Islamic Swahili TV

  • Home
  • Islamic Swahili TV

Islamic Swahili TV Mafundisho ya Qur'aan na Sunnah kwa ufahamu wa wema waliotangulia.

MUISLAMU LIOGOPE JELA LA BUWLAS, JELA LENYE MATESO YA KIWANGO CHA MWISHO.Wote bila shaka tunaiogopa jela kutokana na mad...
25/12/2024

MUISLAMU LIOGOPE JELA LA BUWLAS, JELA LENYE MATESO YA KIWANGO CHA MWISHO.

Wote bila shaka tunaiogopa jela kutokana na madhila na hali mbaya ya kimaisha iliyomo humo. Kuna jela kwenye baadhi ya nchi zimejaa ukatili na unyama ambao umevuka mipaka yote ya kiutu. Kuna zingine mtu akiingia huko hatoki tena, na hata akitoka, basi hata jamaa zake wanashindwa kumtambua kutokana na alivyochakarishwa humo. Hii ni mbali na kukosa uhuru wa mtu aliouzoea, kwani maisha humo ni amri tupu. Wafungwa wanaweza kuamriwa kulala saa 11 jioni na kuamka saa 10 alfajiri. Lakini kutokana na hali hiyo, inabidi kuzoea tu.

Hii kwa kifupi ndio jela ya dunia. Sasa huko aakhirah, kuna jela inayojulikana k**a “BUWLAS”. Jela hii ni mahususi kwa wote wenye kiburi hapa duniani. Kiburi maana yake ni kuikataa haki iliyo dhahiri yenye ushahidi kamili. Ni k**a Firauni alivyokataa kumwamini Muwsaa (‘Alayhis Salaam) pamoja na muujiza aliouona ambao uliwafanya wachawi mabingwa waamini na kuporomoka kusujudu. Kiburi pia ni kuwadharau watu kutokana na hali aliyonayo mtu ya utajiri, au cheo, au mamlaka, au elimu, au utaifa, ukabila na kadhalika. Wote wenye tabia hizi, basi wanasubiriwa na jela hii ya “Buwlas”.

Jela hii ikoje? Wenye kiburi watafufuliwa vipi Siku ya Qiyaamah kabla ya kuswekwa humo? Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) anasema:

"يُحْشَرُ الْمُتَكَبِّرُونَ يَوْمَ الْقِيَامَةِ أَمْثَالَ الذَّرِّ فِي صُوَرِ الرِّجَالِ، يَغْشَاهُمُ الذُّلُّ مِنْ كُلِّ مَكَانٍ، فَيُسَاقُونَ إِلَى سِجْنٍ فِي جَهَنَّمَ يُسَمَّى بُولَسَ، تَعْلُوهُمْ نَارُ الأَنْيَارِ يُسْقَوْنَ مِنْ عُصَارَةِ أَهْلِ النَّارِ طِينَةِ الْخَبَالِ ‏"‏.‏ قَالَ أَبُو عِيسَى هَذَا حَدِيثٌ حَسَنٌ.‏

“Wenye kiburi watakusanywa Siku ya Qiyaamah (kwenye uwanja wa mahshar) wakiwa mfano wa chembe ndogo mno iliyo katika umbo la mwanaume, na watafunikwa na udhalili kutoka kila mahali. Halafu wataswagwa kupelekwa kwenye jela iliyoko ndani ya Jahannam iitwayo “Buwlas”. Moto wa mioto utawafunika juu yao, na watanyweshwa usaha na taka mwili za watu wa motoni (ambazo ni) “Twiynatul Khabaal”. [At-Tirmidhiy: (2492)]

Watakuwa wanakanywagwa na watu hapo ikiwa ni malipo ya mfano wa kiburi walichokuwa nacho hapa duniani.

Tusisahau kwamba neema zote tulizonazo tumetunukiwa na Allaah k**a majaribio. Tusije kujisahau tukaingia kwenye kundi hili tukaishilia kusekwa kwenye jela ya “Buwlas”.

Kwa faida zaidi JIUNGE na group letu la Facebook la UISLAMU CHAGUO LANGU na LIKE page yetu ya Facebook ya Islamic Swahili TV na FOLLOW Account yetu ya Facebook ya Al Furqaan.

Wabillaahi at-Tawfiyq.

KULENI NA KUNYWENI NA WALA MSIFANYE ISRAFU ,HAKIKA YEYE ALLAAH HAPENDI WANAOFANYA ISRAFU.Tukijaribu kuhesabu vinywaji vy...
22/12/2024

KULENI NA KUNYWENI NA WALA MSIFANYE ISRAFU ,HAKIKA YEYE ALLAAH HAPENDI WANAOFANYA ISRAFU.

Tukijaribu kuhesabu vinywaji vya halali tunavyotumia, bila shaka tutakuta ni vingi sana kuanzia vya moto hadi vya baridi. Tuna chai ambayo inajulikana na watu wote na imekuwa ni katika biashara kubwa zinazoongoza duniani ikifuatiwa na kahawa. Tuna maziwa, vinywaji baridi vya aina mbalimbali, juisi na kadhalika bila kusahau maji ambayo yanawashirikisha viumbe wote hai.

Vinywaji vyote hivi tunavyovitumia, ni katika neema kubwa kabisa tulizokirimiwa na Allaah Ta’aalaa k**a wanadamu kulinganisha na viumbe wengine. Na kwa ajili hiyo, tunatakikana tuitumie neema hii kwa njia inayomridhisha Allaah kwa kutokufanya israfu au mengine yasiyostahiki k**a Anavyotuambia:

"وَكُلُوا وَاشْرَبُوا وَلَا تُسْرِفُوا إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُسْرِفِينَ"

“Na kuleni na kunyweni, na wala msifanye israfu, hakika Yeye (Allaah) Hapendi wanaofanya israfu”. [Al-A’araaf: 31]

Israfu ni tabia mbaya inayomchukiza Allaah. Tabia hii inahatarisha mtu kunyan’ganywa neema yoyote aliyopewa na Allaah Mtukufu. Israfu ni kutumia kitu katika halali lakini kwa ziada isiyohitajika. Mfano mdogo tu ni yale yanayoshuhudiwa kwenye mialiko ya walima na mingineyo ambapo sinia ya kuliwa na watu sita, wanawekewa watu wawili tu, na kinachobaki kinamwagwa. Tabia hii kwa kiasi kikubwa imepungua sana pengine kutokana na gharama za maisha kupanda, au watu kiasi fulani kujirekebisha na tabia hiyo.

