30/07/2023
Mwandishi ni Denis Mpagaze .
Mfahamu Mzee Mkapa: Rais Aliyeleta Ukombozi wa Kifikra na Uchumi; Waelewa Wakampa 5; Wajuaji Wakamtukana!
Denis Mpagaze
_________________________________
Mzee Mkapa aliingia madarakani nchi ikiwa imedumaa kiuchumi, akatawala kwa falsafa ya “Huwezi kupata maendeleo bila kubadili fikra” akasisitiza watu wafikiri kwa bidii hadi nchi ikakombolewa, waliozembea kufikiri aliwatukana hadharani wakamuita mbabe, dikteta na mwizi wa mali za umma kwa sababu ni hulka ya binadamu kushughulika na madhaifu ya mtu kuliko mazuri yake, hata Mungu huwa tunamfanyia hivyohivyo pale tunapotumia muda mwingi kumuomba vitu ambavyo hatuna badala ya kumshukuru kwa vitu vingi alivyotupatia.
Kuna mwalimu aliingia darasani na karatasi nyeupe zenye doa katikati, akawagawia wanafunzi kisha akawaambia kila mmoja alezee alichoona kwenye karatasi; wote walizungumzia doa limechafua karatasi. Mwalimu akawauliza ina maana hakuna aliyeona sehemu nyeupe kwenye karatasi?” Mliiona isipokuwa katika jamii ya walimwengu kosa moja litosha kufukuza mke. Maana yake ni kwamba ukimuangalia Mkapa kwa macho ya wanafunzi huwezi kuona meupe, utaishia kuona madoa yake tu.Karibu tuangalie meupe 13 kutoka kwa Mkapa!
Moja: Urais wa Mkapa ni message kwa wazazi kuacha kuwapangia watoto wao vitu vya kusomea, Mungu Aliishawapangia Makubwa! Huyu Mkapa aliyezaliwa Jumamosi ya tarehe 12 Novemba 1938 kijijini Lupaso Masasi baba yake alitamani awe padre wa jimbo akawa rais wa nchi. Najua baba alitamani hivyo maana aliishaonja utamu wa kumtumikia Mungu. Siunajua mzee alikuwa katikista pale Ndanda Mission, Masasi?
Basi bwana Ben akasoma msingi, sekondari hadi chuo kikuu. Msingi alisoma Lupaso na baadaye alikwenda seminari ya Junior Benedictine (Kigonsera) kuutafuta Upadre ili kutimiza ndoto ya baba yake, lakini Mungu akasema wewe ni Rais wa nchi, siyo Padre, ondoka upesi, Mkapa akarudi zake Ndanda kuendelea na Middle School, alivyomaliza darasa la kumi akataka kwenda uaskari, Mungu akasema wewe ni Rais wa nchi siyo askari,songa mbele, Mkapa akalisongesha hadi Pugu, enzi hizo Pugu inaitwa St.Francis College.
Pugu akaandika historia ya kufundishwa na Nyerere kisha wakatawanyika, Nyerere akaelekea kutafuta uhuru, Mkapa akaelekea kutafuta elimu ya juu nchini Uganda, akapiga miaka yake mitatu pale Makerere University, 1962 akatoka na jiwe lake la Lugha na Fasihi, akarudi kuitumikia nchi kwa nafasi ya Ukatibu Tawala Dodoma, milango ikafunguka, Mkapa akawa balozi, mbunge, waziri wazazi wakashuhudia uwaziri wa aliyetakiwa kuwa padre, halafu wakaondoka zao duniani bila kusubiria urais wa mwanao!
Mbili: Mkapa aliamini Tanzania inahitaji strong institutions not strong men ili kutoka mavumbini ndo maana akaanzisha taasisi kibao; palipo na umasikini alifungua TASAF na MKUKUTA maskini wakaanza kula na kushiba; palipokosa uhakika wa afya bora alifungua bima ya afya watu wakawa na uhakika na afya zao, palipojaa rushwa alianzisha TAKURU kuitokomeza; waliokosa uhakika wa elimu ya juu alianzisha TCU na Bodi ya Mikopo maskini wakaingia vyuo vikuu kwa mbwembwe na ushamba, k**a unavyojua tena maskini akipata ghafla!
