09/10/2025
WAZIRI MAVUNDE AZINDUA UJENZI WA MGODI WA KINYWE (GRAPHITE) MAHENGE — MRADI WA DOLA MILIONI 510 KUCHOCHEA UCHUMI NA AJIRA
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Peter Mavunde (MB), amezindua rasmi ujenzi wa mgodi mkubwa wa madini ya Kinywe (Graphite) katika eneo la Mahenge, Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro, unaotekelezwa na kampuni ya Faru Graphite Corporation, ubia kati ya Serikali ya Tanzania (hisa 16%) na Black Rock Mining Limited (hisa 84%).
Uzinduzi huo unaashiria hatua muhimu katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ya sekta ya madini, ikiwa ni sehemu ya maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuharakisha uwekezaji wa kimkakati utakaoinua uchumi wa nchi.
“Mradi huu si uchimbaji wa rasilimali pekee, bali ni injini ya maendeleo itakayochochea ukuaji wa viwanda, biashara, ajira na ustawi wa jamii kwa ujumla,” alisema Waziri Mavunde wakati akizindua ujenzi huo.
Kwa mujibu wa Mhe. Mavunde, mradi wa Mahenge Graphite utagharimu takribani dola za Marekani milioni 510 (sawa na takribani shilingi trilioni 1.3) na unatarajiwa kutoa ajira za muda 400 wakati wa ujenzi na ajira za kudumu zaidi ya 900 mgodi utakapoanza uzalishaji kamili.
Zaidi ya hapo, ajira zisizo za moja kwa moja 4,500 zinatarajiwa kuibuka kupitia mnyororo wa thamani wa wachuuzi, wasambazaji, wakulima na watoa huduma.
Serikali inatarajia kuvuna zaidi ya dola bilioni 3.2 (takribani shilingi trilioni 7) katika kipindi chote cha uhai wa mgodi, kupitia kodi, tozo, mrabaha na gawio la hisa za Serikali.
Akifafanua zaidi, Waziri Mavunde alisema madini ya Graphite ni muhimu katika utengenezaji wa betri za magari ya umeme, vifaa vya kielektroniki na paneli za nishati ya jua, hivyo Tanzania inajiweka kwenye ramani ya dunia k**a kitovu cha malighafi za teknolojia safi (green technology)