Ili kujiepusha na israfu, kwa mfano, k**a una kiu kidogo, basi weka maji kiasi tu cha kumaliza kiu chako. Usije kujaza gilasi, maji yakakushinda, kisha ukayamwaga. Hayo unayoyamwaga ni sehemu ya Neema ya Allaah ambayo utakuja kuulizwa Qiyaamah.

Tujiepushe na israfu katika vinywaji ili kuidumisha neema hiyo. Tusishangae kuona nchi mbalimbali zikikabiliwa na ukame wa muda mrefu unaoleta maafa hata kwa mifugo. Huenda ni baadhi ya matokeo ya israfu zetu.

Kwa faida zaidi JIUNGE na group letu la Facebook la UISLAMU CHAGUO LANGU na LIKE page yetu ya Facebook ya Islamic Swahili TV na FOLLOW Account yetu ya Facebook ya Al Furqaan.

Wabillaahi at-Tawfiyq.

MOJA YA NEEMA YENYE MAZINGATIO KWETU WANAADAMU NI NEEMA YA CHAKULA.Kila siku tunakula na kunywa. Tukitaamuli safari ya c...
20/12/2024

MOJA YA NEEMA YENYE MAZINGATIO KWETU WANAADAMU NI NEEMA YA CHAKULA.

Kila siku tunakula na kunywa. Tukitaamuli safari ya chakula tulichotengewa mezani au mkekani, tutakuta safari yake ni ndefu kuanzia kilipokuwa mbegu shambani, kukua hadi kukomaa, kuvunwa na kufikishwa sokoni hadi mezani mbele yako. Hii ni katika neema kubwa za Allaah ambazo wengi tunaghafilika nayo. Allaah Akituzindusha kuhusu neema hii Anatuambia:

"فَلْيَنظُرِ الْإِنسَانُ إِلَىٰ طَعَامِهِ • أَنَّا صَبَبْنَا الْمَاءَ صَبًّا • ثُمَّ شَقَقْنَا الْأَرْضَ شَقًّا • فَأَنبَتْنَا فِيهَا حَبًّا • وَعِنَبًا وَقَضْبًا • وَزَيْتُونًا وَنَخْلًا • وَحَدَائِقَ غُلْبًا • وَفَاكِهَةً وَأَبًّا • مَّتَاعًا لَّكُمْ وَلِأَنْعَامِكُمْ"

“Basi atazame mwana Aadam chakula chake • Kwamba Sisi Tumemimina maji kwa uneemefu • Kisha Tukaipasua ardhi ikafunguka (kwa mimea) • Tukaotesha humo nafaka • Na mizabibu na mimea ya mboga (ikatwayo ikamea tena) • Na mizaituni na mitende • Na mabustani yaliyositawi na kusongamana • Na matunda na majani ya malisho ya wanyama • Yakiwa ni manufaa kwenu na kwa wanyama wenu wa mifugo”. [‘Abasa: 24-32].

Kila neema tuliyopewa na Allaah, basi tujue ina thamani yake, na thamani yake ni kuitunza vyema, kuitumia vyema na kumshukuru Allaah. Kila neema tuliyonayo, iwe ndogo, iwe kubwa, basi kwa hakika, bila shaka, tutakuja kuulizwa Siku ya Qiyaamah. Allaah Anatuambia:

"ثُمَّ لَتُسْأَلُنَّ يَوْمَئِذٍ عَنِ النَّعِيمِ "

“Kisha bila shaka mtaulizwa Siku hiyo kuhusu neema. [At-Takaathur: 08]

Miongoni mwa vipengele vya kushukuru neema ya chakula au kinywaji, ni kumhimidi Allaah baada ya kumaliza kula. Matamshi mengi ya himdi na du’aa yamethibiti toka kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumaliza kula. Kati yake ni:

1- "الْحَمْدُ لِلَّهِ الَّذِي كَفَانَا وَأَرْوَانَا، غَيْرَ مَكْفِيٍّ، وَلاَ مَكْفُورٍ"

“Himdi Anastahiki Allaah Ambaye Ametutosheleza mahitajio yetu na Akatuondoshea kiu, hazilipiki (Fadhila Zake) wala hazikanushiki”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5459)].

2- "الْحَمْـدُ للهِ حَمْـداً كَثـيراً طَيِّـباً مُبـارَكاً فِيْهِ، غَيْرَ مَكْفِيٍّ وَلا مُوَدَّعٍ وَلا مُسْتَغْـنىً عَنْـهُ رَبَّـنا"

“Himdi Anastahiki Allaah, himdi zilizo nyingi, zilizo njema na zilizojaa baraka tele ndani yake, haziwezi kulipika, wala kuachwa, wala kutohitajiwa tena, ee Rabbi wetu”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5458), Abu Daawuwd (3849), Ibn Maajah (3284 na Ahmad (5/256)].

3- "الْحَمْدُ لِلَّهِ الَّذِيْ أَطْعَمَ وَسَقَى وَسَوَّغَهُ وَجَعَلَ لَهُ مَخْرَجًا"

“Himdi Anastahiki Allaah Ambaye Amelisha, Amenywesha, Akakifanya (chakula) kuwa chepesi kuingia mwilini, na Akakiwekea njia ya kutoka mwilini.” [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (3851) na Ibn As-Sunniy].

4- "اللّهُمَّ أَطْعَمْتَ وَسَقَيْتَ وَأَغْنَيْتَ وَأَقْنَيْتَ وَهَدَيْتَ وَأَحْيَيْتَ، فَلَكَ الحَمْدُ عَلَى مَا أَعْطَيْتَ"

“Ee Allaah! Umelisha, Umenywesha, Umetosheleza, Umekinaisha, Umeongoa, na Umehuisha. Basi ni Yako Himdi kwa yote Uliyotoa”. [Hadiyth Hasan. Imekharijiwa na Ahmad katika “Al-Musnad” nambari 1600].

