel Whyte, aliuawa kwa kuchomwa kisu. Julai 2024, mfungwa Edwin Cordero, alifariki dunia akipigana. Januari 2019, gereza hilo lilipata hitilafu ya umeme, wafungwa na mahabusu wakakaa gizani na kwenye joto kali kwa wiki nzima.

Ndani ya miaka mitatu iliyopita, watu watatu wamejiua kwenye gereza la MDC. Hali hiyo ndiyo ambayo imekuwa ikisababisha wanasheria wa Diddy, walalamike mteja wao kupelekwa MDC, kwa sababu wanaona usalama wake ni mdogo.

DIDDY ALIVYOSAKWA

Novemba 23, 2023, mwanamuziki Cassie Ventura, alifungua mash*taka Mahak**a ya Wilaya, Manhattan, dhidi ya Diddy, akidai kipindi wakiwa wapenzi mwaka 2007 mpaka 2018, galacha huyo wa Hip Hop, alimfanyia vitendo vingi vya ukatili wa kijinsia. Kesi hiyo, walimalizana nje ya mahak**a.

Siku hiyohiyo (Novemba 23), mwanamke mwingine, Joi Dickerson, alifungua mash*taka kwenye Mahak**a ya Wilaya, Manhattan, akidai Diddy alimleweshwa kwa dawa za kelevya, akambaka, akamrekodi video za ngono na kusambaza.

Desemba 6, 2023, mwanamke aliyetambulika kwa jina la Jane Doe, alifungua mash*taka Mahak**a ya Wilaya, Manhattan, akidai Diddy akishirikiana na wanaume wengine wawili, walimlewesha kwa dawa, kisha wakamsafirisha kutoka Detroit hadi New York, walipombaka ndani ya studio za Bad Boy Entertainment.

Februari 26, 2024, prodyuza Rodney Jones “Lil Rod”, alifungua kesi Mahak**a ya Wilaya ya Kusini, New York, amkimsh*taki Diddy, kumlazimisha kutumia dawa za kulevya pamoja na kufanya mapenzi na wanawake makahaba.

Machi 25, 2024, nyumba za Diddy, zilizopo Los Angeles na Miami, zilivamiwa na maofisa wa Idara ya Usalama wa Ndani, Marekani. Aprili 4, 2024, Grace O’Marcaigh, alifungua kesi Mahak**a ya Kaunti ya Los Angeles, akidai kubakwa kwenye Yacht na mtoto Diddy, Christian Combs “King Combs”.

Grace alidai mahak**ani kuwa Diddy ndiye aliyemsaidia King Combs kumbaka, kisha alimhonga fedha dereva wa Yacht, anyamaze. Mei 23, 2024, mwanamke, April Lampros, alifungua kesi Mahak**a ya Wilaya ya Kusini, New York, akidai kati ya mwaka 1990 na 2000, Diddy alimfanyia mashambulizi mengi ya kingono.

Mei 22, mwanamitindo wa zamani, Crystal McKinney, alifungua madai Mahak**a ya shirikisho, Manhattan, akimtuhumu Diddy kumlewesha kwa dawa za kulevya na kumfanyia shambulizi la ngono, studioni kwake, New York, mwaka 2003.

Juni 2024, Diddy alikutwa na hatia mahak**ani ya kumlewesha kwa dawa za kulevya na kumshambulia kingono, Derrick Smith, 51. Mahak**a iliamuru Diddy amlipe Smith fidia ya dola za Marekani 100 milioni (Sh270 bilioni). Hata hivyo, mawakili wa Diddy wamekata rufaa.

Septemba 11, 2024, mrembo Dawn Richard, alimsh*taki Diddy, Mahak**a ya Wilaya ya Kusini, New York, akimtuhumu kumfanyia mashambulizi ya kingono na kumuumiza kisaikolojia, alipokuwa anashiriki kipindi cha televisheni cha “Making the Band 3”, kilichoanzishwa na Diddy.

PIGO KUU

Diddy mwenyewe na wanasheria wake, walikuwa wakikanusha kila tuhuma, ikiwemo ya Cassie. Mei 18, 2024, Diddy alipigwa bomu zito, unaweza kuliita “coup de grace” – “pigo la kusimamisha moyo”. Video akimpiga na kumburuza Cassie, ziliwekwa mtandaoni.

Video hizo, zilirekodiwa kupitia kamera za usalama (CCTV Camera), zinamwonesha Cassie akiwa amebeba begi akitembea kwa haraka, kisha Diddy anatokea kwenye korido akimkimbiza, alimpofikia, alianza kumpiga kwa ngumi na mateke, kisha akamburuza kumrudisha chumbani. Ni tukio la Machi 2016, Hoteli ya InterContinetal, Los Angeles.

Mei 19, 2024, Diddy alijitokeza kuomba msamaha. Pamoja na hivyo, tukio la kumpiga Cassie, lilionekana kumfikisha pabaya. Wengi walitabiri kuwa iliwadia tamati ya patriarch wa Bad Boy Entertainment. Hatimaye, sasa anaishi kwa kujiminya kwenye cubbyhole yenye nondo nzito, gerezani MDC.

Mlinzi wa zamani wa Diddy, Gene Deal, amesema mara kadhaa kuwa tabia ya boss huyo wa Rivolt TV, kwa kiasi kikubwa imechangiwa na mentors wake wawili, Russell Simmons na marehemu Andre Harrell. Russell, alipoona anasumbuliwa na tuhuma nyingi mashambulizi ya ngono kwa wanawake, alikimbilia Bali, Indonesia, anakoishi.