Palipo na upotevu wa mapato, alianzisha TRA, mapato yakaongezeka karibu mara tatu kutoka dola 612,587 hadi kufikia dola 1,796,862, Benki ya; ili kulinda rasilimali za wanyonge alianzisha MKURABITA kurasimisha rasilimali zao wanyonge MKURABITA; ili kuvutia uwekezaji alianzisha TIC, wageni wakachangamkia fursa wazawa wakalala Mkapa akashangaa watanzania mko wapi?
Katika kuimarisha usalama wa nchi Mkapa alianzisha TISS nchi ikawa na usalama wa uhakika, yako mengi isipokuwa naomba sinichoshe, nisikuchoshe, tusichoshane kuyataja yote, k**a vipi tafuta kitabu chake yamo yote! Kinaitwa My Life; My Purpose!
Tatu: Albert Einstein aliposema ukiwa na mawazo mafupi yasiyozidi mwaka mmoja panda mpunga, ukiwa na mawazo yanayoishia miaka kumi panda mti, ukiwa na mawazo makubwa kupita miaka 100 panda elimu kwa watu wako, Mkapa alipanda elimu kwenye vichwa vya watanzania kwa sababu fikra na mawazo yake yalipitiliza miaka mia. Aliamini maendeleo huanzia kichwani. Kichwa kisipokaa vizuri utaitesa midomo yako kwa kuzungumza watu badala ya issue halafu ukiambia uache wivu wa k**e unarusha ngumi.
Halafu alishirikisha taasisi za dini kutoa elimu ya juu kwa watanzania kwa sababu wahenga waliishamwambia asingeweza kukweya mnazi kwa mkono mmoja. Mkapa akatoa majengo ya Mazengo Sec kwa waanglikana wakaanzisha St. Joseph University Dodoma, majengo ya Benki Iringa wakapewa wakatoliki wakafungua Ruaha University; majengo ya TANESCO Morogoro wakapewa waisilamu wakaanzisha Chuo Kikuu cha Kiislamu, majengo ya sekondari ya Magamba Rushoto wakapewa waluteri wakaanzisha Sebastian Kolowa Memorial University, watanzania wakajimwaga vyuo vikuu, elimu ya chuo kikuu ikawa kitu cha kawaida nchini, vyuo vikuu vikazagaa kila kona ya nchi k**a tution, full kuzalishia wasomi huru gerezani, Mzee Magufuli alivyoshika nchi akavitia kabale, vyuo janja janja vikafa kifo cha mende, mashaka yakatanda kwa waliosoma huko itakuaje?
Nne: Mkapa aliuchukia umaskini kwa sababu palipo na umaskini chuki na wivu hutamalaki, maskini anaweza kupiga vibarua kutafuta pesa ya kumloga mwenzake kisa tu anamshahara wa ukatikista. Hili Mkapa alilishuhudia kwao jinsi maskini walivyomuonea wivu baba yao katikista na kuibambikizia familia yake kwamba ni wachawi hadi wamesababisha uchawi. Ramli ilipigwa na mganga kwa malipo ya maskini wenye wivu. Mama yake Mkapa na bibi walikula kisago hadi bibi akapoteza maisha. Ilikuwa mwaka 1947. Unajua tatizo la umaskini unakimbilia kula ubongo.