Duaa hizi ni sehemu ya kutusaidia maswali yanayotusubiri Siku hiyo.

Kwa faida zaidi JIUNGE na group letu la Facebook la UISLAMU CHAGUO LANGU na LIKE page yetu ya Facebook ya Islamic Swahili TV na FOLLOW Account yetu ya Facebook ya Al Furqaan.

Wabillaahi at-Tawfiyq.

MUDA MFUPI UJAO UNAKWENDA KATIKA KITUO CHA KWANZA CHA AKHERAH (KABURINI) , USIJISAHAULISHE.Mtu akilala na kuamka, ukamuu...
19/12/2024

MUDA MFUPI UJAO UNAKWENDA KATIKA KITUO CHA KWANZA CHA AKHERAH (KABURINI) , USIJISAHAULISHE.

Mtu akilala na kuamka, ukamuuliza hapo hapo ni saa ngapi, bila shaka hawezi kukujibu. Ili kukujibu, ataitafuta saa. Ukimuuliza ni masaa mangapi kalala, pia hawezi kuwa na jibu.

Na mtu aliyepoteza fahamu pia, kwa ajali au kwa sababu nyingine yoyote, akirudisha fahamu, basi hawezi kujua muda aliopoteza fahamu mpaka aambiwe na yote yaliyojiri.

Vijana waliokimbilia pangoni, Allaah Aliwalaza kwa muda wa miaka 309. Lakini Alipowaamsha, walihisi k**a wamelala kwa muda wa siku moja tu au sehemu ya siku. Hawakujua kabisa k**a wamelala muda wote huo wa karne tatu. Haya yote ni kwa kuwa wakati mtu anapolala, anakuwa hana tena mahusiano na wakati. Kwa kuwa tunapokuwa macho, wakati tunauhisi kwa kufuatilia mwenendo wa jua, au kwa kutizama saa na kadhalika. Mtu k**a hana saa, wala halioni jua, hawezi kabisa kujua wakati. Ni k**a watu waliofungwa jela ndani ya jela.

Na wakati tutakapokufa, tutaingia katika kanuni nyingine kabisa tofauti na kanuni za maisha yetu ya dunia. Huko hakuna jua la kutujulisha wakati, au mwezi wa kutujulisha miezi au miaka. Angalia -k**a inavyotueleza Qur-aan- mfano wa mtu yule aliyepita kwenye kijiji, akakikuta kimeporomoka na kubaki magofu tu. Akajiuliza vipi Allaah Ataweza kukirejesha tena k**a kilivyokuwa pamoja na watu wake waliokuwa wakiishi ndani yake?! Allaah Akamfisha mtu yule kwa muda wa miaka 100. Alipomfufua, Akamuuliza -kupitia kwa Malaika Wake- muda aliokaa pale akiwa maiti. Akajibu ni siku moja au baadhi ya siku. Ni sawasawa na walivyohisi vijana wa pangoni. Allaah Akamwambia kwamba amekaa pale kwa muda wa miaka 100, na chakula chake hakikuharibika wala kinywaji chake, lakini punda wake tu aliyekufa ndiye aliyebakia mifupa. Haya yote yanaelezwa na Aayah ya 259 ya Suwrat Al-Baqarah kuonyesha Uwezo wa Allaah.

Wengi wetu tunakiona Qiyaamah k**a kiko mbali sana, na kwamba kwenye makaburi tutakaa sana kukisubiri. La hasha! Kiko karibu kuliko tunavyodhania. Tutakapokufa, basi hapo kaburini kwenye maisha ya barzakh, ndio tutakuwa kwenye kituo cha kwanza cha aakhirah. Hapo hakuna saa ya kujua wakati, au jua la kuzama na kuchwa la kutujulisha siku mpya, au mwezi wa kutujulisha mwezi mpya wa hijria, huko mambo ni mengine kabisa. Watu watakuwa wanapambana na adhabu za kaburi, au wananeemeka na neema zake, huko pengine kuna nyakati za kihuko tofauti na za kidunia. Tahamaki, watash*tukia baragumu la pili linapulizwa na wanatoka makaburini kukabiliana na mengineyo yanayofuatia baada ya kufufuliwa. Rabbi tunaomba Hifadhi Yako Siku hiyo ngumu kabisa. Tunaomba tuwe salama kwenye Kivuli Chako. Tunaomba Tusalimike na kitisho na kizaazaa kikubwa cha Siku hiyo.

Hapo waliokaa makaburini miaka mamilioni, na waliokaa kwa wiki, wote watajiona k**a wamekaa huko siku moja au sehemu ya siku tu. Qaabiyl na Haabiyl wakifufuliwa leo, basi watajiona k**a wamekaa makaburini kwao siku moja tu au sehemu ya siku.

"كَأَنَّهُمْ يَوْمَ يَرَوْنَهَا لَمْ يَلْبَثُوا إِلَّا عَشِيَّةً أَوْ ضُحَاهَا"

“Siku watakapoiona, watakuwa k**a kwamba hawakubaki (duniani au makaburini) isipokuwa jioni moja au mchana wake”. [An-Naazi’aat: 46]

Na hapa ndipo tutakuja kugundua kwamba si umri wa ulimwengu, wala umri wa dunia yetu, wala umri wa maisha yetu ya duniani na ya barzakh, isipokuwa ni muda mfupi na mchache sana.

Kwa faida zaidi JIUNGE na group letu la Facebook la UISLAMU CHAGUO LANGU na LIKE page yetu ya Facebook ya Islamic Swahili TV na FOLLOW Account yetu ya Facebook ya Al Furqaan.

Wabillaahi at-Tawfiyq.

FIKIRIA HUU UCHAFU UNAOTOKA KATIKA MIILI YETU KILA SAA, TUJIANDAE NA MAJIBU YA KWENDA KUJIBU.Kila kitu kinachotoka kweny...
19/12/2024

FIKIRIA HUU UCHAFU UNAOTOKA KATIKA MIILI YETU KILA SAA, TUJIANDAE NA MAJIBU YA KWENDA KUJIBU.