Machi 2024, Russell alitumiwa hati ya mash*taka dhidi yake kutoka Marekani, ambayo aliipokea akiwa Bali. Russell hajawahi kurejea Marekani kuitikia wito. Hivi sasa, Russell hamiliki mali yoyote Marekani, aliuza akahamia Bali.

Kwamba michezo ya kubaka wanawake na hata kuwageukia wanaume, kwa mujibu wa Deal, Diddy amejifunza kutoka kwa Russell na Harrell, ambaye ni bosi wa zamani wa studio ya muziki ya Uptown Records. Kupitia Uptown, Harrell alimwajiri Diddy na kumkuza kimuziki, kabla ya mogul huyo hajaanzisha label yake, Bad Boy Entertainment.

Kufikishwa mahak**ani kwa Diddy bila shaka ni kilele cha docuseries za In The Dark na Surviving Diddy, bila kuacha mahojiano mfululizo kuhusu Freak Off Parties. Inatafsiri anguko la mbuyu katika biashara ya muziki. Binadamu ambaye amechonga barabara za wengi; Notorious BIG, Craig Mack, Mase, Fabulous, 112, Faith Evans, Total, kutaja wachache.

Kutoka Tupac, Mike Tyson, Bill Cosby hadi R Kelly, na sasa Diddy, kesi nyingi zinatokana hulka ya kuwatumia wanawake Weusi k**a chombo cha burudani. Nao wanawake Weusi wamekuwa wakitumia hilo k**a mtaji, kwa kusingizia wasio na hatia ili kujipatia fedha au kutumika kwa visasi na kupeleka masupastaa Weusi wanaume jela.

Shida kubwa ni lifestyle. Nyota Weusi wengi wana mwanzo wenye zigzaga. Wanapotoboa kimaisha, huingiwa na ulimbukeni. Msemo wa “maskini akipata makalio hulia mbwata”. Ukijumlisha tatizo la kihistoria tangu zama za utumwa, fujo nyingi huelekezwa kwa wanawake, matokeo yake ni mfanano wa anachopitia Diddy.

Ni gharama kubwa ambayo Diddy anailipia hivi sasa. Kusafirisha wanawake na kuwajaza kwenye parties zake za Freak Off. Kuwezesha ngono waziwazi kwa makundi na kurekodi kila tendo. Ni gharama ya mbegu mbaya ya kuwatumia wanawake Weusi k**a watumwa wa ngono.

Ndimi Luqman MALOTO

MUUAJI WA MWAKA MPYA Bingwa wa taharuki HUSSEIN TUWA ametuletea kitabu cha MUUAJI WA MWAKA MPYA, kinachokujumuisha hadit...
26/06/2024

MUUAJI WA MWAKA MPYA

Bingwa wa taharuki HUSSEIN TUWA ametuletea kitabu cha MUUAJI WA MWAKA MPYA, kinachokujumuisha hadithi fupi fupi, zikiongozwa na riwaya ya “Muuaji wa Mwaka Mpya” yenyewe.
K**a u-mpenzi wa riwaya kwa ujumla, basi hupaswi kukikosa kitabu hiki, na k**a wewe ni mpenzi wa hadithi fupi fupi, basi hakika hiki ni kwa ajili yako.
Kitabu kinauzwa shilingi za kitanzania ELFU KUMI NA TANO TU (15,000/-); na kinapatikana kwenye maeneo yafuatayo:

DAR ES SALAAM:

1) Duka la Kona ya Riwaya - Kinondoni Block 41 (0655 428085)

2) Posta Mpya - Kwa George (0755 454152)

3) Elite Bookstore - Tangi Bovu

4) Duka la Kalamu Tulivu (Kwa Molito) - Magomeni Kanisani, mtaa wa Limbeni - (0718 975659)

NJE YA DAR ES SALAAM:

ARUSHA — Chuo cha Makumira: Kwa Mariam (0683 703 275)

MBEYA – Kwa Edna Tibandelana (0754 0910481)

MOROGORO – Kwa Markus Mpangala (0719 226 293)

Kwa mikoa mingine tutaweza kumfikishia msomaji mpaka alipo, kwa kuwasiliana moja kwa moja na duka letu la KONA YA RIWAYA kwa namba iliyotajwa hapo juu (0655 428085).

KITABU: Muuaji wa Mwaka MpyaHadithi: Kivuli Namba 8Mtunzi: Hussein TuwaSIKU MBILI KABLA ya kukutanishwa na madam Warda, ...
23/06/2024

