09/06/2024
Nukuu muhimu; Mpendwa msomaji tunapenda kukujulisha kwamba licha ya kwamba simulizi hili linahusu kisa cha kweli, majina ya watu au sehemu zinazotajwa katika hadithi hii hayahusiki wala kumlenga mtu au sehemu yoyote ambayo Kwa njia moja au nyingine huenda ikashabihiana na hadithi hii...
Wahenga walisema 'kua uyaone' ya dunia ya M***a...lakini pia unaambiwa ukistaajabu ya M***a utaona ya filauni. Sijui k**a wewe msomaji wa makala hii umeyaona yapi? Lakini pengine dunia sio mbaya ila hawa viumbe waishio ndani ya dunia ndo wabaya.
Kutokana na hulka na matendo au mwenendo wa binadamu katika dunia ndo maana kuna watu na viatu. Aidha ndo maana tunaimbiana mashairi yenye vina na mishororo yenye vijembe na mafumbo ili mradi kila mmoja alivyotendwa na hawa viumbe wa Adamu. Siku hizi hata nyimbo za Dini hazitungwi tu Kwa kusambaza ujumbe wa wokovu wa Kristo, ila pia zimesheheni maneno ya kwenye khanga maadamu 'fumbo mfumbie mjinga, mwelevu keshang'amua'. Utasikia..'mashimo waliyonichimbia wameangukamo wenyewe..' ' Mitego waliyonitegea inewanasa wenyewe' ama 'walidhani nitaanguka sasa wanashangaa' hawa wanaoimbwa ni kina nani?
Simulizi letu linamhusu dada mmoja kwa jina Sonita, ambaye Kwa ridhaa yake ameona vema kufunguka ya moyoni kwenye jukwaa la fikira pevu kuhusiana na changamoto lukuki ambazo amezipitia katika Maisha yake.
Dada Sonita ni yatima aliyelelewa na mama wa kambo akiwa na ndugu zake wengine wawili. Mama yao, Bi chao alifariki pindi akimzaa yeye kisha ilibidi bibi yao, Malkia Nyembe, k**a alivyofahamika kuwatwaa na kuwalea. Baada ya muda k**a miaka miwili hivi bibi yao pia alifariki kwa ugonjwa wa pumu. Hapo baba yao Mzee Sizimwe hakuwa na budi ila kuoa mke mwingine. Hivyo sonita na nduguze walilelewa na mama yao wa kambo.
Familia ya mzee Sizimwe haikuwa yenye maisha ya juu katika kujikimu kimaisha, baada ya kustaafishwa kutoka shirika la posta na simu mzee Sizimwe alijishughulisha na kilimo cha mazao ya biashara hasa yaliyokua na kukomaa kwa muda mfupi, k**a vile vitunguu, nyanya, biringanya, bamia, karoti n.k Alikuwa na ustadi wa kukadiria muda mwafaka wa kusia mbegu na kisha kuhamisha miche ili kuendana na musimu wa mvua za Vuli. Sonita na nduguze hawakuwa na amani siku za upanzi kwani walimjua vema baba yao ambaye hakuwa na simile mtu hata angediriki kuwazuia wasiende shule ilimradi wakapande miche shambani. Kazi ya upanzi ilianza macheo hadi machweo na walipotoka shamba walikuwa hoi kutokana na uchovu.Kutokana na umahiri wake aliweza kulima misimu miwili wa mwaka. Kipindi cha uvunaji wafanya biashara toka marikiti walipanga foleni nyumbani kwake kulangua mazao ya biashara na kazi hii ilimpatia umaarufu mkubwa. Wakati alitembelewa na maafisa ugani ambao baada ya kuona alivyokuwa na bidii ya mchwa, walizitenga bustani zake kuwa kituo cha mafunzo ya wakulima wadogo na walimshauri kujiunga na chama cha ustawi wa wakulima wa ugani ambapo baada ya muda mfupi alianza kupokea mikopo ya pembejeo na zana zingine za kilimo.
Jembe halimtupi mkulima, Mzee Sizimwe hakuwa yule wa mwanzo, baada ya alipata mtaji na kufungua duka la jumla bondeni karibu na eneo la gulioni. Hakuwa na ugumu wa kuwasomesha wanaye alioachiwa na marehemu mkewe Bi Chao.
Sijui kwa nini wahenga walisema kwamba mama wa kambo si mama, bila shaka wangelisema mama wa kambo pia ni mama...mama wa kambo wote wangejua kuthamini utu wa watoto wa kufikia ambao huja kuwalea kwa waume zao. Bi Nanje k**a alivyoitwa mama mdogo wao Sonita hakuwa na matatizo makubwa dhidi yao katika mambo k**a lishe au mavazi, lakini alikuwa na shida moja kubwa... hakupenda wasome. Aidha hakujali hali zao kiafya pale walipougua au kuhitaji matibabu na mara nyingi alisema wanajiuguza kukwepa kazi za nyumbani. Licha ya hayo yote alitokea kumchukia sana Sonita baada ya kugundua kwamba alipendwa zaidi na babake...tufatilie zaidi ili upate uhondo wa stori hii unaponiga...