Kila kitu kinachotoka kwenye mwili wa mwanadamu kinaonekana ni kichafu kuanzia haja ndogo na kubwa, jasho la mwili, k**asi, kohozi, mate na hata manii ambayo ndio tumeumbwa nayo. Kila kimoja kati ya hivi kinatofautiana na kingine kwa mujibu wa kilivyo. Na hata matapishi ambayo ni chakula kizuri kilichoingia tumboni na kuanza kuchakatwa, k**a yatatoka mtu akatapika, basi watu kuyaangalia mara mbili inakuwa ni mtihani.

Matapishi haya ndiyo huja kufyonzwa na mwili na kupelekwa maeneo tofauti ikiwemo sehemu ya kutengenezewa maji ya uzazi ambayo hatimaye hutulia katika sehemu yake kusubiri yachupishwe na kutulia kwenye ukuta wa tumbo la uzazi na kuanza mchakato baada ya mchakato hadi mtu kuzaliwa. Wote tumepitia mchakato huo, hakuna wa kubisha. Na hata manii hayo pia yanaonekana ni kitu kichafu ingawa si najisi.

Mada hizi zinazotoka mwilini k**a hazikuangaliwa kwa usafi stahiki, basi mtu atakuwa hakaribiki kutokana na harufu. Mtu akivaa soksi kwa siku mbili mfululizo bila kubadili, bila shaka ataudhi watu sana kwa harufu kali ya miguu. Mtu akilala, hata akapiga mswaki kabla ya kulala, akiamka atakuta kinywa kimekwishataghayuri kwa harufu. Nguo nazo inabidi kubadili takriban kila siku, la sivyo mambo yataharibika.

Hali hii ya maumbile yetu, huenda Allaah Ametuumbia nayo ili tujitathmini na kuondosha sifa ya kiburi. Ni k**a tunaambiwa kuwa ukiwa hai hali yako ni hii, sasa ukifa, basi mambo yatakuwaje! Na kwa ajili hiyo, mtu akifa tunaamuriwa tumzike haraka iwezekanavyo kabla hajaanza kuharibika. Hapa hakuna tofauti kati ya tajiri wala masikini, wala kiongozi wala raia, wote ni hali moja.

Huenda pia hali hii ikatufanya tupate ladha halisi ya Pepo, kwa kuwa Peponi hakuna hali k**a hizo. Mtu mwenye njaa kali, ndiye anayehisi ladha halisi ya chakula hata kwa kipande cha mkate mkavu, k**a huna njaa, basi hata chakula kiwe kizuri vipi, hutoweza kuburudika nacho itakikanavyo.

Kadhalika, inawezekana kuwa Allaah Anatutakia kheri zaidi kutokana na maumbile haya. Anataka tupate thawabu zaidi wakati tukijitahidi kwa usafi ili tusiwaudhi watu kwa harufu za kinywa, harufu ya kikwapa na harufu nyinginezo. Muislamu hulipwa thawabu kwa juhudi k**a hizi za usafi, na ni jambo ambalo Allaah pia Hulipenda k**a Anavyosema:

"إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ التَّوَّابِينَ وَيُحِبُّ الْمُتَطَهِّرِينَ"

“Hakika Allaah Anapenda wenye kutubia mara kwa mara, na Anapenda wenye kujitwaharisha”. [Al-Baqarah: 222]

Kiufupi, huenda hali hii ya vinavyotoka mwilini inatukumbusha pia kwamba sisi ndio tuliokirimiwa zaidi kuliko viumbe wengine kwa upande wa vyakula, mbogamboga, matunda na vinywaji ambayo imepelekea maumbile yetu yawe hivi. Hebu jaribu kuhesabu aina za vyakula, aina za mbogamboga, aina za matunda, aina za vinywaji nk. Hesabu aina za mafuta ya kupikia, samli za aina tofauti na vinginevyo vingi. Hivi vyote tunavila na kuvinywa na kuingia ndani ya miili yetu. Ni neema kubwa kwa kweli. Wanyama wala nyama ni nyama tu basi, hawahitaji tunda wala chai, ndege walao nafaka au wadudu, ni hivyo tu walavyo basi, hawahitajii juisi wala kahawa. Lakini sisi na hasa wenye uwezo, vinavyoliwa havihesabiki. Na haya yote tutakwenda kuulizwa ni vipi tuliyatumia. Hakuna neema ya bure tu hivi.

"ثُمَّ لَتُسْأَلُنَّ يَوْمَئِذٍ عَنِ النَّعِيمِ"

“Kisha bila shaka mtaulizwa Siku hiyo kuhusu neema”. [At-Takaathur: 08]

Tujiandae na majibu katika Siku hiyo ngumu kabisa.

Kwa faida zaidi JIUNGE na group letu la Facebook la UISLAMU CHAGUO LANGU na LIKE page yetu ya Facebook ya Islamic Swahili TV na FOLLOW Account yetu ya Facebook ya Al Furqaan.

Wabillaahi at-Tawfiyq.

NI ZOEZI LA KILA SIKU LENYE MAZINGATIO AMBALO VIUMBE WOTE TUNALIFANYA.Kila siku tunalala na kuamka.  Kabla ya kulala, tu...
18/12/2024

NI ZOEZI LA KILA SIKU LENYE MAZINGATIO AMBALO VIUMBE WOTE TUNALIFANYA.

Kila siku tunalala na kuamka. Kabla ya kulala, tunatayarisha vizuri kitanda kwa ajili ya kupata usingizi mzuri. Baada ya kupanda kitandani, huwa tunajaribu kuutafuta usingizi. Usingizi huu k**a ujulikanavyo ni mauti madogo. Na mauti haya madogo, yaani usingizi wenyewe, hauji ila baada ya roho kutoka mwilini. Unastukia tu usingizi umekuchukua bila kujua umekujaje.