KITABU: Muuaji wa Mwaka Mpya

Hadithi: Kivuli Namba 8

Mtunzi: Hussein Tuwa

SIKU MBILI KABLA ya kukutanishwa na madam Warda, niliitwa ofisini kwa bosi wangu, wakati huo nikifanya kazi kwenye kampuni ya kubeba abiria jijini Dar, iliyokuwa imejipanga kuwatoa akina Uber, Bolt na Faras kwenye gemu.
"Tumepata tenda ya kutoa huduma kwa mteja wa kudumu. Nataka uende huko. Utakuwa dereva wa familia na utaishi hapo hapo nyumbani kwa mteja… najua we' ni msela tu, so hili halitakuwa shida kwako, no?" Bosi aliniuliza huku amenikazia macho yaliyonionya nisithubutu kubishana naye.
"Aaaa-ah, bosiii! Sasa hivyo si nitakuwa nafanya kazi saa nyingi kuliko wenzangu lakini?"
"Na hela pia itakuwa nyingi kuliko wenzako… na kuanzia keshokutwa? Bosi wako atakuwa huyo mteja wetu, si miye tena."
Sikumwelewa.
"Ndo nini? Umenifukuza kazi kijanja, au?"
"No bhana! Bado utaendelea kuwa mwajiriwa wetu lakini maelekezo yote ya kazi, na mshahara wako, utapokea kutoka kwa huyo mteja wetu. Kampuni yetu itakuwa inapata kamisheni tu kutoka kwa mteja."
Ufupi wa maelezo ni kwamba siku mbili baadaye niliwasili kwenye kasri la huyo mteja wetu, bosi wangu mpya.
Nilipoteremka kutoka kwenye gari la kampuni na kubinya kengele ya geti la jumba lake, nilikuwa nimeshajuzwa kuwa bosi wangu mpya alikuwa ni mmoja wa matajiri wakubwa nchini, ambaye nilishawahi kumwoma mara kadhaa kwenye magazeti na mitandao ya kijamii. Pia, nilishabainishiwa kuwa kazi yangu kwenye lile kasri itakuwa ni kumwendesha mke wa huyo bosi wangu mpya.
Bosi wangu mpya, tajiri kijana Malik Sultani, alikuwa amesimama nje ya lango kuu la kasri lake.
"Karibu! Nadhani umeshaelezwa kila kitu kuhusu majukumu yako hapa?" Alinisaili, huku akinipa mkono.
Niliafiki kwa kichwa huku nikitamka kwa ulimi, kuwa nimeshaelezwa majukumu yangu tangu kule ofisini kwetu, ilhali nikiupokea mkono wake.
"Good. Nifuate," aliniambia, akageuka na kuingia ndani. Nikamfuata hadi sebuleni kwake.
“Kutana na mke wangu, Warda. Warda, kutana na Swedi, dereva wetu kuanzia leo. Safari zako zote yeye nd’o atakuwa anakupeleka,” alisema, huku akimwoneshea kila mmoja wetu kwa mwenzake, kwa kutumia mkono wake ambao haukuwa kwenye mfuko wa suruali yake ghali, lakini miye nilikuwa nimepigwa butwaa.
Simu ya bwana Malik ikaita, nikamsikia akiongea na ile simu kana kwamba yupo mbali sana na pale tulipokuwa.
“Er, As’lam Alaykum…”
“Naam?” Niliitika kana kwamba nimeitwa, nikigutushwa kutoka kwenye mduwao wangu na sauti nyororo ya mke wa bosi, niliyekuwa nimebutwaika kwa kumkodolea macho.
Nikajua kuwa kuna kitu nimekosea.
“Eeh, no, I mean… waaleikumsalam… er salam, am yeh, ndiyo!” Nilijifaragua na kubwabwaja huku nikiendelea kumkodolea macho, nikiwa nimetalikiwa umakini wa kauli.
Warda, mke wa bosi mpya, alikuwa ameketi kwenye kiti cha matairi wakaliacho walemavu wa miguu, ilhali kuanzia sehemu ya katikati ya tumbo lake bapa kuja chini ikiwa imefunikwa kwa blanketi zuri na ghali.
Nilimwona vyema kuanzia usoni hadi katikati ya tumbo lake tu, lakini nilichokiona kilitosha kunibutwaisha.
Sura yake, rangi ya ngozi yake, mkato wa kifua chake... ah, hapana. Huyu Warda alikuwa ameumbika jamani!
But on a wheelchair?
Ama kweli…hujafa hujaumbika!
“Vipi, uko sawa?” Bi. Warda aliniuliza kwa upole, huku macho yake yakiniita niende kumkumbatia pale kitini alipoketi.
Nilivurugwa.
“Aam, niko tu… I mean, sawa tu, bibie.”
“Niite Madam, please.” Aliniambia kwa ulimi, ila nilikuwa nina uhakika kabisa kuwa macho yake yaliniambia, “njoo unibusu please.”
Nikajitukana tusi la nguoni kimoyomoyo.
“Okay good. Now that mmeshafahamiana, njoo nikuelekeze zaidi kabla sijatoka, okay?” Bosi Malik aliniambia huku akiirejesha mfukoni simu yake, na akigeuka kurudi kule nje tulikotoka. Nikamfuata kwa ajizi kubwa kabisa, kwani akili na ufahamu wangu vilibaki kwa madam Warda.

