25/07/2023
Mwaka Mpya wa Kiislamu Zanzibar:
Rais Dr. Mwinyi aweka Historia
• Ofisi ya Muft ZNZ yasema Historia itamkumbuka
Na Bakari Mwakangwale
KALAMU zimeandika na historia itamkumbuka Rais wa Zanzibar Dr. Husein Ali Mwinyi, kwa kuipitisha Siku ya Mwaka Mpya wa Kiislamu Hijiriyya, kuwa ni Sikukuu ya Kitafa Zanzibar.
Hayo yameelezwa na Katibu Mtendaji Ofisi ya Muft Mkuu wa Zanzibar, Alhaj Khalid Mfaume, akiongea Visiwani Zanzibar, katika maadhimisho ya Mwaka Mpya wa Kiislamu, 1445H.
Rais Dr. Mwinyi, ameitangaza siku ya Hijiriyya (mwaka mpya wa Kiislamu) kuwa ni siku ya Sikukuu Kitaifa kwa Zanzibar, kwa mamlaka aliyopewa Kikatiba chini ya kifungu 6 (1) (a) cha Sheria ya Masuala ya Rais wa Zanzibar, Namba 3 ya Mwaka 2020, hivyo kuwa ni siku rasmi ya mapumziko inayotambulika na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Kwa maana hiyo Alhaj Mfaume alisema, sasa Zanzibar ni nchi ya kwanza kwa Afrika, inayo adhimisha Mwaka Mpya wa Kiislamu kwa utaratibu huu kwa siku hiyo ya Mwaka Mpya kuwa ni siku inayotambuliwa rasmi na Serikali na kuwa ni siku ya mapumziko.
“Tunampongeza Rais Dr. Mwinyi, kwa kuikubali Siku ya Mwaka Mpya wa Kiislamu (Hijiriyya) kuwa ni siku ya mapumziko jambo hili linadhihirisha wazi kuwa Mh. Rasi (Dr. Mwinyi) ni kiongozi msikivu na ni kiongozi mwema.”
“Na kwa jambo hili jema alilolifanya kalamu zimeandika, na historia itamkumbuka siku zote na Allah (s.w) atampa fungu lake, kwani hatuna uhakika lakini kwa taarifa tulizonazo ni kwamba Zanzibar ni nchi ya kwanza kwa Afrika, inayoazimisha Mwaka Mpya wa Kiislamu, kwa utaratibu k**a huu na siku hiyo kuwa ni siku ya mapumziko inayotambuliwa rasmi.” Amesema Alhaj Mfaume.
Alhaj Mfaume alisema, shughuli za Mwaka Mpya wa Kiislamu, zimeanza kuadhimishwa rasmi Mwaka jana 1444H, sawa na Mwaka 2022, hapo Visiwani Zanzibar.
Alisema, katika maadhimisho hayo ndipo fikra ya kuanzisha maadhimisho ya Mwaka Mpya wa Kiislamu Zanzibar, kila Mwaka ikapatikana lengo likiwa ni kurudisha urithi na nidhamu iliyoachwa na Wanazuoni na Msheikh wao waliotangilia mbele ya haki katika kuadhimisha siku hii.
“Mwaka 1444H, sawa na Mwaka 2022, Ofisi ya Muft Mkuu wa Zanzibar, iliandaa maadhimisho ya Mwaka Mpya wa Kiislamu kwa mara ya kwanza kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii.”
“Tulichangia Damu Salama, tulitembelea wagonjwa kisha tulifanya Kongamano la kuukaribisha Mwaka Mpya wa Kiislamu, katika Kongamano hilo ndipo tuliomba mapunziko katika siku hii muhimu katika historia ya Uislamu.” Amesema Alhaj Mfaume.
Alisema, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba na Sheria Utumishi na Utawala Bora, aliwasilisha ombi hilo, ndipo ikapelekea Mh. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Dr. Hussein Mwinyi, kupokea mapendekezo hayo na kuufanya Mwaka Mpya wa Kiislamu kutambuliwa na kuwa ni siku ya mapumziko.
Alhaj Mfaume alisema, maadhimisho hayo yamekuwa na ratiba ya kutanguliwa na shughuli mbalimbali ndani ya wiki nzima lengo likiwa ni kuitangaza na kuitambulisha Kalenda ya Mwaka Mpya wa Kiislamu, haswa kwa vizazi vya sasa kwani haifahamiki kwa wengi pamoja na kuhimiza maadili mema Visiwani Zanzibar.
“Ofisi ya Muft Mkuu wa Zanzibar, imeona ipo haja kubwa ya kuipa hadhi siku hii ili Waislamu wa Zanzibar waijue Tarekh yao ya Kiislamu, ukizingatia kuwa Zanzibar ni nchi yenye Historia kubwa ya Elimu ya Dini, kwani hata baadhi ya nchi za Afrika walikuwa wakifika kusoma Zanzibar kwa Wanazuoni wakubwa waliokuwepo.” Amesema Alhaj Mfaume.
Alisema, katika kuelekea maadhimisho ya Mwaka Mpya 1445H, Ofisi ya Muft Mkuu wa Zanzibar, iliandaa matukio mabalimbali ya kijamii kabla ya kufikia kilele cha Maadhimiosho hayo.
Aliyataja matukio hayo kuwa ni kuweka kambi maalum ya matibabu ya macho, ambayo ilifanyika Mwezi 25, Dhul Hijja (sawa na Julai 14, 2023) katika Hospitali ya Kivunge, Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Katika kambi hiyo wagonjwa wa macho 560, wamepatiwa dawa, wagonjwa 440, wamepatiwa Miwani ya kusaidia kuona na kusomea na wagonjwa 356, wamefanyiwa upasuaji wa kuondoa mtoto wa jicho na wanaendelea vizuri.
Alisema tukio lingine lilikuwa ni maonyesho ya Kiislamu na Biashara Zanzibar, yaliyofanyika Mwezi 25 Dhul Hijja (sawa na Julai 14, 2023).
Katika maonyesho hayo, Taasisi mbalimbali zimeweza kushiriki zikiwemo Taasisi za Serikali, Dini, Hijja, Vyuo Vikuu vya Kiislamu Zanzibar, pamoja na Taasisi za kusaidia jamii za Kiislamu.