07/11/2024
Taasisi ya Wakaguzi wa Mizani na Vipimo yaani Masoroveya nchini Kenya(ISK) imetangaza kwamba itawashughulikia vilivyo matapeli wanaojifanya kuwa ni masoroveya kwa kuwalaghai Wakenya huku wakiathiri pakubwa sekta ya ardhi nchini humo.
Rais wa Taasisi hiyo ya Masoroveya nchini Kenya(ISK) Eric Nyadimo alisema kwamba taasisi ya ISK inashirikiana na wadau mbalimbali katika jitihada za kutokomeza kabisa shughuli za masoroveya bandia nchini humo.
Rais Nyadimo alitoa kauli hiyo wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Tisa la Kimataifa linalokutanisha Wakaguzi wa Mizani na Vipimo yaani Masoroveya kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika, lililoanza siku ya Alhamisi ya Novemba 7, 2024.
Kongamano hilo limeandaliwa kwa dhamira ya kuja na mbinu za kisasa na endelevu za kuboresha utumizi wa ardhi, kuhifadhi mazingira na kukabilina na mabadiliko ya tabianchi.
“Tunafanya kazi pamoja na wadau wote wa Bodi za usajili kuhakikisha kuwa tumewakabili vilivyo matapeli. Tunahimiza umma kutoa taarifa za ulaghai kwa taasisi zetu za ISK, kwa Idara ya Upepelelezi na Makosa ya Jinai(DCI) ama tume ya madili na kupambana na ufisadi nchini Kenya(EACC) kuhusu visa vya wanakandarasi kukosa kutoa huduma halali kwa mujibu wa mkataba wa maafikiano ili hatua za haraka za kisheria zichukuliwe kukabili na kutatua masuala hayo.” Nyadimo alikariri.
Kongamano hilo la siku mbili linakamilika rasmi Ijumaa ya Novemba 8, 2024.