***

Bosi Malik alinionesha gari nililopaswa kumwendeshea mke wake. Lilikuwa ni gari ghali, la kisasa na lililotengenezwa mahususi kwa kubeba abiria mwenye kutembelea kiti cha matairi k**a kile cha mkewe.
Sehemu ya kiti cha nyuma ya kile cha dereva palikuwa pana kiti cha kubeba abiria mmoja tu, na ubavuni mwa kiti hicho palikuwa wazi bila ya kiti chochote. Badala yake, palikuwa pana kijidaraja maalum ambacho baada ya kubofya sehemu maalum pale kwenye gari, kinashuka nje taratibu, halafu kile kiti cha matairi kinapandishwa juu yake na kubanwa kwa vishikio maalumu ili kisichezecheze. Kisha, kile kidaraja kinarudishwa taratibu ndani ya gari kikiwa na kile kiti juu yake. Kikiingia ndani ya gari kile kiti cha matairi ndiyo kinakamilisha sehemu ya pili ya kiti cha abiria kwenye ile sehemu ya nyuma.
Tulitumia takriban saa moja na nusu kuelekezana namna mbalimbali za kukitembeza kile kidaraja, tukitumia kiti kingine cha matairi ambacho kilikuwa kitupu na bosi Malik akikikalia badala ya madam Warda.
Nikaelewa somo.
Baada ya hapo, bosi Malik akanitambulisha kwa wafanyakazi wengine walio chini ya himaya yake. Palikuwa pana mpishi, mpigaji pasi na mfuaji (walikuwa wana mashine zao za kufulia pale pale nyumbani), msichana wa kazi ndogongo za usafi wa nyumba, mwangalizi wa bustani kubwa na maridadi sana za maua, ambaye pia ndiye aliyekuwa anasimamia usafi wa bwawa lao la kuogelea.
Kisha, nikaoneshwa kijumba changu kidogo kilichokuwa pembezoni kabisa ndani ya uzio wa jumba lile.
Mzee… ni hatari!
K**a kile ndiyo kingekuwa kijumba cha kupanga, basi bila laki tano kwa mwezi nina hakika mtu asingekipata. Kila kitu ndani, kuanzia bafu na choo, kijisebule kidogo hadi kijivaranda cha kupungia upepo. Pia, kulikuwa na simu maalumu ya kupokelea maelekezo kutoka nyumba kubwa kuhusu safari za madam Warda.
Ndugu yangu! Kuna watu wanajijengea chekechea ya pepo papa hapa duniani aisee, Dah!
Kwa wakati ule k**a ningeambiwa kuwa hata ndani ya pepo huweza kuibuka jahanamu hakika nisingekubali.
Lakini sasa? Mnhu! Hilo nalikubali kabisa.
_________________________

**Haya, kwani alikutwa na nini mpaka hatimaye akafikia kuamini kuwa pepo yaweza kuzaa jahanamu?

Usikose kununua kitabu cha MUUAJI WA MWAKA MPYA kujua zaidi.
MUUAJI WA MWAKA MPYA ni kitabu cha hadithi fupi fupi ikiwemo “Muuaji wa Mwaka Mpya” yenyewe na hii ya “Kivuli namba 8.”
Kitabu kitaingia rasmi sokoni ifikapo Juni 24,2024. Bei yake itakuwa ni shilingi elfu 15. Kwa kujua zaidi, mtwangie Zamira huku 0655 428085.

Si mnajua tena?

KITABU: Muuaji wa Mwaka MpyaHadithi: Mchonga Mwiba – sehemu ya 2Mtunzi: Hussein Issa Tuwa ILIPOISHIA JANA:"Ah, ni nani h...
21/06/2024

KITABU: Muuaji wa Mwaka Mpya
Hadithi: Mchonga Mwiba – sehemu ya 2
Mtunzi: Hussein Issa Tuwa

ILIPOISHIA JANA:
"Ah, ni nani huyu muuaji lakini?" Aliuliza, kwa namna ya kujisemea mwenyewe.
"Mwiba, afande." Mmoja wa wale askari alimjibu, na Alex akamkazia macho.
"Hilo jina nalijua… nilisoma gazetini kuhusu muuaji huyu." Alisema huku bado akionekana kuwa na mawazo, “ni mtu mwenye hilo jina ndiye ninayemuulizia hapa.”