Hapo roho inakuwa imetoka mwilini, kwani usingizi hauji ila kwa kutoka roho mwilini. Yeyote umwonaye kalala, basi ujue roho yake haipo, hapo anakuwa ndani akossa madogo. Viungo vyake vyote vya nje vinakuwa vimetulia tuli, na kinachobakia kikifanya kazi ni masikio tu. Allaah Anatuambia:

"اللَّـهُ يَتَوَفَّى الْأَنفُسَ حِينَ مَوْتِهَا وَالَّتِي لَمْ تَمُتْ فِي مَنَامِهَا ۖ فَيُمْسِكُ الَّتِي قَضَىٰ عَلَيْهَا الْمَوْتَ وَيُرْسِلُ الْأُخْرَىٰ إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ"

“Allaah Huzichukua roho wakati wa kufa kwake, na zile zisizokufa katika usingizi wake, kisha Huzizuia ambazo Amezikidhia mauti, na Huzirudisha nyingine mpaka muda maalumu uliokadiriwa. Hakika katika hayo bila shaka kuna ishara kwa watu wanaotafakari”. [Az-Zumar: 42]

Ndio maana Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa anaamka husema akimshukuru Allaah:

"الحَمْدُ لله الذِيْ أَحْيَانَا بَعْدَ مَا أَمَاتَنَا وَإِلَيْهِ النُّشُوْرُ"

“Himdi ni Yake Allaah Ambaye Ametuhuisha (Ametuamsha) baada ya Kutufisha (Kutupa usingizi), na Kwake ndio ufufuo”. [Al-Bukhaariy (6324)]

Hivyo basi, usingizi wetu huu ni k**a zoezi la kila siku la kuandaliwa akossa makubwa ya roho kutoka na kutorejea tena mwilini. Mauti hayo ni tofauti na haya madogo. Hayo yana sakaraat, yana vishindo, yana kufunuliwa pazia la kumwona Malaika wa kutwaa roho (Malakul Mawt) na Malaika wengineo wa adhabu au wa rahmah, na mengi mengineyo yanayohusiana na zoezi hilo na yanayofuatia. Hapo tutaona yote tunayohadithiwa na Qur-aan kwa mujibu wa hali ya mtu. Allaah Anatuambia:

"لَّقَدْ كُنتَ فِي غَفْلَةٍ مِّنْ هَـٰذَا فَكَشَفْنَا عَنكَ غِطَاءَكَ فَبَصَرُكَ الْيَوْمَ حَدِيدٌ"

“(Aambiwe): Kwa yakini ulikuwa katika mghafala na haya! Basi Tumekuondoshea kifuniko chako, basi kuona kwako leo ni kukali”. [Qaaf: 22].

Ndugu Muislamu! K**a unavyotandika kitanda chako kwa shuka nzuri, mito mizuri na mablanketi mazuri ili upate usingizi mnono, basi ujue kitanda hiki pia ni k**a kaburi lako dogo la mauti madogo. Na k**a unavyokitayarisha hivyo, basi litayarishe pia kaburi lako kubwa baada akossa makubwa kwa kila amali njema, na kujiepusha na kila baya, madhambi, dhulma na akossa mengineyo. Hilo haliepukiki, na safari yake ni ndefu.

Kwa faida zaidi JIUNGE na group letu la Facebook la UISLAMU CHAGUO LANGU na LIKE page yetu ya Facebook ya Islamic Swahili TV na FOLLOW Account yetu ya Facebook ya Al Furqaan.

Wabillaahi at-Tawfiyq.

ZINDUKA ! QIYAAMAH KIPO KARIBU SANA JE UNAJIANDAAJE NA TETEMEKO LA SIKU HIYO ?Tumesikia na kushuhudia tukio la kutokea t...
18/12/2024

ZINDUKA ! QIYAAMAH KIPO KARIBU SANA JE UNAJIANDAAJE NA TETEMEKO LA SIKU HIYO ?

Tumesikia na kushuhudia tukio la kutokea tetemeko kubwa nchini Uturuki na Syria tarehe 05/02/2023. Maelfu ya watu walikufa, maelfu wengine walijeruhiwa, na maelfu wengine walioponea walipoteza kila kitu kuanzia nyumba zao na vyote vilivyomo ndani, mbali na maelfu pia waliowapoteza ndugu zao, jamaa zao na kadhalika. Bila shaka ni mtihani na msiba wa kushtua sana. Unahitaji subra ya hali ya juu kabisa kuukabili.

Tetemeko kwa kweli linatisha na kuogofya sana. Wale waliolikabili wakiwa ndani ya majengo na hasa marefu, hao ndio kiukweli wanajua maana halisi ya tetemeko. Utakuta jumba lote linayumba pamoja na uzito wake wote, sauti kali ya vyote vilivyomo ndani ya nyumba vikigongana na kucheza huku na kule pamoja na mtikisiko wa ajabu. Tetemeko hili la Uturuki na Syria, ukubwa wake ni wa nyuzi 7 na nukta kadhaa hivi kwa kipimo cha Rechter, na athari zake ndizo hizo k**a zinavyoonekana kwenye vyombo vya habari. Sasa hilo la Qiyaamah litakuwaje?

Allaah Anatuambia:

"يَا أَيُّهَا النَّاسُ اتَّقُوا رَبَّكُمْ ۚ إِنَّ زَلْزَلَةَ السَّاعَةِ شَيْءٌ عَظِيمٌ • َوْمَ تَرَوْنَهَا تَذْهَلُ كُلُّ مُرْضِعَةٍ عَمَّا أَرْضَعَتْ وَتَضَعُ كُلُّ ذَاتِ حَمْلٍ حَمْلَهَا وَتَرَى النَّاسَ سُكَارَىٰ وَمَا هُم بِسُكَارَىٰ وَلَـٰكِنَّ عَذَابَ اللَّـهِ شَدِيدٌ"

“Enyi watu! Mcheni Rabb wenu, hakika zilizala la Saa (Qiyaamah) ni jambo kuu • Siku mtakapoiona, kila mnyonyeshaji atamsahau anayemnyonyesha, na kila mwenye mimba ataizaa mimba yake, na utawaona watu wamelewa, kumbe hawakulewa lakini ni Adhabu ya Allaah kali”. [Al-Hajj: 01-02]

Tukio k**a hili linapotokea, hakuna mtu anashughulika na mwingine. Analoangalia wakati huo ni kujiokoa mwenyewe kwanza. Katika Hadiyth iliyohadithiwa na Mama yetu ‘Aaishah, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema:

