17/05/2021
Tuanze siku kwa kuziombea Familia zetu.
SALA YA KUOMBEA FAMILIA.
Ewe Mungu Mwenyezi wa milele, sisi k**a familia tunakushukuru kwa zawadi ya Mama Kanisa Katoliki ambaye siku zote hutupatia malezi bora kwa ajili ya wokovu wetu. Kanisa halichoki kutuhimiza tutafakari na kuishi utakatifu wa familia ya Nazareti ya Yesu, Maria na Yosefu.
Familia hii iliishi upendo uliojengwa kwa fadhila
za imani, uaminifu, utii, uvumilivu na upole hata
wakawa watakatifu. Tunaziweka mbele yetu familia ya Nazareti iwe dira, baraka na mfano kwa familia zetu. Tunakushukuru Baba kwa ajili ya familia zote zinazojitahidi kuishi fadhila hizo za Familia takatifu na tunakuomba uzidi kuwaimarisha wanandoa ili tupate kwao mifano mingi na bora ya kuigwa.
Ee Bwana, tunaomba Roho Mtakatifu
atuangazie tuweze: kutambua familia kuwa
Kanisa la nyumbani na shule ya imani na
upendo; kuimarisha familia kwa sala, sakramenti na tunu za kiinjili na kushirikiana kwa heshima katika familia kwa usitawi wa roho na wa mwili kwa wanafamilia wote.
Tunaziombea familia zetu na Jumuiya Ndogondogo za Kikristo ziwe bustani bora na salama za kuchipusha na kulea miito mitakatifu ya Ndoa, Utawa na Upadre.
Tunawaombea vijana na watoto wetu Uchaji wa
Mungu ili wawe na bidii ya kujitunza kwa
kushika amri za Mungu na kuishi fadhila za
kiinjili, wawe na roho ya kimisionari yaani
walipende Kanisa na kuwa na moyo wa kueneza
ufalme wako kwa matendo ya imani.
Baba wa huruma, tunakukabidhi familia zenye
misukosuko ya mafarakano, ulevi, ubinafsi,
uregevu-dini, uvivu, ushirikina, hofu, magonjwa
sugu na mengineyo yenye kuleta huzuni; kwa
hisani yako uwape neema, mwanga na nguvu za kuanza maisha mapya yenye amani, waweze
kufurahia upatanisho na uponyi wa pendo lako la kibaba kati yao.
Tunaomba toba na msamaha kwa ukatili, manyanyaso na hata mauaji katika familia zetu na uwaponye wote waliojeruhiwa kwa maneno, matendo na makwazo ya aina yeyote. Aidha tunakuomba uwe kitulizo na faraja kwa wagonjwa na wazee, pia tegemeo la yatima na wajane. Wenye matatizo ya kiafya au ya kijamii wasikate tamaa bali waunganishe hali zao na msalaba wa Mwanao na kukutumaini wewe Mweza yote. Jamii iwajibike nao kwa kuzijali haki zao na kuwapa misaada wanayohitaji.
Tunakuomba ubariki miradi na kazi zetu ili familia zipate usitawi na maendeleo; na utujalie hekima ya kukushukuru kwa maisha ya haki, amani na ukarimu na mwisho tukaimbe sifa zako pamoja na familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu na jeshi lote la mbinguni.
Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu, Amina.
Baba yetu…
Salamu Maria….
Atukuzwe Baba…