LEO INAENDELEA…
Baada ya yale mauaji ya kwanza kutokea, msemaji wa jeshi la polisi alipokuwa akiongea na wana habari kuhusu mauaji yale, alisema, "... ni mauaji ya kinyama kabisa. Marehemu amechomwa kwa kisu mara nyingi sana, sehemu ya mbele ya mwili wake. Yaani… ni k**a vile ameangukia sehemu yenye miba mirefu, migumu na mikali sana! Huu ni unyama mkubwa, na jeshi la polisi litafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kuwa…"
Kile kipande cha video kilisambaa sana mitandaoni.
Alipouawa Tunu, magazeti yakapata cha kuandika. Moja likaandika kwa maandishi makubwa kabisa, "MWIBA WAUA TENA." Na hapo muuaji yule asiyejulikana akawa amepata jina.
"Okay, so Fatma ilibidi aende maternity baada ya mauaji ya pili?" Aliuliza na kulitazama lile faili lililokuwa mbele yake, "hili faili ni jembamba sana, halinitii moyo kuwa nitapata mengi ya kunisaidia humu."
"Aam, yaa… alilazimika kwenda likizo ya uzazi siku ya pili baada ya mauaji ya pili… nd’o akamshauri bosi akwite wewe uje uuendeleze upelelezi huu, afande."
"Oh, that's great, Fatma. That's just great!" Panasha alimlalamikia Inspekta Fatma kwa kumbebesha kesi ile tata.
"Sio kwamba alipenda, chifu… ujauzito wake ulikuwa una matatizo sana. Daktari alimshauri akae mbali kabisa na kazi… akawekwa bed rest."
Panasha hakuzingatia hayo maelezo, kichwa chake kilikuwa kinachemka.
"Mnadhani ni kwa nini Mwiba anawaua hawa warembo?" Aliuliza huku akiwa amekunja uso.
"Aam, kwa mujibu wa Fatma baada ya kile kifo cha kwanza, alisema mtindo wake wa uuaji unaashiria wivu wa kimapenzi. Alisema huenda marehemu aliuawa na mpenzi wake."
Panasha alimtazama Konstebo Happiness.
"Crime of passion?" Alisema kwa kuuliza.
"Ye, yes… ndivyo ilivyoonekana pale mwanzo."
"Mlimpata mpenzi wake?"
"Ndiyo afande, lakini tulijiridhisha kuwa hakuhusika. Alikuwa nje ya nchi wakati huo na alirudi nchini baada ya kupata taarifa hizi…" Mmoja wa wale askari alijibu.
"Lakini… baada ya mauaji ya pili kutokea, hata Fatma alibadili mawazo juu ya sababu za haya mauaji.” Happiness alisema.
"Of course! Isingewezekana wote wawili… watatu, wawe wapenzi wa mtu huyo huyo mmoja na wote awauwe kwa wivu wa kimapenzi…" Panasha aliunga mkono.
"Kwa hiyo we' rai yako ni nini, afande?" Mmoja wa wale askari alimuuliza.
"Achana na rai zangu kwa sasa… nataka nijue mjuacho nyie niliowakuta kwenye hii kesi kwanza," Panasha alimjibu, "na vipi kuhusu sababu ya vifo vyao? Mnadhani ni nini kilichoondoa uhai wao?"
Wale wenzake waliguna kwa mshangao.
"Si kuchomwa visu afande!" Konstebo Happiness na mwenzake mmoja walimjibu, japo maneno waliyotumia yalikuwa tofauti, ujumbe wao ulikuwa huohuo.
Panasha akaguna.
"Fatma aliwaambiaje?"
"Yeye hatukufika naye huko. Ila nadhani kwenye hilo faili kutakuwa kuna majibu ya hilo…?" Happiness alimjibu, sauti yake ikidhihirisha kukosa imani na Panasha kwa lile swali la nini ilikuwa sababu ya vifo vya wale marehemu, ambalo kwa mtazamo wake, lilikuwa ni la kijinga.
Kimya kifupi kikachukua nafasi. Kisha Panasha akaagiza picha za marehemu wote watatu ziwekwe pale ukutani.
"Ni kweli hawa marehemu wamechomwachomwa visu, lakini hawakuuawa kwa visu." Alisema huku akizitazama zile picha.
Wenzake wakamtumbulia macho ya mishangao.
"Ah, kivip—"
"Unaona majeraha ya kujikinga kwenye maiti yoyote kati ya hizo, hapo?" Panasha alihoji huku akiuoneshea kwa kichwa, ule ukuta wenye picha za marehemu.
"Majeraha ya kujik– Ah, ila kweli aisee!" Happiness alisema.
"Unanielewa sasa, eenh?" Alex alimwambia, "k**a wangekuwa wameuawa kwa visu, lazima wangeinua mikono kujikinga!"
"Na kwa maana hiyo, wangekuwa wana majeraha ya visu mikononi pia!" Askari mwingine akadakia.
"There you go!" Panasha akamuunga mkono kwa Kimombo.
Wale askari sasa wakaanza kumtazama kwa heshima mpya.
"Ah, ina maana aliwachoma visu baada ya, ya kuwa… wameshakufa?" Happiness alisema kwa kuchanganyikiwa. Panasha hakuona haja ya kumjibu.
"Wamekufaje sasa?" Mwingine akahoji.
"Naweza kuweka dau kuwa aliwaua kwa kuwakaba au kuwabana pumzi kwanza, kisha nd’o akaidungadunga miili yao kwa visu." Panasha akasema.
"Eh, Mungu wangu!" Happiness aliguna, “hii kesi ya ajabu kwa kweli. Sasa, kwa nini muuaji afanye hivyo?”
“Inabidi tumk**ate, tumuulize.” Panasha akamjibu bila kutilia maanani, akili yake ikiwa inachemka kwa kiwango cha mtokoto.
Kimya kingine kikatamalaki.
“Jamaa atakuwa kichaa basi! Atakuwa ana wazimu unaomsukuma kuwaua warembo na kuwachomachoma visu huyo.” Mmoja wa wale askari alisema.
“Hapo utakuwa unaotea tu. Njia ya kuyajua majibu ya hilo ni kumk**ata tu.” Panasha alimwambia.
“Tunasubiri maelekezo yako tu, afande.” Yule jamaa alimjibu. Panasha akamkata jicho lililojaribu kuupenya ubongo wake.
“Okay, kuna nini kingine ninachopaswa kujua, ili sote tuwe na welewa sawa kwenye hii kesi kabla hatujaendelea?” Aliuliza.
Wale askari walitazamana, kisha Konstebo Happiness akakohoa kidogo, “Aam, labda ni kuhusu Mchonga Mwiba tu, afande. Ukiondoa hilo hatuna tulijualo zaidi.”
Panasha akamkazia macho.
“Mchonga Mwiba?”
Wale skari walitazamana tena.
“Er, ndiyo afande.”
“Mwiba nao unachongwa?” Panasha alishangaa.
“Er, ndiyo hapo sasa, afande!” Mjibuji alimzidishia mshangao.
“Fafanua, Konstebo!” Panasha alimkoromea.
Ndipo kwa mara ya kwanza, Inspekta Alex Panasha aliposikia habari za Mchonga Mwiba.

