15/01/2024
PANGO
Kongole kuniumiza, pango nakusema heko,
Kwa dhati umeniliza, kunicharaza kiboko,
Machungu nimeyameza, najiona mbwa koko,
Pongezi kuniumiza, uhuniwo endelea.
Endelea kuchukiza, mama yangu yuko huko,
Kwa kishindo limumeza, kwa kupinga tabya zako,
Kisiri kamwangamiza, tusijue na aliko,
Pango unatumaliza, yu wapi mjomba naye?
Naye ulimuingiza, tunduni wewe uliko,
Fununu wanotembeza, walio shabiki wako,
Ni kwamba limumaliza, hupendi pinzani kwako,
Sifa zako kupoteza, weye hutaki Yarabi!
Yarabi watuumiza, tusaze si’ tulioko,
Tutakuja kuuguza, tupunguze mfumuko,
Kibaba tuje kijaza, kidogo kidogo tuko,
Pango tutakuongoza, ujawe nyingi afia.
Afia kututumuza, ikupe misuli yako,
Ambayo wamenyofoza, kukuacha huna lako,
Basi acha kuniliza, najua wakuchimbako,
Pango umeniumiza, watuua watu wako.