16/06/2024
Tatizo la wanandoa kushindwa kupeana tendo la ndoa limetajwa kuleta madhara kazini kutokana na wafanyakazi wengi kwenda kazini wakiwa na hasira na chuki zinazotokana na kutoridhishwa kimwili.
Mkuu wa dawati la jinsia mkoani Iringa, Elizabeth Swai amesema migogoro mingi inayotokea maeneo ya kazi inatokana na wanandoa kutotimiza wajibu wao wa kupeana tendo la ndoa.
Swai ameyasema hayo leo Jumapili Juni 16, 2024 mjini Iringa alipokuwa akifungua semina kwa watumishi na wanafunzi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa.
Amesema tatizo hilo linawakumba hasa wanawake na huwafanya wengi wao kwenda kazini wakiwa na chuki inayotokana na kutotimiziwa haja ya tendo la ndoa.
"Mtu asipotimiziwa kwa kutokupewa inaleta madhara hata kazini hasa wanawake wanakuwa na hasira sana," amesema Swai.
Aidha, ametoa rai kwa wanandoa wajitahidi kuwajibika katika kupeana tendo la ndoa kwa sababu linapunguza kwa kiwango kikubwa migogoro ndani ya ndoa inayochangia matukio ya kujeruhiana na hata vifo.
Amesema kwa mwanaume akiwa na uhitaji na mwanamke akimnyima tendo la ndoa akili huwa zinaruka, hali inayosababisha achukue sheria mkononi kwa kufanya vitendo vya ukatili kwa mwenza wake.
"Mjitahidi sana kuwajibika kwa kupeana, msinyimane, kwa sababu linapunguza sana migogoro ndani ya ndoa. Mwanaume akiwa na uhitaji wa mwanamke halafu umnyime, akili huwa zinawaruka na kujikuta wanafanya ukatili,β