***
Alijuzwa kuwa baada ya mauaji ya pili kutokea, aliibuka mtu kwenye mitandao ya kijamii aliyejiita ‘Mchonga Mwiba’. Huyu alianza kuandika makala za kumlaani muuaji aliyepachikwa jina la Mwiba. Maandiko yake yalikuwa yakimsimanga muuaji kuwa ni mwoga na mgonjwa anayehitaji tiba. Na tiba yake anayo yeye, Mchonga Mwiba.
“Seriously?” Panasha alihoji.
“Kabisa afande!” Alijibiwa, huku zile picha za wale marehemu zikitoweka pale ukutani.
“Sasa kwa nini bado hajak**atwa tu mpaka sasa?”
Muda huo ukaonekana ukurasa wa Facebook wa mtu anayejiita Mchonga Mwiba pale ukutani. Panasha akaukodolea macho. Aliitazama profile picture ya mtumiaji huyo. Ilikuwa ni picha ya kichongeo cha penseli katikati ya miiba mingi.
“Hatujui alipo, afande! Si unajua hilo ni jina tu la kwenye mitandao ya kijamii?”
“Yaaaa, na… looks like aliifungua hii akaunti mahsusi kwa ajili ya kumsimanga huyo muuaji.” Panasha alijisemea mwenyewe, huku akianza kusoma baadhi ya mijadala iliyokuwa ikiendelea mtandaoni, kwenye ule ukurasa wa Facebook wa ‘Mchonga Mwiba’.
“Hii unayoona hapa ni mpaka pale yalipotangazwa mauaji ya pili. Ikitangazwa kuwa Mwiba kaua kwa mara ya tatu, jamii ya Facebook itacharushwa upya na huyu mtumiaji.”
Na ilionekana kuwa kweli. Panasha aliona jinsi maoni ya wafuatiliaji yalivyokuwa yameujaza ukurasa wa Mchonga Mwiba pale Facebook.
Wapo waliokuwa wakimkanya kuwa anajihatarisha. Wapo waliokuwa wakimpongeza na kumuunga mkono. Wapo waliokuwa wakimtukana kuwa anatafuta umaarufu kwenye vifo vya watu wasio na hatia.
Na wapo waliomwambia kuwa na yeye atatumbuliwa tu na Mwiba siku moja.
Majibu ya Mchonga Mwiba yalikuwa makavu na mafupi.
Anatamani muuaji amfuate na yeye basi k**a kweli yeye ni mwiba.
Anamwambia muuaji kuwa mwiba wake ni butu, ndio maana anawaua wanawake wanyonge wasio na uwezo wa kujitetea. Ila yeye ndiye mwenye kichongeo cha mwiba huo. Akitaka kuwa muuaji wa kutisha, basi awaue wenye uwezo wa kujitetea, na hawezi kuliweza hilo bila kumfuata yeye ili amchonge awe mwiba mkali.
Jamii haikumwelewa Mchonga Mwiba. Polisi pia hawakumwelewa.
“Hebu nielezeeni zaidi kuhusu huyu Mchonga Mwiba.” Panasha alisema huku bado akiutazama ule ukurasa wa Facebook, wa Mchonga Mwiba.
Yule mtaalamu wa TEHAMA akamweleza.
__________________
**Unadhani alielezwa nini kuhusu Mchonga Mwiba?
Usikose kununua kitabu cha MUUAJI WA MWAKA MPYA kujua zaidi.

***MUUAJI WA MWAKA MPYA ni kitabu cha hadithi fupi fupi ikiwemo “Muuaji wa Mwaka Mpya” yenyewe na hii ya “Mchonga Mwiba.” Kitabu kitaingia rasmi sokoni ifikapo Juni 24,2024. Bei yake itakuwa ni shilingi elfu 15.

Si mnajua tena?


20/06/2024

Kitabu: Muuaji wa Mwaka Mpya.

Hadithi: Mchonga Mwiba.