Ili kuwapa ahueni maskini Mkapa alifuta kodi ya kichwa iliyowafedhehesha wazee wetu nadhani tulioishi enzi zile tunakumbuka, kuna wazee na ndevu zao walishinda porini kuwakwepa askari mgambo baada ya kukosa shilingi mia ya kulipa kodi! Maskini alinuka katika nchi huru. Maskini alivaa nguo zenye viraka katika nchi huru. Suruali ya baba likiisha lilishona kaptura za watoto.Mkapa aliifuta hadi kodi ya baiskeli na mifugo ili kumpa ahueni maskini.Mkapa alicontrol mfumko wa bei ili kumlinda mnyonge. Katika utawala wake kilo ya sukari tuliinunua kwa shilingi mia tano kwa muda mrefu!
Aliandaa mazingira mazuri na kuwataka maskini wachape kazi kwani mtaji wa maskini ni nguvu zake mwenyewe. Alipenda kusema sisi ni maskini mfukoni lakini matajiri kichwani, kasoro haziondoki kwa uhodari wa kuzianisha, la msingi ni kujenga uwezo wa uchumi wa kisasa. Hatuwezi kuweka fedha mifukoni mwenu ila tutandaa fursa za kupata pesa. Mazingaombwe ya kujazana mapesa muachieni Cheyo wa Bariadi. Tunatakiwa kubadilisha maisha yetu au tutabadilishwa tutasombwa k**a vile mawimbi alisemq Mkapa.
Mkapa alichukua nchi hii watu wanatembea peku, lakini ameicha watu wote wamevaa viatu, Mzee Mwinyi ni shahidi, alitusimulia siku ya masishi ya Mkapa, anasema alishangaa watu wote waliokuja kumuaga Mkapa pale kijijini wote wamevaa viatu.
Enzi zake hadi wajumbe wa nyumba kumi walikanyaga Ikulu wakala na Rais, siku hizi thamani ya wajumbe inaonekana siku ya uchaguzi tu, ndo maana nao wameamua kuwakomesha! Wanatumia falsafa ya tuko pamoja lakini ukigeuka nyuma huwakuti.
Tano: Mkapa hakupenda kuabudiwa kabisa ndo maana alikataa kuitwa Mtukufu Rais k**a walivyoitwa Mtukufu Al-Hassan Mwinyi na Mtukufu Daniel Arap Moi; alikataa picha yake kutumika kwenye sarafu, alipata PhD nyingi za heshima lakini hakukubali kamwe kuitwa Dr. Mkapa, haata barabara ya kwenda kwao imekuja kujengwa na Rais Magufuli kwa fedha za serikali. Magufuli anasema Mkapa hakupenda vitu viitwe kwa jina lake, sasa kuanzia leo uwanja wa mpira utaiwa Mkapa Stadium najua hatanifanya kitu.
Mkapa ndo alitujegea uwanja wa kisasa hadi Brazil wakaja kuweka kambi tukawaona akina Ricardo Kaka, Robinho Do Santos na Ruis Fabiano live. ‘Taifa Stars’ na Brazil wakakipiga mwaka 2010, tukafungwa 5-0. Siku ya uzinduzi wa uwanja Septemba 2007 tulimtia aibu Mkapa kwa kufngwa 1-0 na Msumbiji.
Hakupenda kuonyeshwa kwenye TV mara kwa mara k**a Moboutu Seseko na hivyo aliziasa luninga ziwe zinaonyesha mambo mengine ya maendeleo hususan ya vijijini.
Mkapa alisaidia wengi bila kuitangazia dunia k**a mnavyofanya nyie. Alitumia kanuni ya utoapo utoapo fanya kuwa siri ikiwezekana hata mkono wako wa kushoto usione! Soma Mathayo 6:3! Tujifunze kwa Ben. Aliwasaidia wengi na ikabaki kuwa siri yake. Kuna mzee alimlipia dola elfu 20 kwa ajili ya matibabu ya binti yake akabaki kupigwa na butwaa. Lakini pia aliwahi kutinga mahak**ani kumtetea Prof. COSTA MAHALU, aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, kwa kosa la kuisababishia serikali hasara ya € 2, 065, 827.60 kuhusiana na jengo la ubalozi huo. Balozi Mahalu akapona na sasa ndo VC wa SAUT.
