15/04/2022
URUSI KUANDAA MPANGO KUISAIDIA AFRIKA, PUTIN KUHUTUBIA VIONGOZI WAKE
NCHI ya Urusi, imetangaza kuandaa mpango maalumu wa kuzisaidia nchi za Afrika, katika kukabiliana na athari za vita kati yake na Ukraine.
Hayo yamesemwa leo Ijumaa na Naibu Mwenyekiti wa K**ati ya Baraza la Shirikisho la Mambo ya Nje Urusi, Andrey Klimov, katika mkutano wake na waandishi wa habari wa Afrika, uliofanyika kwa njia ya mtandao.
Klimov amesema, mpango huo maalumu wa kuzisaidia nchi za Afrika, unalenga kuimarisha mahusiano kati ya Urusi na Afrika, huku akiahidi mabalozi wa taifa hilo barani Afrika, watazungumza na maafisa wa masuala ya kigeni wa nchi husika, kuhusu utekelezwaji wa mpango huo.
Aidha, Klimov amesema aimeonya uwezekano wa dunia kukumbwa na baa la njaa, endapo vikwazo vya kiuchumi dhidi yake havitaondolewa haraka iwezekanavyo.
Klimov amesema, Urusi ambayo ni wazalishaji na wasambazaji wakubwa duniani wa mafuta, ngano, gesi , wamewekewa vikwazo vya kiychumi na usafirishaji, ambavyo vinasababisha washindwe kusambaza bidhaa hizo muhimu katika nchi wahitaji, hasa za Afrika, Asia na Amerika ya Kusini.
“Bandari ya Urusi tunayotumia kusambazia chakula kuleta kwenu, kupitia Bahari ya Mediterranean imefungwa, hatuwezi kusambaza. Vikwazo hivi vilivyo kinyume cha sheria havidhuru Urusi, tuna usalama wa kutosha. Lakini inatishia Afrika na nchi nyingine ambazo hazina usalama wa chakula,” amesema Klimov.
Aidha, Klimov amesema, kwa kuwa nchi yake imewekewa vikwazo katika matumizi ya mifumo ya kifedha duniani, nchi za Afrika zinaweza kununua bidhaa zake kwa kutumia fedha yake, Rubble.
“Mnaweza kufikiria jinsi Urusi ilivyopigwa marufuku kufanya miamala, Afrika inaweza kufanya miamala kwa kutumia Rubble,” amesema Klimov.
Klimov amesema, shirikisho hilo litaanda mkutano kati ya Urusi na nchi za Afrika, utakaofanyika Novemba 2022, ambapo Rais wa nchi hiyo, Vladimir Putin atahutubia.
“Mwaka huu shirikisho litafanya kazi na Afrika, Urusi itafanya mkutano na Afrika. Mkutano unaokuja utafanyika Novemba 2022. Tutajadili kuhusu hili. Tutafafanua operesheni yetu maalumu ya kijeshi nchini Ukraine, tutarejesha mahusiano yetu ambayo yameharibiwa na nchi za mashariki,” amesema Klimov.