Ghadhabu za muuaji zilitapakaa chumba kizima.
Samani zilikuwa zimetupwa huku na huko. Baadhi ya vyombo na vipodozi vilikuwa vimetawanyika shaghalabaghala, sakafuni. Damu ilikuwa imetapakaa ukutani, sakafuni, kwenye mashuka ya kitanda, kwenye kitanda chenyewe… na mwilini kwa mwenye damu ile.
Inspekta Alex Panasha alikuwa akiukodolea macho mwili uliolala chali pale kitandani, baada ya kuwa ameshatazama mazingira yote ya chumba kile ghali.
Marehemu alikuwa uchi wa kuzaliwa, isipokuwa ile sehemu ya makutano ya miguu yake miwili, ambayo ilikuwa imefunikwa kwa pembe ya shuka iliyokuwa imejivuruga pale kitandani, nayo ikiwa imelowa damu.
Ni k**a vile ile shuka iliufunika ule utupu wa marehemu kwa sadfa tu, bila kukusudiwa iwe hivyo… au labda, muuaji aliamua kumsitiri mhanga wake k**a wazo la mwisho tu kabla hajaondoka eneo lile.
Panasha akaguna.
Akazidisha umakini wake kwa yule marehemu.
Alikuwa amechomwa mara nyingi sana kwa kisu, eneo lote la kifuani na tumboni. Kisu kilichotumika, kilikuwa kimelala kando ya mwili wake pale kitandani, kikiwa kimetapakaa damu.
Hakuweza kuuona uso wake.
Akamung'unya mdomo wake wa chini huku akitazama kilichomfanya ashindwe kuuona uso wa marehemu.
Fremu kubwa ya picha, ambayo kimsingi ingepaswa iwe imening'inizwa ukutani, au iwe imesimamishwa juu ya meza au shubaka la vitabu au la vitu vya urembo sebuleni, ilikuwa imeufunika uso wa marehemu.
Mguno mwingine hafifu ukamtoka.
Kutokea pale alipokuwa, aliiona sehemu ya nyuma ya ile fremu, na sio ile ambayo ingeweza kuonesha picha iliyohifadhiwa kwenye fremu ile.
"Konstebo!" Aliita kwa sauti.
"Afande!" Sauti ya kiaskari ilimwitika kutokea nje ya chumba kile.
Konstebo Happiness alijitokeza na kusimama nje ya chumba kile, kizingitini. Hakuingia ndani. Hali ya mule ndani ilishamvuruga kichwa na matumbo hapo awali. Hakutaka kuirudia tena hali ile. Alikwepesha macho yake kutoka pale kitandani.
"Una uhakika wapiga picha wetu wamechukua picha zote za eneo hili?" Panasha alimuuliza bila kujali hali iliyosababisha amkute nje ya kile chumba yule askari wa k**e, mara alipofika eneo lile.
"Ndiyo afande… na hawakubadili chochote… hivyo hivyo nd’o tulivyoikuta hali ya humu ndani."
"Waite!"
Wapiga picha za maeneo ya jinai wa jeshi la polisi, ambao bado walikuwepo eneo la tukio, walifika. Wote wawili. Wakasimama palepale kizingitini.
"Mlipata picha ya huyu mteja bila hii fremu hapa usoni?" Panasha aliwauliza.
"No, tulipiga picha eneo la jinai k**a tulivyolikuta, afande. Hatukulibadili eneo kwa kuiondoa hiyo frem—”
“Ah, sasa mliwezaje kumtambua kuwa nd’o huyooo… huyo…” Alijaribu kulikumbuka jina la yule marehemu.
“Rebeka Mwita?”
“Yes, Rebeka – mliwezaje kumtambua bila kumwona sura?”
“Ah, dada anayekujaga kumfanyia usafi ametutajia jina lake.” Mmoja alijibu.
“Na hata tungemwona sura bado tusingeweza kujua jina lake bila kuchukua hatua zaidi za kupata utambulisho wake baadaye.” Mwingine akaongezea.
“Okay. Fair enough. Sasa nataka apigwe picha tena!" Alisema, kisha, kwa mkono wake wenye glovu, aliiondoa ile fremu kutoka usoni kwa marehemu na kuilaza vilevile ikiwa uso chini, kando ya ule mwili.
Mpiga picha aliupiga picha kadhaa ule mwili uliolala chali, huku ile fremu ikiwa kando yake.
"Subiri…" Panasha aliamuru, kisha akaigeuza ile fremu kiasi ile sehemu iliyopaswa iwe imewekwa picha, ikawa inatazama juu. Ilikuwa ni picha ya marehemu wao, akiwa kwenye joho na kofia ya kuhitimu chuo kikuu, tabasamu pana la furaha pichani, likikinzana na mkenuo wa uchungu uliomganda marehemu yule, usoni.
"Okay, endelea sasa…" Aliamuru, na yule mpiga picha akafanya kazi yake.
"Unaweza kwenda," Panasha alisema, na mpiga picha alipokuwa anaelekea nje ya chumba kile, akamtupia kauli, "hizo picha nazihitaji haraka sana!"
"Ndiyo afande!"