Sita: Mkapa alikuwa msomaji mzuri wa vitabu ndo maana alijua mengi! Kutosoma vitabu ni kujiongezea janga la umaskini alipenda kusema Mkapa. Mbele ya Mkapa k**a husomi na kufanya tafiti alikuona kenge. Waandishi walipata taabu sana enzi zake. Aliwaita wavivu wa kufikiri. Kufikiri sio kipaji ni tabia. Hotuba za Mkapa zilikonga nyoyo za wengi kwa sababu ya utamaduni wake wa kufikiri. Enzi zake nchi ilikaa kimya kumsikiliza mwanaume akiongea. Aliongea kila mwezi. Mkapa aliargue hakushout!
Mkapa alikuwa k**a "library" inayotembea. Alipenda kusema "No Research, No Right to Speak". Tunaongea vitu juu juu tu kwa sababu hatuchimbi. Tunajadili sana uvumi kuliko "issues". Halafu watu wanaosoma vitabu huwa wana majibu ya kuudhi wakigundua unabwabwaja. Mfano siku ya meimos watu walivyolalamika eti ameshindwa kulinda ajira za wazawa na kuwaachia wageni alisema, “Mimi sijali rangi ya paka najali k**a anak**ata panya au la". Someni vitabu ili muendelee kupata maarifa. Maarifa ni nguvu kubwa zaidi ya vifaru. Unaweza soma hata vitabu vya Mpagaze vya wasomi Huru Gerezani na Ukombozi wa Fikra basi.
Saba: Nyumbani Mkapa atakumbukwa daima k**a Rais aliyekuza uchumi, kujenga taasisi imara na kufanya makosa kwenye ubinafsishaji na uuzwaji wa nyumba za serikali na kufanya toba miezi nane kabla ya kufa kwa sababu kukosea ni ubinadamu kukiri makosa ni uungwana, lakini huko nje Mkapa atakumbukwa daima k**a mpatanishi wa amani. Kenya Mkapa anakumbukwa kwa kutuliza lile sekeseke la Uchaguzi Mkuu mwaka 2007 liliondoka na roho za wapendwa wetu 1,000; Burundi nako, Mkapa alimaliza vurugu za warundi waliopigana bila sababu ya msingi na kufanya uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia kwa Nkurunziza kuingia madarakani; Rwanda nako Mkapa aliwasaidia kuponya madonda ya mauaji ya kimbari!
Nane: Mkapa ndo alikuza uhuru wa habari ingawa washikaji zake wanamponda kwamba ndo aliua uhuru wa habari. Imani ya Mkapa kwa vyombo vya habari ilikuwa juu sana. Hakula chakula cha jioni pasipo kusikiliza taarifa ya habari k**a wewe usivyokula kabla hujachat.Alisoma sana magazeti hadi barua za wasomaji na wakati mwingine aliwaagiza wasaidizi kuwatafuta waandishi wa barua zilizomgusa. Waandishi wengi wa Tanzania aliwaita wavivu wa kufikiri kutokana na aina ya habari walizoandika na maswali mepesi waliyomuuliza. Waandishi wengi waliuliza maswali ya kutafuta uteuzi.
Ilifikia wakati akakosa imani na vyombo vetu baada ya kusema yanayosemwa na vyombo vya habari ni uongo, ni wivu tu umewajaa, hakuna baya alilofanya ila ni wivu tu ambao unatokana na uvivu wetu wa kufikiri.
Mkapa aliwabana kwa sababu amewahi kufanya uandishi hivyo anajua mwandishi makini na chenga. Mkapa amewahi kutangaza RTD na kuhariri magazeti ya chama pamoja na Daily News, alitumia jina la bandia kuwakosoa viongozi kupitia gazeti. Alijiita "Mwana wa Matonya! Lakini pia ndo mwanzilishi wa SHIHATA, yaani Idara ya Habari Maelezo ya leo. Mkapa amefariki muda mfupi baada ya kuangalia TV.