"يُحْشَرُ النَّاسُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ حُفَاةً عُرَاةً غُرْلاً ‏.‏ قُلْتُ: يَا رَسُولَ اللَّهِ، النِّسَاءُ وَالرِّجَالُ جَمِيعًا يَنْظُرُ بَعْضُهُمْ إِلَى بَعْضٍ؟ قَالَ صلى الله عليه وسلم: ‏"‏يَا عَائِشَةُ، الأَمْرُ أَشَدُّ مِنْ أَنْ يَنْظُرَ بَعْضُهُمْ إِلَى بَعْضٍ‏"‏ ‏.‏

“Watu watakusanywa Siku ya Qiyaamah wakiwa miguu peku peku, uchi wa mnyama bila nguo, hawajatahiriwa”.. Bibi ‘Aaishah alishtuka na kusema:

“Ee Rasuli wa Allaah! Na wanawake na wanaume wote watatazamana (nyuchi)! Rasuli akamwambia: Ee ‘Aaishah! Mambo yatakuwa ni magumu mno kuweza hata kuangaliana”. [Swahiyh Al-Bukhaariy (6527)]

Hawatoweza kuangaliana kutokana na kizaa zaa cha Siku hiyo, kila mtu roho juu juu akiifikiria nafsi yake tu, hata Mitume pia, isipokuwa Muhammad (Swalla Allaah ‘alyhi wa aalihi wa sallam) ambaye atakuwa anauombea umati wake badala ya nafsi yake. Tutafufuliwa bila kitu chochote, vyote tulivyokuwa navyo hapa duniani, tutakuwa tuliviacha tulipoiaga dunia, na tutarudi tena kwa Allaah k**a ile siku ya mwanzo Alipotuumba.

"كَمَا بَدَأْنَا أَوَّلَ خَلْقٍ نُّعِيدُهُ ۚ وَعْدًا عَلَيْنَا ۚ إِنَّا كُنَّا فَاعِلِينَ"

“K**a Tulivyoanza umbo la awali Tutalirudisha tena. Ni ahadi iliyo juu Yetu. Hakika Sisi Ni Wenye Kufanya”. [Al-Anbiyaa: 104]

Tukio hili ni nafasi kwetu ya kuwa tunakumbushwa. Ndugu zetu waliofariki walikuwa ndani ya majumba yao wakiwa katika hali ya usalama na amani. Lakini nyumba hizo hizo zikageuka ghafla na kuwa zana ya kuwatoa uhai wao. Ghafla bila kutarajia wamejikuta washahamia kwenye maisha mengine ya barzakh kusubiri baragumu la pili la Qiyaamah.

Wengi wetu tunakiona Qiyaamah k**a vile kiko mbali sana. La hasha! Kiko karibu sana kuliko tunavyodhania. Mtu unapokufa, basi Qiyaamah chako kidogo kishasimama, kwa maana unakuwa umeshaingia katika duara la kwanza la Qiyaamah la maisha ya kaburini ukisubiri duara la pili la Qiyaamah kikuu cha kufufuliwa na kutoka makaburini, na kisha yanayofuatia baada ya hapo. Tujiandae vyema kwa hayo yote.

Kwa faida zaidi JIUNGE na group letu la Facebook la UISLAMU CHAGUO LANGU na LIKE page yetu ya Facebook ya Islamic Swahili TV na TUTEMBELEE account yetu ya Facebook ya Al Furqaan.

Wabillaahi at-Tawfiyq.

IJUE SIRI KUBWA YA KUMSABBIH ALLAAH, NI MAAJABU ! KWA NINI HUFANYI TASBIYH ?Ukifuatilia suala la Allaah kusabihiwa kweny...
13/12/2024

IJUE SIRI KUBWA YA KUMSABBIH ALLAAH, NI MAAJABU ! KWA NINI HUFANYI TASBIYH ?

Ukifuatilia suala la Allaah kusabihiwa kwenye Qur-aan Tukufu, utakuta ajabu kubwa.

1- Utakuta kwamba “Tasbiyh” ina uwezo wa kuondosha Qadari ya Allaah. Katika kisa cha Nabiy Yuwnus ‘Alayhis Salaam, Allaah Anatuambia:

"فَلَوْلَا أَنَّهُ كَانَ مِنَ الْمُسَبِّحِينَ • لَلَبِثَ فِي بَطْنِهِ إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ"

“Na lau k**a hakuwa miongoni mwa wenye kumsabbih Allaah • Angelibakia tumboni mwake mpaka Siku watakayofufuliwa”. [Yuwnus: 143-144].

Alikuwa anasema katika kumsabbih Allaah:

"لا إِلَهَ إِلاّ أَنْتَ سُبْحَانَكَ إِنِّيْ كُنْتُ مِنَ الظَّالِمِيْنَ"

2- Utakuta kwamba “tasbiyh” ndiyo utajo ambao milima na ndege ilikuwa ikiitikia pamoja na Nabiy Daawuwd ‘Alayhis Salaam. Allaah Anatuambia:

"وَسَخَّرْنَا مَعَ دَاوُودَ الْجِبَالَ يُسَبِّحْنَ وَالطَّيْرَ"

“Na Tukatiisha milima iwe pamoja na Daawuwd ikisabihi pamoja na ndege”. [Al-Anbiyaa: 70]

3- “Tasbiyh” ni utajo wa viumbe vyote ulimwenguni; mbinguni na ardhini. Allaah Anatuambia:

"أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّـهَ يُسَبِّحُ لَهُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَالطَّيْرُ صَافَّاتٍ ۖ كُلٌّ قَدْ عَلِمَ صَلَاتَهُ وَتَسْبِيحَهُ ۗ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ بِمَا يَفْعَلُونَ"

“Je, huoni kwamba wanamsabihi Allaah walioko mbinguni na ardhini, na (pia) ndege wakiwa wamekunjua mbawa zao. Kila mmoja (Allaah) Amekwishajua Swalaah yake na tasbihi yake. Na Allaah Ni Mjuzi kwa yale wayafanyao”. [An-Nuwr: 41]

4- Zakariyyaa ‘Alayhis Salaam alipotoka mihrabuni kwake, aliwaamuru watu wake walete “Tasbiyh”. Allaah Anatuambia:

"فَخَرَجَ عَلَىٰ قَوْمِهِ مِنَ الْمِحْرَابِ فَأَوْحَىٰ إِلَيْهِمْ أَن سَبِّحُوا بُكْرَةً وَعَشِيًّا"

