02/01/2026
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imeendesha mafunzo maalum kwa watendaji wa vituo vya kupiga kura kuelekea uchaguzi mdogo wa udiwani wa Kata ya Kirua Vunjo Magharibi, Wilaya ya Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro. Mafunzo hayo yamewahusisha wasimamizi wa vituo, makarani pamoja na wasaidizi wa uchaguzi, yakilenga kuwajengea uwezo wa kusimamia zoezi la upigaji kura kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Afisa Uchaguzi wa Jimbo la Vunjo, Lucas Msele, amesema mafunzo hayo ni muhimu katika kuhakikisha uchaguzi mdogo unafanyika kwa haki, uwazi na kwa kuzingatia misingi ya kisheria.
Washiriki wameeleza kufaidika na mafunzo waliyopata, hususan katika matumizi ya vifaa vya uchaguzi, utunzaji wa siri ya kura na taratibu za siku ya uchaguzi, huku uchaguzi mdogo wa udiwani wa Kata ya Kirua Vunjo Magharibi ukitarajiwa kufanyika tarehe 5 Januari 2026.