Tisa: Katika utawala wake Mkapa alikutana na majanga mazito yakamuimarisha badala ya kumdhofisha ndo maana hakuikimbia Ikulu. Mei 21, 1996, mwaka mmoja tu baada ya kuingia madarakani likatokea balaa la kuzama kwa meli ya MV Bukoba, mwaka uliofuta yaani 1997 mafuriko ya el nino yakavuruga nchi, Februari 13, 1998 sekeseke la mauaji ya mwembe chai likatia doa utawala wake, Oktoba 14, 1999 baba wa Taifa akaondoka duniani, Januari 27, 2001 mauaji ya Pemba yakautia doa tena utawala wake, Julai 4, 2001 makamu wa Rais Dr. Omar Ali Juma akaaga dunia!
Mkapa anakili kupitia kitabu chake kwamba tukio la mwaka 2001 la kuuawa waandamanaji 22 na polisi kisiwani Pemba waliokuwa wakipinga matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar wa mwaka 2000 lilimtikisa vilivyo lakini alivilaumu sana vyombo vya habari kulikuza. Alikuwa na wasiwasi pale Rais wa Zanzibar Salmin Amour alipotaka kubadilisha sheria na kutawala kipindi cha tatu. Lakini baadae yeye na wafuasi wake wakaamua yaishe.
Kumi: Mkapa aliumia sana aliposhambuliwa yeye binafsi na familia yake kwa mambo yaliyohusu nchi. Madai kwamba alimpendelea baba mkwe wa mwanaye katika kubinafsisha mgodi wa makaa ya mawe Kiwira yalimuumiza sana. Pia madai kuwa aliwapendelea NET GROUP solutions Ltd wakati wa kubinafisha TANESCO kwa sababu ya shemeji yake kulimuumiza sana pia.
Anasema hata mashumbulizi aliyorushiwa kuhusu matumizi ya anwani ya Ikulu wakati yeye na mke wake walipochukua mkopo NBC kununua nyumba walikuwa wanaishi Ikulu hayakuwa fair. Hata suala la EPA lilimuumiza sana ingawa liliibuka tayari ametoka madarakani. Anasema Gavana wa Benki Kuu enzi hizo Daud Bilali ndo alimuingiza chaka.
Kumi na moja: Mkapa aliamini uwepo wa vyama vingi vya siasa unadhoofisha demokrasia ndo maana hakuvikubali kabisa ingawa alivivumilia. Aliwahi kusema ushauri unatokana na nguvu ya hoja tutaupokea lakini ushauri unatokana hoja ya nguvu tutaikataa. Na kweli hilo alilionyesha hadharani pale watu walipoonyesha kwenda tofauti na hoja zake. Vyama vinavyosema vinajiandaa kuikomboa Tanzania ni wapumbafu, malofa, Tanzania iliishakombolewa na CCM. Hata wakati anafungua nyumba za Mkapa pale Chato alirudia hilo.
Aliwahi kusema yeye siyo soft, hajui kubembeleza na katika hilo mke wake alimuelewa vizuri. Anasema mke wake Anna ndo gundi iliyo shikilia familia. Anakiri kuwa yeye siyo mtu rahisi kuishi naye na anamshukuru kwa kuwa mtu wa subira. Wafanyabiashara wanaingia kwenye siasa ili kulinda maslahi, wasomi wanaingia kwenye siasa kutafuta safari na posho. Nitamuachia Mungu wangu na nyinyi kuamua ni tofauti gani nimeifanya humu duniani.
Kumi na Mbili: Umahiri wake katika kazi ulimsaidia Mkapa kuaminika sana. Mkapa amekuwa balozi Nigeria, waziri wa mambo ya nje mara mbili, enzi za Mwinyi na Nyerere 1977-1980 na enzi za Mwinyi 1984 -1990, amekuwa waziri wa Habari na Utamaduni 1980-1982, amekuwa waziri wa habari na utangazaji 1990-1992 na Waziri wa Sayansi Teknolojia na Elimu ya juu 1992-1995.Hama hama zilivyozidi ilibidi watoto wao wabaki Marekani kukamilisha masomo yao. Hii dunia bwana, na wakati wewe mabosi wako wanakaa vikao kila siku kuangalia ni namna gani wakufukuze, Mkapa mabosi wake walimgombania.
