17/01/2025
SHANGAZI*
Juzi kati nilipokuwa kwetu Kimbiji mara fulani niliketi na kaka mkubwa.
Tukikumbushana enzi za zamani vipindi vya njaa vilitutesa sana hadi kuchemsha mapapai, akanichekesha shemeji mama Husein akasema yeye aliwahi jaribu chemsha matango akakuta yanakuwa maji tuu hayakazi alidhani yatakuwa k**a maboga au mayungu.
Lakini ajabu kubwa kuna vipindi vya neema nyingi sana, Samaki na misimu ya samaki maalum, misimu ya matunda tofauti na misimu ya nafaka k**a mahindi na mpunga na mazao mengine.
Kwetu sijui zao gani hatujawahi kulima, hadi pamba. Zao ambalo hatukulima ni maharagwe na viazi mbatata ninavyokumbuka.
Maharagwe nimeanza kuona kilimo chake Arusha nilipokuwa kidato cha kwanza huko na mbatata nimeona kilimo chake nilipokuwa nikiishi Iringa.
Tukawakumbuka watu wa zama hizo wengine wameshafariki Allah awarehemu, wengine wahai.
Enzi zake si zangu kwa sababu ananizidi miaka 10 lakini zipo enzi zangu ambazo yeye alikuwa miongoni au zipo enzi zake ambazo mimi niliziwahi.
Tukamkumbuka shangazi yetu shakiki wa baba akiitwa mama Omar. Kaka akasema mimi nilikuwa sipendi kwenda kwa mama Omari nikiagizwa nalia njia nzima nilikuwa nina ugomvi naye. Ugomvi gani na shangazi yako? Nilikuwa nikienda kwake ananiita shangazi, sasa mimi mtoto wa kiume kuniita shangazi aaah alikuwa akinikera kwelikweli.
Hahahaha nikacheka alhamdulillah. Maana nami nilikuwa nakumbana na kadhia hii pia na ilikuwa yaniudhi kweli.
Hii ilikuwa kwa mashangazi zetu wote(binti Hamza) niliowawahi kasoro binti Hamza Mkubwa Mwafatima ndio alikuwa si mwenye kutuita shangazi.
Lakini, Mama Omari, mama Ussi, Mama Laki, Mama Mwazani, hawa ndio niliowawahi miye wote walikuwa wakituita shangazi.
Ukweli katika umri ule lilikuwa likinikera sana alhamdulillah. Ila mambo ni ya muda tuu na muda ukipita basi.
Si jambo hilo tu lilikuwa likinikera enzi hizo, yapo mambo kadhaa. Mfano nilikuwa nikikereka kuitwa Mwarabu, mzungu, zeruzeru. Wengine walidiriki kuniita Mwadawa kwamba nimefanana na dada yangu. Aaaah hii nayo ilikuwa kero kubwa sana. Ila ni utoto.
Lakini mara fulani ilikuwa ni kero mno mimi kuitwa Mzanzibari. Ilikuwa bora uniite msukuma ila sio kuniita Mzanzibari.
Ila sasa muda umefika nakuangalia tu, uniite utakavyo moyo hauumi wala sihangaiki kubadili kitu.
Si shangazi k**a shangazi zangu walivyokuwa wakiniita bali hata uite mama. Ukiniita Mzanzibari napenda pia, Buchu ulikuwa wapi bwana au ulienda kwenu Zanzibar nasema naam. Mmakunduchi, Kizimkazi, kijana wa mama Abdul. Sawa tuu.
Ukiita mzungu twende, mwarabu haya, zeruzeru nimoo, red indian okay.
Bali wapo wanaoniita DP world aaah nakataa sasa ndio miye mwenyewe.
*_Mambo mangapi unang'ang'ana kuyabadili, yanakuumiza yanakupa wakati mgumu. Yaache leo pumzisha moyo wako. Shida zao zisiwe zako._*
K**a ilivyo, *_Si kila haki ya mtu ni wajibu wako, si kila shutma zao ni shida zako_*
Muda ukipita mkaguane tena, maana muda hubadili mambo mengi sana.
*_Compromise_*
*_BuchuJr_*
Julai 12, 2024