***

Wakiwa ofisini kwao, Kituo Kikuu cha Polisi, Alex aliwatazama wale maafisa wasaidizi waliokuwa wakifuatilia kesi ile ya mauaji ya mtungo, kabla yake.
"Kwa hiyo mnaniambia kuwa Inspekta Fatma… yuko martenity?" Aliuliza kwa kutoamini.
"Ndiyo afande… yuko kwenye likizo ya uzazi wiki ya pili sasa." Mmoja wao alimjibu. Alex alipiga mbinja ya mastaajabu huku akitikisa kichwa.
“Huu si utakuwa ujauzito wake wa pili, huu?”
“Yes Sir!”
“Na watu tuliamini kuwa hana kizazi!” Alex alisema, “ni shababi gani huyo aliyemdunga mimba jamani? N'na hamu ya kumwona!" Aliendelea huku tabasamu chokonozi likitekenya mdomo wake.
Wenzake wakacheka.
"Hakuna ajuaye… na hakuna aliyefanikiwa kujibiwa alipomuuliza swali hilo." Konstebo Happiness alimjibu huku akitabasamu.
Alex Panasha akacheka.
"Aah, mi' atanijibu tu. Sio kwa kunilazimisha nikatishe likizo yangu kuja kushika kesi yake hapa!" Alisema, kisha hapohapo uso wake ukarejesha umakini.
"Turudi kwenye kesi yetu sasa," alisema, kisha akashusha macho kwenye faili lililolala wazi mbele yake pale mezani. Halafu, akapeleka macho kwenye ukuta uliokuwa moja kwa moja mbele yake.
Kwenye ukuta ule, palikuwa pameshushwa pazia maalumu la plastiki nyeupe, lenye ukubwa wa k**a futi sita kwa sita hivi. Askari mmoja akazima baadhi ya taa za mle ndani. Kukawa na mwanga hafifu.
Kisha afisa wa masuala ya TEHAMA, akatumia rimoti kuwasha kitupa taswira, yaani overhead projector, na mara hiyo pale kwenye ile pazia ikatokea picha ya mwanamke wa umri wa mwanzo wa ujana akiwa ameuawa.
Sehemu ni tofauti.
Namna alivyolala ni tofauti.
Pahala alipolala ni tofauti.
Yeye alikuwa amelala sakafuni, na kulilowesha kwa damu zulia ghali lenye manyoya mazito lililokuwa pale sakafuni.
Ila aina ya kifo ni k**a ile ambayo Inspekta Panasha ametoka kuishuhudia kwa macho yake, kiasi cha saa moja na nusu tu iliyopita.
Alikuwa amechomwachomwa kwa kisu mara nyingi mwilini.
"Eee, huyu ni Getrude Katala…” Konstebo Happiness alisema, “aliuawa nyumbani kwake mwezi mmoja uliopita, maeneo ya Six, kule Goba."
Panasha aliitazama kwa muda ile picha.
Hayati Getrude alikuwa ametumbua macho kwa mshangao mkubwa kabisa. Kisu kilichotumika kumuua kilikuwa kando yake pale chini. Hata kutokea pale alipokuwa, Alex aliweza kuona kuwa kilikuwa ni kisu tofauti na kile alichotoka kukiona saa moja na nusu iliyopita, kwenye yale mauaji ya kule Masaki.
Aliinuka na kuusogelea ukuta, akaitazama ile picha kwa makini, akiwa kimya. Kisha akarudi kitini na kumwashiria yule mtaalamu wa TEHAMA aendelee.
Picha nyingine mbaya ikajaa pale ukutani.
"Eeyyy!" Panasha alimaka.
"Er, huyu ni Tunu Njaidi. Ye' aliuawa wiki mbili tu zilizopita…" Konstebo Happiness alisema.
Inspekta Panasha alijikuta akijisogeza mbele pale kitini ili aione vyema ile picha.
K**a muuaji alikuwa anaua kwa ghadhabu, basi kwa Tunu ndipo ghadhabu zake zilikuwa zimepindukia kiwango. Zaidi ya kuchomwachomwa kwa kisu sehemu ya mbele ya mwili wake, Tunu alikuwa amechanwachanwa tumbo vibaya.
Macho ya Tunu yalikuwa yamemtumbuka. Ulimi uliovimba ulikuwa umetokeza nje ya kinywa chake, mchirizi mwembamba wa damu ulionekana kugandia kutoka kwenye moja ya tundu za pua yake.
Panasha alianza kuinuka.
"Naweza kuizum tu hiyo picha, afande." Mtaalamu wa kitengo cha kompyuta alimwambia, akiotea vyema kuwa Alex alikuwa anataka kwenda kuisogelea ile picha pale ukutani.
"Oh, okay… do that please."
Muda huo ile picha ikakuzwa pale ukutani. Inspekta Alex Panasha aliitazama kwa udadisi mkubwa, huku akimwelekeza yule mtaalamu akuze maeneo kadhaa ya mwili ule ili ayaone vyema.
"Okay… so, baada ya Tunu pale," alisema huku akimwoneshea yule marehemu wa ukutani, "ndiyo akaja mteja wetu wa leo?" Aliuliza hatimaye.
"Ndiyo afande." Konstebo Happiness alijibu huku akimwashiria yule mwenzake mwenye rimoti, na picha ya yule marehemu waliyetoka kumshuhudia muda mfupi uliopita, ikajianika tena pale ukutani.
"Ah, hiyo nimeshaiona live, itoe tu kwa sasa." Panasha alisema. Picha ikayeyuka kutoka pale ukutani, projekta ikazimwa. Taa za kawaida zikawashwa tena mle ndani.
Panasha akawatazama wale askari wenzake.
"Ah, ni nani huyu muuaji lakini?" Aliuliza, kwa namna ya kujisemea mwenyewe.
"Mwiba, afande." Mmoja wa wale askari alimjibu, na Alex akamkazia macho.
"Hilo jina nalijua… nilisoma gazetini kuhusu muuaji huyu." Alisema huku bado akionekana kuwa na mawazo, “ni mtu mwenye hilo jina ndiye ninayemuulizia hapa.”

____________________________________

Naam, hivi ndivyo “Mchonga Mwiba” inavyoanza. Je Inspekta Alex Panasha (msome kwenye riwaya ya TUZO) ataweza kumdhibiti Mwiba?

Ni ndani ya kitabu cha “MUUAJI WA MWAKA MPYA” ndimo utakutana na kisa hiki kwa ukamilifu wake...
Mtunzi ni Hussein Tuwa

Address

Ilala Boma
Dar Es Salaam
DARESSALAAM

Website

Alerts

Be the first to know and let us send you an email when Fanani na Hadhira posts news and promotions. Your email address will not be used for any other purpose, and you can unsubscribe at any time.

Contact The Business

Send a message to Fanani na Hadhira:

Share

Category