17/08/2024
Reginald Mengi na safari ya ufukara mpaka utajiri
"Nimezaliwa katika umasikini wa kutupwa, lakini jambo hilo hata siku moja halikunikatisha tamaa," ni moja ya kauli ambazo Reginald Abraham Mengi alikuwa hacoki kuzisema kila alipopata wasaa wa kuzungumzia alipotokea maishani.
Reginald Mengi ni jina kubwa Tanzania na Afrika kwa ujumla, lakini wajua ametokea wapi.
Mengi alizaliwa wilayani Machame, Kilimanjaro, Tanzania mwaka 1942, akiwa mmoja wa watoto saba wa Bw Abhraham Mengi na Bi Ndeekyo Mengi.
"Familia yetu ilikuwa masikini sana, kila siku ilikuwa ni vita ya kupambana na umasikini. Tulimiliki sio zaidi ya ekari moja tukiishi kwenye vibanda vya udongo tukichanganyika na ng'ombe wachache na kuku. Ninaporudisha fikra na kutazama nyuma ni vigumu napatwa na ugumu wa kufikiri namna tulivyoweza kuishi katika hali ile," alipata kusema kwenye uhai wake.
Alianza safari yake kielimu shule katika shule ya msingi Kisereny Village Bush School, kisha akajiunga Nkuu District School, kisha Siha Middle School, na baadaye Old Moshi Secondary School. Kwa ufadhili wa Chama cha Ushirika kilichokuwa na nguvu ya kifedha ushawishi KNCU Mengi alisomeshwa masomo yake ya shahada ya kwanza ya uhasibu nchini Uingereza.
Baada ya masomo ughaibuni, Mengi alirudi Tanzania 1971 na kuajiriwa na kampuni ya Cooper and Lybrand Tanzania ( sasa Prince water house Cooper) mpaka mwaka 1989 alipoamua kujikita kwenye ujasiriamali
Baada ya kuachana na ajira, Mengi aliiboresha kampuni yake ya Industrial Projects Promotion Limited na baadae kufahamika zaidi k**a IPP Limited.
Kupitia IPP Limited Mengi alaianzisha kampuni mbalimbali na kufanya biashara kadha wa kadha kuanzia uzalishaji wa sabuni, soda, maji ya kunywa, madini, mafuta, gesi asilia na kilimo.
Hata hivyo, umaarufu mkubwa wa Mengi ni kutokana na kumiliki vyombo vya habari, kuanzia magazeti, vituo vya runinga na redio. Runinga yake ya ITV pamoja na kituo cha Redio One ni moja ya vituo vikubwa vya utangazaji huku magazeti yake ya Guardian na Nipashe yakiwa miongoni mwa magazeti makubwa zaidi Tanzania.
Mpaka umauti unamfika, Mengi alikuwa Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vyombo Vya Habari Tanzania.
Mengi pia amekuwa akijitoa katika kusaidia wasionacho na wenye uhitaji kwenye jamii ikiwemo walemavu wa ngozi na kugharamia matibabu ya watoto wenye matatizo ya moyo nchini India.
Mwaka 2014, jarida maarufu la masuala ya fedha Forbes lilikadiria utajiri wa Mengi kuwa unafikia Dola milioni 560.
Mjane wa Mzee ni Jacqueline Ntuyabaliwe ambaye alipata kuwa Miss Tanzania mwishoni ma miaka ya 90.