“Basi akawatokea watu wake kutoka mihrabuni, akawaashiria: Msabihini (Allaah) asubuhi na jioni”. [Maryam: 11]

5- Nabiy Muwsaa ‘Alayhis Salaam alimwomba Allaah Amfanye nduguye Haaruwn kuwa msaidizi wake atakayemsaidia katika kumsabbih Allaah na kumtaja. Anatuambia Allaah:

"وَاجْعَل لِّي وَزِيرًا مِّنْ أَهْلِي • هَارُونَ أَخِي • اشْدُدْ بِهِ أَزْرِي • وَأَشْرِكْهُ فِي أَمْرِي • كَيْ نُسَبِّحَكَ كَثِيرًا • وَنَذْكُرَكَ كَثِيرًا"



“Na Nifanyie msaidizi kutoka ahli zangu • Haaruwn, ndugu yangu • Nitie nguvu kwaye • Ili tukusabihi kwa wingi • Na tukudhukuru kwa wingi”. [Twaahaa: 29-34]

6- “Tasbiyh” ndiyo utajo wa watu wa Peponi. Allaah Anatuambia:

"دَعْوَاهُمْ فِيهَا سُبْحَانَكَ اللَّـهُمَّ وَتَحِيَّتُهُمْ فِيهَا سَلَامٌ"

“Wito wao humo ni: Utakasifu ni Wako ee Allaah. Na maamkizi yao humo ni Salaamun!” [Yuwnus: 10]

7- “Tasbiyh” ni utajo wa Malaika. Allaah Anatuambia:

"وَالْمَلَائِكَةُ يُسَبِّحُونَ بِحَمْدِ رَبِّهِمْ وَيَسْتَغْفِرُونَ لِمَن فِي الْأَرْضِ"

“Na Malaika wanasabbih na kumhimidi Rabb wao, na wanawaombea maghfirah walioko ardhini”. [Ash-Shuwraa: 05]

8- “Tasbiyh” imekuja kwa vitenzi tofauti katika Qur-aan.

(a) Cha wakati uliopita. Allaah Anasema:

"سَبَّحَ لِلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ"

“Vimemsabbih Allaah Pekee vilivyomo katika mbingu na ardhi, Naye Ndiye Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote”. [Al-Hadiyd: 01].

(b) Cha wakati uliopo. Anatuambia Allaah Ta’aalaa:

"يُسَبِّحُ لِلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ الْمَلِكِ الْقُدُّوسِ الْعَزِيزِ الْحَكِيمِ"

“Vinamsabbih Allaah Pekee vilivyomo katika mbingu na vilivyomo katika ardhi, Mfalme, Ametakasika na sifa zote hasi, Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote”. [Al-Jum-‘ah: 01]

(c) Kitenzi agizi. Allaah Ta’aalaa Anatuambia:

"سَبِّحِ اسْمَ رَبِّكَ الْأَعْلَى"

“Sabbih Jina la Rabb wako Mwenye ‘Uluwa Aliyetukuka kabisa kuliko vyote”. [Al-A’alaa: 01]

Vitenzi vyote hivi viko katika Aayaati za mwanzo za Suwrah. Na hapa bila shaka kuna siri kubwa.

9- “Tasbiyh” ni sababu ya kupata mambo ya kumridhisha na kumfurahisha Muislamu duniani na aakhirah. Allaah Anatuambia:

"فَاصْبِرْ عَلَىٰ مَا يَقُولُونَ وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ قَبْلَ طُلُوعِ الشَّمْسِ وَقَبْلَ غُرُوبِهَا ۖ وَمِنْ آنَاءِ اللَّيْلِ فَسَبِّحْ وَأَطْرَافَ النَّهَارِ لَعَلَّكَ تَرْضَىٰ"

“Basi subiri juu ya yale wanayoyasema. Na sabihi ukimhimidi Rabb wako kabla ya kuchomoza jua, na kabla ya kuchwa kwake. Na katika nyakati za usiku pia sabbih na katikati ya mchana, lazima utapata ya kukuridhisha”. [Twaahaa: 130] [Twaahaa: 130]

Na ili kuyapata hayo, Allaah Anatuhimiza hapa tumsabbih nyakati hizi tajwa na nyakati zingine zote.

10- “Tasbiyh” ni ponyo la dhiki ya kifua na kisaikolojia. Allaah Anasema:

"وَلَقَدْ نَعْلَمُ أَنَّكَ يَضِيقُ صَدْرُكَ بِمَا يَقُولُونَ • فَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ وَكُن مِّنَ السَّاجِدِينَ"

“Na kwa yakini Tunajua kwamba kifua chako kinadhikika kwa yale wanayoyasema • Basi sabihi na mhimidi Rabb wako na uwe miongoni mwa wanaosujudu”. [Al-Hijri: 97-98]

Angalia namna Aaayah hii inavyoelekeza namna ya kuondosha dhiki ya kifua na roho kwa ‘Tasbiyh”. Ukihisi hali hiyo, basi kimbilia kumsabbih Allaah, ni dawa ya ponyo.

Haya yote yanaonyesha siri kubwa iliyoko ndani ya “Tasbiyh”. Ulimwengu wote wa juu na wa chini, av yote vilivyomo humo vinamsabbih Allaah; kila kimoja kwa namna yake Anayoijua Allaah. Muislamu usije ukajitoa ndani ya duara hilo. Usije kuwa ndani ya kundi la walioghafilika. Ni amali rahisi kabisa ya ulimi isiyohitajia zana, wala wakati maalum wala sehemu maalum. Usipoteze nafasi hii muhimu.

Kati ya “Tasbiyh” bora kabisa na zenye malipo makubwa ni:

سُبْحَانَ اللهِ وَبِحَمْدِه عَدَدَ خَلْقِهِ وَرِضَا نَفْسِهِ وَزِنَةَ عَرْشِهِ وَمِدَادَ كَلِمَاتِهِ

Kwa faida zaidi JIUNGE na group letu la Facebook la UISLAMU CHAGUO LANGU na LIKE page yetu ya Facebook ya Islamic Swahili TV na FOLLOW Account yetu ya Facebook ya Islamic Swahili TV.

Wabillaahi at-Tawfiyq.

