05/01/2026
Halmashauri ya Wilaya ya Geita imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 500 kwa vikundi maalum vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani, kwa lengo la kuwawezesha kiuchumi na kuboresha maisha yao.
Hafla ya kukabidhi mikopo hiyo imefanyika katika viwanja vya Halmashauri ya Wilaya ya Geita, ikiongozwa na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Geita, Bi. Janet Mobe.
Akizungumza katika hafla hiyo, Bi. Mobe amewataka wanavikundi waliopata mikopo hiyo kuitumia kwa malengo yaliyokusudiwa, kufanya kazi kwa bidii pamoja na kurejesha kwa wakati, ili kutoa fursa kwa vikundi vingine kunufaika na mikopo hiyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Mheshimiwa Paschal Mapung’o, amewakumbusha wanavikundi umuhimu wa matumizi sahihi ya fedha hizo, akisisitiza kuwa mikopo hiyo ni chachu ya maendeleo endapo itatumika kwa uangalifu na nidhamu ya hali ya juu
Naye Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Bw. Jonas Kilave, ameeleza kuwa zaidi ya vikundi 200 viliomba mikopo hiyo, ambapo baadhi vilikidhi vigezo na kupata mikopo huku vingine vikishindwa kukidhi masharti na hivyo kutopata kwa awamu hii
Baadhi ya wanavikundi waliopata mikopo hiyo wameeleza kufurahishwa na hatua hiyo, wakiahidi kufanya kazi kwa bidii, kuendeleza miradi yao na kurejesha mikopo kwa wakati ili na vikundi vingine vipate nafasi ya kunufaika