Kumi na tatu: Mkapa aliipenda Afrika ndo maana hata baada ya kustaafu aliendelea kutupigania sana waafrika na siku zote alikuwa akiwashutumu mabeberu kwa hadaa zao dhidi ya Afrika. Alikuwa sehemu ya kundi hili la viongozi wa Afrika waliojipambanua k**a kizazi kipya kinachotafuta suluhisho la matatizo ya watu wake kutoka ndani. Viongozi hao ni pamoja na Thabo Mbeki, Meles Zenawi, Olusegun Obasanjo, Abdelaziz Bouteflika na Abdoulaye Wade.
Kumi na nne: Mkapa anatufundisha kwamba ndoa ni zaidi ya dini zetu. Jamaa alikuwa mume wa mke mmoja na watoto wawili. Alioa mwaka 1966 akiwa kijana wa miaka 28. Alimuoa Anna Joseph Shauri Maro wakati huo mtumishi wa wizara ya habari, aliyesomea Uingereza. Ndoa yao ilifungwa ukweni Moshi katika kanisa katoliki. Mkapa alibaki kuwa mkatoliki kwa maisha yake yote na Anna ameendelea kuwa mlutheri hata sasa kwa sababu walipendana kwa dhati.
Halafu Mkapa alisikiliza sana mawazo ya mke wake pengine ndo maana alifanikiwa maana wanawake ni wabeba maoni. Wakati mwingine wajumbe wamekushughulikia kwa sababu hukumshirikisha mkeo kwamba unatia nia akakuombea!
Wazo la Mkapa kugombea Urais lilianzia kwa Jenerali Ulimwengu na vijana wenzake waliokuwa bungeni enzi hizo, wazo likaenda kwa Mzee Warioba na kufika kwa Mkapa, Mkapa akalipeleka kwa wife, theni kwa jamaa zake na mwisho kwa Mzee Nyerere. Nyerere alishangaa lakini akakubali kumuunga mkono ingawa alikuwa na mgombea wake, Salim Mohammed Salim. Wengi walipigwa butwaa siku Mkapa alipochukua fomu. Jamaa hakuwa na umaarufu kwa sababu aliishi sana nje, lakini pia hakuwa msemaji sana hadi Augustine Mrema akamwita "Bubu". Kuna magazeti yaliandika kwamba Ken Mkapa wa Yanga alijulikana zaidi Tanzania kuliko Mkapa. Kwenye kampeni za Mkapa, Jenerali Ulimwengu alikuwemo, sema walikuja kuzinguana baadaye! Watoto hao ni Nicodemus Mkapa ambaye ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi.
Nimalizie kwa kusema, ingawa Mkapa alikuwa tafu muda wote waliokuwa karibu naye wanasema ni mtu aliyependa matani na kuchekesha sana. Hata ule upara alisema ulitokana na kubeba vyombo shuleni. Shuleni walijipikia. Anasema alipokuwa chuoni watoto wa k**e walimzimia kishenzi kwa sababu alijenga hoja.
The Big Ben amelala lakini fikra zake ziko macho ndo maana tunamuita hayati na siyo marehemu. Ukifa bila kuacha alama unaitwa Marehemu, ukiacha alama na fikra zinazoishi unaitwa Hayati! Alipinga wazo la kuzikwa Ikulu katika sehemu iliyopangwa na serikali lakini alisema hapana, akifa arudishwe kwao. Amerudishwa kwao baada ya kufa kwa ugonjwa wa malaria na moyo kusimama ghafla!
Pumzika kwa Amani the Big Ben!