UKISEMA NENO AU KUSHIRIKI KATIKA MAUAJI YA MWIZI NAWE NI KATIKA WAUAJI MBELE ALLAAH TA'ALA.Ni mara nyingi tunashuhudia k...
12/12/2024

UKISEMA NENO AU KUSHIRIKI KATIKA MAUAJI YA MWIZI NAWE NI KATIKA WAUAJI MBELE ALLAAH TA'ALA.

Ni mara nyingi tunashuhudia kibaka akipata kipigo kikali kisha kuchomwa moto. Kila anayepita hapo na kuona tukio, naye haraka hujiunga kupiga na kutafuta haraka zana za kuchomea mtu huyo k**a tairi, mafuta, kiberiti na kadhalika bila kujua k**a ni mwizi kweli au la?

Kila anayepiga, na kila anayesaidia kufanikisha zoezi la kumchoma sawa sawa kwa neno, au kwa kitendo, basi hao wote wanakabiliwa na sh*taka la mauaji ya nafsi mbele ya Allaah Siku ya Qiyaamah, na pia kesi ya kutesa na kuua kwa kutumia moto.

Kuchoma mtu au kiumbe chochote hata wadudu ni jambo lililoharamishwa. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

"لا يُعَذِّبُ بالنَّارِ إلّا ربُّ النَّارِ"

“Hatesi kwa moto ila Mola wa moto”. [Hadiyth Swahiyh. Iko kwenye Al-Muhallaa (11/383)]

Na hata panya ukimk**ata kwa mtego, unachotakiwa ni kumuua haraka na kwa pigo moja tu. Usimkawize baada ya kumnasa, utazidi kumtesa kisaikolojia. Muue mara moja. Mauti yanatisha hata kwa wanyama! Usimchome wala kumzamisha kwenye maji. Haya ndiyo tunayoamrishwa na Dini yetu ya kutovuka mipaka iliyowekwa na Allaah na Rasuli Wake (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hali inakuwa vipi kwa mwanadamu!

Hivyo basi, ukisadifu kukutana na tukio k**a hilo, jipitie zako na njia zako. Usishiriki kwa lolote, utasalimika.

Kwa faida zaidi JIUNGE na group letu la Facebook la UISLAMU CHAGUO LANGU na LIKE page yetu ya Facebook ya Islamic Swahili TV na FOLLOW Account yetu ya Facebook ya Al Furqaan.

Wabillaahi at-Tawfiyq.

NI KIBURI KUREFUSHA NGUO YAKO, KATA KANZU AU SURUALI YAKO ,TAHADHARI NA MOTO.Kwa mafundi wa kushona Tsh. 500 tu inatosha...
10/12/2024

NI KIBURI KUREFUSHA NGUO YAKO, KATA KANZU AU SURUALI YAKO ,TAHADHARI NA MOTO.

Kwa mafundi wa kushona Tsh. 500 tu inatosha kukata hiyo kanzu Yako au Suruali uliyoivaa, Kwa nini muislamu hujaifikia hatua hii ya kupunguza hiyo nguo Yako ? Unaweza ukaona Msikiti mzima wa watu zaidi ya 100 wanaoswali lakini waliokata nguo zao au waliovaa Nusu muundi hawazidi 10, tena katika hao 10 miongoni mwao hawakuvaa kuburuza nguo kwa ajili ya Allaah Bali kwa sababu ya Mtindo mpya ya mavazi unaoitwa k**atia chini.

Mafundisho ya muislamu mwanamume kufupisha nguo yake ni ya kale sana na hakuna muislamu asiyeyajua, haya ni mafundisho ya Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi Wasallam), basi ni lini waislamu watafuata mafundisho haya ? Ni kiburi walichonacho baadhi ya waislamu hii leo kiasi Cha kupuuza na kutosikia juu ya makatazo ya kuburuza au kuvaa nguo ndefu ! Mtu anaridhika kanzu aishukilie au jeans aikunje lakini sio kukata. Kushusha Nguo Chini Ya Vifundo Vya Miguu Na Kuiburuza ni Kiburi Ni Haramu.

Ibn ‘Umar: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

"لَا يَنْظُرُ اَللَّهُ إِلَى مَنْ جَرَّ ثَوْبَهُ خُيَلَاءَ"

“Allaah Hamwangalii mwenye kuiburura nguo yake kwa kiburi na kujiona”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5784) na Muslim (2085)].

Abu Hurayrah: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

"لَا يَنْظُرُ اَللَّهُ يَوْمَ القِيَامَةِ إِلَى مَنْ جَرَّ إِزَارَهُ بَطَرًا"

“Allaah Hatomwangalia Siku ya Qiyaamah mwenye kuburuza kikoi chake kwa kiburi”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5788) na Muslim (2087)].

Hapa Rasuli amekufanya kule tu kushusha nguo chini ya vifundo ni kiburi na kujiona kulikoharamishwa. Hivyo basi, ujumbe hapa ni kuwa, kuteremsha nguo chini ya vifundo viwili vya mguu ni haramu, na afanyaye hivyo, atastahiki kuadhibiwa sehemu iliyo chini ya vifundo vya miguu miwili motoni (k**a ilivyoeleza Hadiyth ya Abu Hurayrah). Lakini pamoja na hivyo, kitendo hiki hakiingii ndani ya duara la madhambi makubwa ambayo yatamkosesha mtu kuangaliwa na Allaah Siku ya Qiyaamah isipokuwa tu k**a atakusudia kiburi na kujiona kwa kufanya hivyo.

Kwa faida zaidi JIUNGE na group letu la Facebook la UISLAMU CHAGUO LANGU na LIKE page yetu ya Facebook ya Islamic Swahili TV na FOLLOW account yetu ya Facebook ya Al Furqaan.

Wabillaahi at-Tawfiyq.

Address


Telephone

+255717277443

Website

Alerts

Be the first to know and let us send you an email when Islamic Swahili TV posts news and promotions. Your email address will not be used for any other purpose, and you can unsubscribe at any time.

Contact The Business

Send a message to Islamic Swahili TV:

Shortcuts

  • Address
  • Telephone
  • Alerts
  • Contact The Business
  • Claim ownership or report listing
  • Want your business to be the top-listed Media Company?

Share